Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nitazungumzia kidogo tu mambo yanayohusu kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni ya Kamati kuhusiana na zao la chai ni maoni ambayo yapo very clear, yanaeleza jinsi gani wawekezaji wameweza kununua mashamba makubwa na kuyatelekeza bila kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tabia hii siyo njema kwa sababu kama mwekezaji alifikiri anaweza akaifanya biashara, amefanya utafiti wa kina kwa ajili ya kufanya biashara ya chai. Anaposhindwa, ninaamini Mheshimiwa Bashe, kama wenzangu walivyomsifia, ni mtu makini, ni mtu anayesikiliza. Basi wangerudisha kwenye Wizara na kusema tumeshindwa kuendelea na zao la chai, tunaomba tupate mwekezaji mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 31 Mei, mwaka 2024 Mheshimiwa Bashe alituita wadau wa chai wote, akatoa angalizo na akatoa onyo kwamba kiwanda cha Chai cha ROTCO kilichopo Rungwe kisifungwe mpaka ambapo wananchi watakaa kwa muda na kuhakikisha wale watu wameandaliwa; maana chai zinachumwa kila siku, lakini mwekezaji huyu akaendelea kufunga kiwanda. Leo hii tunaongea mashamba yale yamefungwa, wafanyakazi zaidi ya 300 hawana kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyofahamu, ni kweli kwamba tunatakiwa kuwa na mazingira mazuri kwa wawekezaji, ni lazima tuwalinde wawekezaji, lakini mwisho wa siku lazima tuwalinde wananchi ambao chai hii wameilima tangu sisi tukiwa wadogo mpaka sasa tumekuwa wazee. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, Mheshimiwa Bashe ni mtu mwema sana na wamemsifia, na katika maeneo mengi amefanya kazi nzuri sana, lakini kwa suala la Rungwe naomba aje mwenyewe, asitume mtu. Aje yeye mwenyewe. Mimi kila siku nagombana naye, ninamshirikisha anatuma Tume, anatuma Bodi. Bodi inakwenda pale, sijui inakuwaje wanarudi na mambo bado yanakwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba anajua namna ya kuwalinda wawekezaji, kwa sababu ni ukweli kwamba tunaruhusu wawezaji waje na watusaidie. Basi kama ni hivyo, huu uwekezaji ameshindwa, tunaomba watuletee wawekezaji wengine ili wananchi wale waendelee kuuza chai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mashamba ya chai yamekuwa na nyasi. Leo hii ukienda ile njia ya Bujela kuelekea Masukulu chai imekufa, viwanja vimekufa kabisa. Kulikuwa kuna nyumba pale, zimekwisha kabisa. Ina maana ajira ya Wana-Rungwe pale haipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bodi ya Mheshimiwa Bashe iende. Naomba Naibu Waziri aende, wasitume mtu mwingine kufika pale zaidi ya wao watu wawili. Najua maeneo mengine amemaliza, lakini kwetu bado hajamaliza. Tunaomba suala la chai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala parachichi limekuwa ni kilio cha kila siku ambacho tunazungumza hapa. Mwenzangu wa Lupembe ametoka kuzungumza hapa. Tunaiita dhahabu ya kijani. Ni kweli tumetoka kwenye mafungo ya 100 zote sasa hivi tunakwenda angalau kwa shilingi 1,800/= hadi shilingi 2,000/= kwa kilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri asiziachie halmashauri zipange bei, kwa sababu halmashauri zikipanga bei Halmashauri ya Njombe inapanga bei ya chini, halmashauri nyingine inapanga bei nyingine. Naomba aunde Bodi ya zao hili, kwa sababu zao hili ni la kimkakati kwa sasa. Basi ahakikishe kwamba Wizara inatoa mapendekezo ya bei zinazofanana, labda itafanya madalali wanunue maparachichi kote na kutokununua sehemu nyingine na kukimbia kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wananchi wanalalamika kwamba wanunuzi wachache ndio wanaoenda kununua wengine hawajanunua. Ni kweli amefanyia kazi siku mbili hizi, lakini wiki mbili za nyuma zilizopita parachichi zimeoza. Wanunuzi walikuwa hawaendi, ni KUZA peke yake alikuwa anaenda, naye anafanya masharti. Anataka mkulima atoe parachichi shambani, ampelekee kiwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kata 29, ni mkulima gani ana uwezo wa kubeba tani tano au sita kwenda kumpelekea kiwandani? Nashukuru hilo amelifanyia kazi siku mbili hizi, lakini kwa msimu unaokuja namwomba Mheshimiwa Waziri, kila mnunuzi afuate zao shambani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, wale ambao hawajaja kununua bila kutoa taarifa wachukuliwe hatua. Kama waliona parachichi zitakuwa bei, na wao haiwalipi, nafahamu kwamba nao ni wafanyabiashara, lakini kwa nini hawajatoa taarifa kwamba hatutanunua msimu huu ili Wizara iweze kutafuta alternative nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaumia. Naomba Mheshimiwa Waziri mwenyewe ndio aje. Ninaamini Waziri akija na akaongea na wakulima wote, akaweka kikao nao bila kupitia watu wa Katikati, atakuwa amewasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la madalali. Madalali wamekuwa ni watu wabaya sana wanaopita katikati. Tunaomba kabisa wale wawekezaji au wanunuzi waje wenyewe na wala sio madalali. Dalali anakuja shambani anasema, ‘reject’. Kwenye tani moja, nusu tani ni reject, kwa macho yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kuna Maafisa Ugani wanajitahidi, kwani juzi wameweza kukamata hata mizani ambayo siyo mizuri. Kwa hilo, nawapongeza, lakini naomba msimu ujao tujipange kama timu, tuhakikishe tunawasaidia wananchi hawa waweze kupatiwa kile wanachohitaji, kwa sababu mwisho wa siku mkulima analima na anapanda mwenyewe, basi apate kile kidogo anachokipata kwa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi ya kusema zaidi ya hayo, ninaamini Mheshimiwa Bashe atasimamia hilo na atafika sehemu husika ili kuweza kuwasaidia ndugu zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba alisimamie hili na ninaamini atalifanyia kazi, ahsante. (Makofi)