Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Kamati yangu ya Kilimo, Biashara, Viwanda na Uvuvi. Unajua hii sekta inabeba kila kitu mpaka unashindwa hata uanzie wapi kwa sababu inabeba uchumi wa nchi na maisha ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kumpongeza sana Rais wangu kwa kuteuliwa tena na Chama hiki kuwa Rais atakayetuongoza tena katika miaka mitano. Ninaamini aliyoyafanya katika miaka mitano hii, basi nchi hii inaenda kuwa ya asali na maziwa katika miaka mitano mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza sana Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea kwa maana ya Makamu wa Rais wa nchi hii na pia Rais wa Zanzibar kuendelea tena kushika bendera ya kukiongoza chama chetu kwa Urais wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo, nitagusa jambo la watumishi. Umesikia Wabunge wengi hapa wanalalamika kuna vitu kama vituo vya kilimo vimebadilishiwa matumizi na mambo mengi hayaendi. Hii ni kwa sababu hatuna watumishi wa kutosha wa kilimo. Kama tungekuwa tuna watumishi wa kutosha, nina hakika hata hivi vituo vyetu visingechukuliwa kwa sababu wangekuwepo wafanyakazi wa kutosha ambao wangehakikisha kwamba hivi vituo vinafanya kazi. Serikali yetu inapambana sana na suala la watumishi. Kupanga ni kuchagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba waalimu ni muhimu sana…
MWENYEKITI: Samahani Mheshimiwa Mtinga, subiri kidogo.
Waheshimiwa Wabunge, upande wangu wa kushoto kuna kelele sana. Samahani kidogo Mheshimiwa, endelea.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua. Ajira katika nchi yetu bado ni tatizo sehemu nyingi, lakini tunaishukuru Serikali inajitahidi sana kwa walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye kilimo, kwanza ndiyo mwajiri mkuu wa nchi, lakini pia kilimo ndiyo kinasababisha tuweze kuishi kwa sababu ya chakula. Ni kweli Serikali inaweza kuwa inahangaika sana kwenye shule moja ndani ya Kijiji, kuwe na waalimu angalau 10 au saba, lakini angalau kungekuwa kuna Afisa Kilimo mmoja tu kwenye kila kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zipo karibu kila kijiji. Tunahangaika, tunakuwa tuna waalimu 10 au saba, lakini tumesahau kuwa Afisa Kilimo angalau mmoja tu angekuwepo kwenye kila Kijiji, akatoa elimu ya kilimo chenye tija kwa wakulima wetu, tutabadilisha sana uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu, pamoja na kuwa bado tuna umuhimu sana na ajira nyingine, basi iangaliwe kwenye kilimo angalau Afisa Kilimo mmoja kwenye kila kijiji afundishe wale wakulima ambao wengi wao wakishamaliza, hata shule wanabaki pale pale kuwa wakulima. Kwa hiyo, tukiwa na Maafisa Kilimo kwenye kila kijiji ambao watafundisha wakulima wetu kulima kwa tija katika maeneo yao madogo, tutafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumetangazwa kuwa wa pili Afrika kulisha mahindi, lakini kwa kilimo cha kawaida sana cha wananchi wetu wa kijijini ambao wanajihangaikia wenyewe, hawana hata Maafisa Ugani wa kutosha. Je, tukiwapata Maafisa Ugani kwenye kila kijiji wakawafundisha wakulima wetu kutumia maeneo yao madogo ya ekari mbili, tatu au nne kwa tija, tutakuwa wapi? Tutalisha dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali, najua ikama na mambo ya fedha, lakini hebu tuangalie suala la kuajiri Maafisa Ugani kwenye kila kijiji na wafanye kazi. Resources tayari tunazo kwenye kila kata, kama tunavyosema, ni nyingi, lakini wakiwepo hawa watu, na wakafuatiliwa kufundisha wakulima wetu, nina hakika tutafika mbali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo mbinu za kufundisha wakulima wetu hata kuchanganya mazao. Ukienda kwenye jimbo langu utakuta kwenye shamba la ekari mbili la mkulima, kuna miti mingi ya kawaida tu. Ukimwuliza ya nini? Anakwambia ya kuni. Kama wangepata wataalamu wa kilimo, wakawaambia, basi badala ya kuni kwenye ekari mbili hizo, wangeweka hata miembe 200 tu badala ya kuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo miembe 200 inaweza kumpatia shilingi milioni 50 kila mwaka, lakini ni kwa sababu hajui, hajaelekezwa. Maana akipanda miembe, bado atalima mahindi yake kwenye shamba lile lile kwa sababu miembe 200 kwenye ekari mbili, ni upana karibu wa mita kumi kutoka mwembe hadi mwembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wangekuwa wameelekezwa, akalima miembe badala ya kuacha miti ya kuni, angekuwa anapata over 50 milions kila mwaka kwa zao lile la embe, wakati bado analima mahindi yake ambayo amezoea kwenye shamba lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa wataalamu kuwepo ili kubadilisha fikra za wakulima wetu ni jambo la msingi sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie katika umuhimu wa ajira inazotoa kila mwaka. Suala la Maafisa Kilimo ni la msingi sana. Hii itakwenda, wakishaajiriwa hawa, wawe na mwangalizi wa karibu ambaye ni mamlaka ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kwa halmashauri siyo kipaumbele kabisa, yaani halmashauri wanawajua wakulima wakati wa kudai ushuru tu. Wakati wa ushuru, mageti mengi, kila njia wakidai hela ambazo hawakushiriki hata kidogo katika kumsaidia mkulima kulima lile shamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiki kilimo kikiwa na mamlaka yake ambayo itamjali huyu mkulima, basi hata hizo halmashauri zitaupata huo ushuru zaidi ambao zinaupenda sana wakati wa mavuno, lakini wakati wa kumsaidia mkulima hamna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zetu zinahangaika sana na waalimu, zinahangaika na manesi, hujawahi kusikia zinahangaika na mkulima. Hata kama kuna Afisa Kilimo mmoja au wawili kwenye kata, wanapewa majukumu mengine; hukaimu Ofisi ya Kata au anakaimu Utawala. Kwa hiyo, wakulima wanakuwa wameachwa, kitu ambacho ndiyo uti wa mgongo hata wa hizo halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili suala la mamlaka ya kilimo ni la muhimu sana. Sehemu zote ambazo tumeweka mamlaka tumefanikiwa. Tumeweka TARURA tumefanikiwa, tumeweka RUWASA tumefanikiwa na tumeweka TANROADS tumefanikiwa. Hebu sasa tugeukie kwenye kilimo tuweke mamlaka, hili jambo ambalo ndiyo uti wa mgongo wa nchi hii, nina hakika tutafanikiwa kiasi kikubwa na tutailisha dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la mamlaka pia liende pia kwenye suala la uvuvi. Sekta za Uvuvi na Mifugo ni kubwa sana. Kwenye mifugo kuna sekta ndogo ya maziwa ambayo ni kubwa sana, kuna sekta ndogo ya nyama ambayo ni kubwa sana, na kuna sekta ndogo ya ngozi ambayo pia ni kubwa. Haya yote yangefanyiwa kazi yangebadilisha kabisa uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaimba tu kila siku kuwa tuna mifugo, wa pili Afrika, lakini hamna chochote ambacho tunafanya. Ni kwa sababu Sekta ni kubwa. Sasa njoo kwenye uvuvi; kuna wa bahari kuu, kuna wa maji baridi, kuna ufugaji wa samaki unakuja kwa kasi. Hizi zote ni sekta kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Rais wangu, ikibidi hii Wizara ya Mifugo ibaki kuwa Wizara kamili na Uvuvi iwe Wizara kamili, kwa sababu hivi ni vitu vikubwa ambavyo vinaweza kubadilisha kabisa uchumi wa nchi hii. Ukienda huko halmashauri ndiyo kabisa. Eti unakuta Mkuu wa Idara ya Mifugo na Kilimo ni mmoja na wakati vitu vyenyewe hivi ni vipana kweli kweli, akiwa amesomea kilimo, habari ya mifugo anasahau; akiwa amesomea mifugo, habari ya kilimo anasahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba na TAMISEMI, kwanza mwongozo uende kabisa, hii Idara ya Kilimo na Mifugo zirudi kuwa Idara tofauti na Wakuu wa Idara yake tofauti, kwa sababu ni vitu vikubwa vinavyoshikilia uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, namwomba sana Rais wangu, atenganishe hii Wizara, pia halmashauri kule Idara ziwe tofauti na mamlaka ya Mifugo na Mamlaka ya Uvuvi, zianze kwa mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, mtaona jinsi nchi hii itakavyobadilika kwa sababu ndiyo fursa ambayo imeshikilia uchumi wa nchi, imeshikilia maisha ya Watanzania na kila kitu ambacho kitaenda vizuri kabisa katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umeshika hiyo mic yako, lakini yalikuwepo mengi ya kusema. Naomba haya ya mamlaka yafanyiwe kazi, kwani yatatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)