Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo niweze kuchangia kwa uchache ripoti ya Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunipatia kibali saa hii. Pia, napongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo vinafanya kazi kwa uzalendo na weledi mkubwa vikiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko yote, Mwenyekiti wetu wa Kamati ambaye kwa kweli amekuwa akituongoza kwa umakini mkubwa, Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama ambaye kiukweli amesimama kidete, Bunge limekuwa imara, tunamwombea Mwenyezi Mungu ampe heri na miaka mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita kwenye usafiri wa bodaboda na ulinzi na usalama wa Taifa letu. Tutakubaliana sote, kama sio sisi, ni watoto wetu, ni jamii, ni watu waliotuzunguka wanatumia bodaboda kama usafiri rahisi na kuwafikisha mahali haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodaboda na bajaji ni 70% ya vyombo vyote vya usafiri nchini. Yaani ukichukua vyombo vyote ukajumlisha, 70% ni bodaboda na bajaji. Kwa hiyo, wigo huu ni mpana sana, lakini hakuna mchango unaopatikana kwenye bodaboda au bajaji. Mchango wake ni mdogo na tija kwa Taifa ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodaboda ndiyo wanaoongoza kwa ajali nchini, ndiyo wanaoongoza kwa ulemavu nchini, ndiyo wanaoongoza kwa kukaa hospitali kwa muda mrefu na hivyo Serikali kutumia fedha nyingi sana kutibu watu hawa. Ni kwa sababu hawajawekewa utaratibu mzuri. Bodaboda hawana maegesho maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya, na Kamati ililiona kwa sababu kuna watu wasio na nia njema wanatumia mlango ulio wazi wa bodaboda kufanya uhalifu. Niseme tu, vijana wetu wa bodaboda hawawezi kuwa wahalifu, lakini wapo watu wanaingia kwenye ule mwanya wa bodaboda, wanafanya uhalifu; wanapora, wanaiba, wanafanya vitu vigumu kabisa na kuhatarisha usalama wa watu na mali zao, lakini linaitwa jina la pamoja “bodaboda”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa mashahidi, wengi wetu tumepanda bodaboda, wapo ma-graduate ambao ni bodaboda, degree holders bodaboda wapo hapa wanafanya biashara na wanaweza kujikimu. Unaweza kuona hii Sekta ni pana namna gani? Sekta hii haijawekewa mwongozo maalum ili uweze kukidhi mahitaji ya bodaboda wenyewe, lakini na jamii kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri, tukasema Serikali isimame kidete, ishirikiane na LATRA, Mamlaka ya Miji, Wilaya, iweze kujenga mfumo wa kisasa wa kidijiti wa kuweza kufanya utambuzi wa bodaboda wote nchini. Huu mfumo uwe wa Kitaifa. Mfumo huu ukiwa wa Kitaifa unaweza kupunguza athari hasi…

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Felista kuna taarifa, unaweza ukaketi. Mheshimiwa Ighondo.
TAARIFA

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa mzungumzaji taarifa kwamba, hayo anayoyazungumza, nchi ya Rwanda wamefanikiwa sana kudhibiti ajali za barabarani na mfumo usio wa kiholela wa bodaboda kwa kuzingatia kusimamia sheria na pia kutumia mfumo wa kidijiti. Kwa hiyo, nchi yetu pia inaweza kwenda kujifunza kule ili hoja ya mzungumzaji ilete tija kwenye nchi yetu, ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Ighondo. Mheshimiwa Felista unaipokea taarifa?

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa heshima kubwa, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweka mifumo thabiti tutaiheshimisha sekta hii ambayo inaonekana ni ya kawaida. Hata hivyo, katika Taifa letu, ni zaidi ya vijana 800,000 kwa mwaka wanahitimu vyuo vikuu na sekondari, lakini hawana ajira. Katika hawa vijana, 54% kila mwaka wapo tu mtaani, hawafanyi chochote. Tukiirasimisha sekta hii, tukaweza kuiwekea mipangilio, tutakwenda kuzalisha kitu kikubwa, na Serikali itapata mapato, na vijana wetu watasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodaboda sasa hivi ni kama maji, usipooga utakunywa, usipokunywa utapikia. Kila tunapopita tunakutana na bodaboda, watoto wetu wanapanda bodaboda, tuurasimishe mfumo huu ili tuweze kusaidia Serikali ipate mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nayazungumza haya ili tuone tija ya sekta hii. Katika Taifa letu, kidunia tumekuwa wa kumi ambapo vijana wetu wengi hawana ajira. Tukiirasimisha hii sekta, tunaweza tukapata ajira na vijana wetu wakakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili lichukuliwe kwa u-serious wake, lakini kuna watu ambao sio waendesha bodaboda, ni wamiliki wa bodaboda. Hawa wamiliki nao warasimishwe ili wajulikane. Unapoenda kupanda bodaboda umtambue huyu ametoka wapi? ID number yake, anapaki kituo gani? Wilaya yake ni ipi? Hii ni kwa usalama wa Taifa letu na nchi yetu, ili kuweza kukinga watu wenye nia mbaya wa kwenda kulichafua Taifa kupitia mwanya huu wa bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo nasema, kama Taifa tukiazimia kufanya jambo, tukaliweka hapa, tutafanikiwa. Mheshimiwa Bashe amefanikiwa sana kwenye Sekta ya Kilimo. Tusipoongea sisi, mawe yataongea. Mheshimiwa Bashe amefanikiwa kwa sababu amekuwa serious, ameyachukua mambo kwa uzito wake, ameyatekeleza. Hili nalo lichukuliwe namna hiyo ili tuweze kwenda nalo kwa tija ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo nina msiba mkubwa wa JKT. Inawezekana wale wenzetu kwa sababu ni askari wazalendo, hawawezi kwenda front kudai haya madeni; shilingi bilioni 40 ni msiba, ni kilio. Tulisema tutasaida wakandarasi wetu wa ndani. SUMA JKT ni wakandarasi wa ndani wanaopambana, wa viwango vinavyotosha, lakini mitaji yao ni duni, imekaa kwa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta za Kiserikali na sekta binafsi hawalipi pesa zao. Wamedai mpaka wamekuja kwenye Kamati. Tunapandisha sauti kwamba yeyote anayedaiwa na JKT, walipe fedha hizi, na wazilipe haraka kwa kuwa wale hawawezi kuandamana, hawawezi kunung’unika, wale ni wazalendo, sauti yao ni sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili lichukuliwe kwa u-serious mkubwa. Katika hili, tumeshindwa kufanya mambo makubwa. Tulienda Misri, tuliona namna gani majeshi yanavyochangia pato la Taifa zaidi ya 45%. Tukiwezesha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa uzalendo wanaouonyesha, kwa tija wanayoionyesha, Taifa hili litakwenda next level. Niwaambie, tusichukulie blah blah kwa sababu ni wenzetu, tulipe madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)