Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kidogo. Mchango wangu utajikita kwenye huu upande wa ulinzi na usalama, na vile vile kwenye suala zima la uvuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuishukuru Serikali kwa juhudi kubwa ambazo inafanya hasa katika kuzuia huu uvuvi haramu. Kule Musoma kusema ukweli suala la ziwa, hasa Ziwa Victoria limekuwa likitusaidia sana katika kipindi cha zamani, kwa sababu ndiyo lilikuwa msingi wa uchumi wa miji yetu yote iliyoko pembezoni mwa Ziwa Victoria. Kwa bahati mbaya samaki tuliokuwa tunawategemea hawapo, viwanda vyote vimekufa na hii ni kwa sababu ya uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Serikali inajaribu kufanya juhudi kwa kadri iwezavyo ili kuona kama inaweza ikasaidia kuokoa. Kusema ukweli, pamoja na juhudi ambazo Serikali inafanya ya kupeleka vyombo vya ulinzi kule ziwani, lakini bado hawawezi kumaliza uvuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawawezi kumaliza uvuvi haramu, kwa namna ambavyo sasa watu wamekuwa na technics nyingi zinazohusiana na huu uvuvi. Kwa hiyo, wakati mwingine unakuta wanaenda kule, kwa bahati mbaya, kabla hawajafika, taarifa zimeshafika. Hivyo, unakuta wale wavuvi haramu hawapo, tayari wamesha-escape. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, lazima Serikali ijiongeze, ione namna ya kufanya kuhakikisha kwamba lile ziwa linaendelea kuwepo na kuwasaidia watu wetu. Kwa maoni yangu, kama tunataka kupunguza uvuvi haramu, ziko njia mbili tu ambazo nadhani zikifuatwa zinaweza zikatusaidia. Njia ya kwanza ya kuweza kupunguza uvuvi haramu, ni kukubali kuwa na Mamlaka ya Uhifadhi wa Maziwa pamoja na Bahari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jirani yangu Mheshimiwa Francis amezungumzia suala la mamlaka, ni ukweli usiopingika, kila mahali ambapo mamlaka imewekwa, ufanisi umeonekana. Sasa unapozungumza suala la ziwa na uhifadhi wake wote ule, kwamba liwe chini ya Wizara, kusema ukweli hii tutatwanga maji kwenye kinu. Ndiyo maana nasema kwamba, hili halina mbadala, ni lazima tuwe na mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri suala hili nililichangia kwenye lile Bunge, na Waziri aliahidi kwamba hivi karibuni wangeleta hiyo sheria ya kuunda mamlaka. Kwa hiyo, leo nafurahi kumwona Mheshimiwa Waziri Dkt. Kijaji yuko hapa. Naomba basi, aifuatilie hiyo sheria na tuikamilishe ili tuwe na mamlaka ili iweze kutusaidia, kuhakikisha kwamba haya maziwa yetu na yenyewe walau yanaweza kuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona mfano kwa wenzetu wa pale Kigoma, kwa muda mfupi tu lile Ziwa Tanganyika lilipolindwa, tuliweza kusikia mafanikio na kuyaona. Sasa leo ukizungumza, Musoma, viwanda kama vitano vyote vimekufa. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri amekuja Musoma na alivyohudumu tu kwenye hiyo Wizara, alikuja Musoma na alijionea, na akapata taarifa zao kwamba pale sasa hakuna kiwanda hata kimoja kinachofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri aliahidi kwamba atakuja, akiwa hapo aliniambia kwamba akipata nafasi tukimaliza Bunge atakuja kwa ajili ya kukaa na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa angalia, kwa sababu ya umuhimu wa lile ziwa, mpaka wafanyabiashara au wale wavuvi wenyewe wamehiari kutoa michango yao kwa ajili ya kuchangia katika zile gharama za kuzuia uvuvi haramu. Kwa hiyo, nadhani hili ni suala la mamlaka na njia ambayo itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la kuwashirikisha wale wananchi na wavuvi wenyewe. Unajua pamoja na juhudi ambazo Serikali inatumia, lakini bado uvuvi haramu upo wa namna nyingi. Yaani unakuta hata pale ufukweni tu mtu ana kile kimtumbwi kidogo anafanya uvuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri, kwa sababu hawa wavuvi haramu ni watu ambao tunakaa nao, ni rahisi zaidi kuwatambua hasa tukiwashirikisha wananchi wakatusaidia hata kuwatambua, na kutambua hata nyavu na zana zao wanazotumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine kwa kutokufahamu, tunadhani kwamba viwanda vinavyotengeneza nyavu vikizuiwa, uvuvi haramu utapungua. La hasha, kwa sababu leo watu wanashonea nyavu majumbani. Leo zile nyavu unakuta zinaunganishwa, badala ya kuwa na ule unene unaotakiwa au urefu unaotakiwa, wanaunganisha, zinakuwa ndefu zaidi. Hivyo basi, kutokana na hali hii, kwa namna yoyote ile suala la uvuvi haramu litaendelea kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba kama haya mambo mawili yakifuatwa, kama tukawa na mamlaka na vilevile tukawa na ushirikishwaji wa wananchi, ambao ndio wanaoishi na hawa watu itakuwa rahisi kudhibiti uvuvi haramu kila unapojitokeza. Hii haitaokea kwa sababu nyingine, bali kwa sababu wananchi wenyewe watakuwa wamechoshwa na hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mtu anaenda na mtumbwi ziwani, anarudi na kilo tano au kilo kumi. Hivyo, hata gharama alizotumia kwa mafuta ya kwenda na kurudi, hazirejeshwi. bado haziwezi kurudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu wanaona kwamba wanajikuta katika hali ngumu, ndiyo maana wameamua kwa hiari kutoa ushirikiano kwa Serikali ili tatizo liweze kutatuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali, hasa Mheshimiwa Mama Samia, kwa kuleta hizi cage kwa maana ya ufugaji wa vizimba. Hivyo, nasema, endapo hatutazuia uvuvi haramu, hata hivi vizimba navyo havitakuwa na maana kabisa, kwa sababu uvuvi haramu wa sumu utaua samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sumu hiyo haiishii tu kuua samaki wa nje, itaingia pia kwenye vizimba. Hii inamaanisha kwamba mtu atakuwa amewekeza fedha nyingi kwenye vizimba akiwa na matumaini ya kupata samaki, lakini kesho yake anakuta samaki wote wamekufa. Hali hiyo imetokea na kila leo tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, njia pekee ya kuhakikisha ufanisi, ni kutumia vizuri rasilimali ziwa, na tutakapokuwa na njia mbili, ambazo ni imani yangu kwamba zitatusaidia na maisha ya watu wetu yataboreka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)