Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu kuhusu hoja ya Kamati yetu ya Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naungana na waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayofanya, sambamba na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa anayofanya kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utendaji kazi uliotukuka wa viongozi hawa wakuu, ndiyo ulisababisha Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, kwa kauli moja kumpitisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa Mgombea wa Urais kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, pia nampongeza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea mwenza na hatimaye kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Kamati yetu ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa kazi kubwa wanayofanya chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Vita Kawawa, Mwenyekiti wetu; Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Vincent Mbogo pamoja na Wajumbe wa Kamati hii, ambao kwa kweli wamekuwa na ushirikiano Mkubwa sana kwetu. Ushauri wao, mapendekezo na maelekezo yao yamekuwa chachu kubwa katika utendaji kazi ndani ya Wizara yetu ya Mambo ya Ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Mheshimiwa Mwenyekiti kwa taarifa nzuri iliyojaa mambo mazuri kabisa ya kujenga taasisi zetu hizi. Naungana na waliotangulia, kupongeza vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na vilivyo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kazi kubwa wanayofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi imeendelea kuwa tulivu na kuwa salama kwa sababu watu hawa wanafanya kazi kubwa sana. Usalama wa nchi uko mikononi mwa jamii nzima, Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwa upande wa Jeshi la Polisi. Imezungumzwa habari ya ajali za barabarani. Ni kweli ajali za barabarani zimekuwa ni changamoto kubwa inayopunguza nguvu kazi ya Taifa. Hivyo, kama Wizara kupitia Jeshi la Polisi, tuna mikakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kwanza ni marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani Sura 168, sheria ambayo ni ya mwaka 1973 na ilifanyiwa marejeo mwaka 2002. Ni sheria iliyopitwa na wakati, kwa hiyo, tuko hatua za mwisho kupata maoni ya wadau mbalimbali ili kuhakikisha tunatunga sheria inayoendana na wakati na kuzingatia matakwa ya wakati huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni usimikaji wa kamera za kisasa 6,500 ambazo kwa kuanzia, tutazisimika katika Jiji la Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma na baadaye nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa tatu ni ukaguzi wa lazima wa magari (Mandatory Vehicle Inspection). Miradi hii karibia inaanza na katika hili tutakagua magari yote yanayoingia nchini pamoja na yanayotumika nchini ili kuhakikisha kwamba magari yanafaa kutembea katika barabara zetu na kuepusha ajari ambazo siyo za lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo tunaendelea kulifanya kazi, ni kuendelea kutoa elimu kwa umma; shuleni, makanisani, misikitini, masokoni pamoja na maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba wadau wote wanashirikishwa katika suala zima la kuepuka ajali za barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ametoa fedha. Hivi ninavyozungumza, tumeshaleta magari kwa ajili ya highway patrols na tumeshatoa magari 50 kwa ajili ya ma-OCD nchi nzima. Mwisho wa mwezi huu wa Pili, tunapokea magari 122 kwa ajili ya ma-OCD waliobaki nchi nzima ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kulinda raia na mali zao katika maeneo mbalimbali hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia, hasa Wajumbe wa Kamati, kwamba kuna upungufu wa vitendea kazi na vituo katika mikoa mbalimbali. Katika hili, Mheshimiwa Rais ametupatia fedha dola milioni 100 kutoka Taasisi ya Adex iliyoko katika Falme za Kiarabu kupitia Kampuni ya NAFFCO FZCO, ambayo iko Dubai, tumenunua vifaa vya zimamoto pamoja na magari kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tunanunua boti 23 za kuzima moto, helicopter moja, magari ya kuzima moto 150 ambazo tutayasambaza katika mikoa mbalimbali na wilaya zote hapa nchini, mtambo mmoja wa kunyanyua vitu vizito, magari 40 ya kubebea majeruhi na wagonjwa, magari matatu ya kukabiriana na kemikali hatarishi na milipuko, magari matatu ya ngazi, magari 30 ya mawasiliano na amri na karakana sita zinazotembea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, pia tuna ujenzi wa vituo saba katika Mikoa ya Songwe, Kagera, Njombe, Manyara, Geita, Katavi na Simiyu. Pia, kwa upande wa rasilimali watu tayari mwaka 2024 wamehitimu askari 221, na katika mwaka huu wa fedha tayari tumeshapata kibali cha kuajiri askari 425. Hii yote ni katika kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya magari 12 ya kisasa yameshapokelewa, yameenda Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Mwanza, Kilimanjaro na Dar es Salaam kwa maana ya Ilala, Temeke pamoja na Kinondoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jeshi la Magereza, ziko changamoto ambazo zimesemwa na Waheshimiwa Wabunge hasa kuhusu uchakavu wa magereza ya zamani. Katika hili Mheshimiwa Rais ametoa fedha, tumepewa shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya ukarabati wa magereza ya zamani. Kwa mfano, Gereza la Lilungu ambalo liko Mtwara, Gereza la Ukonga, Segerea pamoja na Keko ambayo yako Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zimetengwa kwenye mwaka huu wa fedha wa 2024/2025. Ni imani yangu kwamba baada ya ukarabati huu, basi magereza haya yataendelea kutoa huduma na pia tutaendelea kukarabati magereza mbalimbali awamu kwa awamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, Jeshi pia limeendelea kujenga magereza katika maeneo ambayo hayana magereza hasa kwenye wilaya ambazo hazina magereza na katika hili tumetenga shilingi bilioni nne kwa ajili ya ukamilishaji wa magereza katika Gereza la Karatu ambalo liko katika Mkoa wa Arusha na Gereza la Kilosa ambalo liko katika Mkoa wa Morogoro. Haya yakikamilika, basi nadhani tutakuwa tumepunguza changamoto kubwa ya uhifadhi wa wafungwa na mahabusu katika magereza yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hivi leo tunavyozungumza wafungwa walioko magerezani pamoja na mahabusu ni 27,154. Hivyo, uwezo wa magereza yote 129 tuliyonayo nchini, tunaweza kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902. Kwa ushirikiano wa taasisi za mnyororo mzima wa hakijinai, msongamano umepungua kwenye magereza mbalimbali hapa nchini. Hii ni hatua kubwa ya kuipongeza Serikali kwa kazi hii kubwa inayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja la upande deni la Jeshi la Suma JKT limezungumzwa. Kwa sababu nipo hapa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa, hili jambo tumelipokea kwa uzito mkubwa na kama Serikali tumelichukua, tutalifanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma, na binafsi ili sasa madeni haya yalipwe, ili wenzetu wa Suma JKT waendelee na kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nilihakikishie Bunge lako Tukufu, maazimio tisa yaliyoelekezwa kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na maazimio mawili yaliyoelekezwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, tumeyachukua tayari kwa ajili ya utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa fursa hii, naunga mkono hoja. (Makofi)