Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuwapongeza sana wenyeviti wote wawili kwa mawasilisho mazuri waliyoyaweka Mezani na kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza zaidi Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuishauri Serikali na kutusimamia. Kazi yao ni nzuri sana, na ninaomba niseme kwamba sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi tutaendelea kupokea, kusikia na kutekeleza yale ambayo wanatuelekeza na kutusimamia kama Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba niseme tumepokea maazimio na maoni ya Kamati, na tutakwenda kuyatekeleza kama yalivyowasilishwa, kama ambavyo tumetangulia kutekeleza maazimio mengine ya Kamati yetu hii ndani ya mwaka huu ambao tuko kwenye utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba nichangie machache sana. Naanza kwa kuunga mkono hoja hii, na kama nilivyosema, tunakwenda kwenye utekelezaji, hivyo nitasema machache sana mbele ya Bunge lako siku hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa, naomba nianze na hili la uvuvi haramu. Kwenye uvuvi haramu, tunakiri na tunatambua Bunge lako lilituelekeza kuanzishwa kwa mamlaka ili tuwe na ufanisi kwenye eneo hili. Nasi tulianza utekelezaji na tayari iko kwenye ngazi mbalimbali ndani ya Serikali yetu. Tutakapokamilisha, basi kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema na Kamati yetu ilivyotuelekeza, tutaileta sheria hiyo hapa Bungeni ili tuweze kutekeleza kwa 100% maelekezo ya Bunge letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamesema na naomba nianze kwa ndugu yangu Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Jimbo la Konde kuhusu kinachoendelea kule Pemba. Naomba tu nimwambie kwamba, uvuvi wa maji ya ndani, au maji ya Kitaifa unasimamiwa na Mkurugenzi wa Uvuvi kwa Serikali ya Zanzibar, na kwa upande wa Bara pia inasimamiwa na Mkurugenzi wa Uvuvi ndani ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjulisha Mheshimiwa Mohamed kwamba, hatujazuia wavuvi wetu kuendelea kuvua, lakini yeye mwenyewe kama alivyotangulia kusema kwamba tunashughulika na wavuvi haramu, na kwenye hili hatuna simile. Tunahakikisha tunalinda rasilimali zetu zote za maji ili tuweze kunufaika kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mohamed kwamba tutaendelea kusimamia rasilimali hizi na wala hatuna hofu ya ushindi kwa Chama cha Mapinduzi. Kwa Timu ambayo imetambulishwa jana kwa Watanzania, sisi Chama cha Mapinduzi hatuna mashaka na kura zetu. Ni timu imara na makini. Tunakwenda kushinda, na Pemba yote tunakwenda kuichukua. Kwa hiyo usiwe na mashaka kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, timu yetu iko imara sana na kwenye hili ni kwa sababu tu tumesimamisha timu makini na tunafanya yale ambayo wananchi wa Tanzania wamekituma Chama cha Mapinduzi kufanya na sisi Serikali yao tunaendelea kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo la pili, nalo ni kuhusu chanjo ya mifugo. Kwa hili naomba sana Waheshimiwa Wabunge, moja, tumpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi yake mema kwa Taifa hili na kwa usimamizi wake makini wa rasilimali za Taifa hasa sekta zetu hizi za uzalishaji ikiwemo sekta hii ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema tumpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu ameendelea kuandika historia ya kipekee tangu akabidhiwe mamlaka ya nchi hii kama Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili ndani ya bajeti yetu tunayoitekeleza mwaka huu, ametupatia shilingi bilioni 28.1 kwa ajili ya chanjo ya mifugo. Haijawahi kutokea ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Taifa letu, aliifanya Baba wa Taifa na sasa anaifanya Jemedari makini Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tayari tumeshazindua kampeni ya chanjo na kampeni ya uhamasishaji, ninaomba niwashukuru na kuwapongeza wafugaji wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chama chetu cha wafugaji ndani ya Taifa letu wamekubaliana na jambo hili na tayari mikataba ya wazabuni tumeshasaini tunakwenda kuifanya kazi hii kwa umakini wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamesema tuangalie na twende kwa umakini na tulishapokea kutoka kwenye Kamati yetu. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yetu. Tunakwenda kwa umakini wa hali ya juu na Mheshimiwa Rais wetu akasema kumekuwa na malalamiko ya chanjo ambazo hazifanyi kazi sawasawa. Ni chanjo bandia, ni chanjo ya aina gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais akasema Hapana, amefungua mipaka ya nchi hii. Tuna wawekezaji wamewekeza kwenye viwanda vya chanjo ndani ya Taifa letu na wataalamu wetu wanasimamia. Mheshimiwa Rais katuelekeza chanjo tunayoipeleka kwenye mifugo ya wafugaji wetu kwamba rasilimali ya Taifa letu zitatoka kwenye viwanda vyetu vya ndani. Kwa hiyo, tunaifahamu tangu hatua ya kwanza mpaka hatua ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakwenda kuifanya kazi hii kwa umakini mkubwa. Wataalamu wetu wa mifugo wanakwenda kusimamia zoezi hili pamoja na wataalamu wetu. Tunajua ni wachache, hawatoshi kwenye kata zote tulizonazo, Mheshimiwa Rais akatoa ruhusa tuwatumie watalaamu wetu waliofundishwa ndani ya nchi yetu kuhusu mifugo ambao hawajaajiriwa na Serikali yetu, tuwachukue 3,500. Moja, tutakuwa tumetengeneza ajira za vijana wetu ambao wamefundishwa na watakwenda kutekeleza zoezi hili kwa umakini mkubwa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja ili nimalizie. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, sisi ni Madiwani na viongozi kwenye halmashauri zetu, jambo hili tulibebe, tulipeleke kwenye halmashauri zetu ili tunapoenda kuanza zoezi hili, wananchi wetu wote wawe tayari na watoe mifugo yao ili tuweze kuchanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametoa shilingi 500/= kwa kila ng’ombe na mfugaji atatoa shilingi 500/= kwa kila ng’ombe. Mheshimiwa Rais ametoa shilingi 300/= kwa kila mbuzi na kondoo, na mfugaji atatoa shilingi 300/= kwa kila mbuzi na kondoo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mifugo aina ya kuku kwamba wanaohusika ni akina mama, Mheshimiwa Rais kwa mapenzi makubwa ya wanawake wa nchi hii amesema kuku wetu wote tunapoenda kuwachanja ni bure kabisa bila kuchangia chochote. Hayo ndiyo mapenzi ya Mheshimiwa Rais wetu. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tufikishe elimu hii ili mifugo yetu yote iweze kuchanjwa. Nakushukuru sana. (Makofi)