Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambapo kwa mara nyingine ametupa kibali, tumefika salama katika Bunge hili na tunaendelea na mchakato huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpongeza sana kwa jambo kubwa lililotokea hivi karibuni baada ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi kumpendekeza yeye kuwa mgombea wetu katika uchaguzi unaokuja mwaka huu, na lakini halikadhalika kule Zanzibar pamoja na kupata mgombea mwenza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana Wenyeviti wetu wa Kamati wote wawili: ndugu yangu, Mheshimiwa Mwanyika na Mheshimiwa Vita Kawawa pamoja na Mheshimiwa Makamu Wenyeviti. Naomba nimpongeze dada yangu, Mheshimiwa Mariam Ditopile Mzuzuri kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya.
Mheshimiwa Mwenyeiti, vilevile, naomba nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati. Kamati yetu hii ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo imekuwa tofauti kidogo. Mara nyingi sana imekuwa ni Kamati ya kutoa maelekezo yale yanayoleta tija katika Taifa letu hili. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tuna kila sababu kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu katika muda wa sasa ametupatia Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hii ni bahati kubwa sana. Wakati nikichangia hoja hizi za Kamati mbili, nchi yetu inaweka historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati imezungumzia baadhi ya miradi, lakini nataka ku-cite miradi michache sana. Mradi wa kwanza, ni wa Mchuchuma na Liganga ambao toka mimi ninaingia mwaka 2010 katika Bunge hili, mradi huu umeendelea kuzungumziwa; lakini chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha mwelekeo tofauti kabisa katika mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza, kule Njombe, zaidi ya shilingi bilioni 15.4 zimetolewa kwa wananchi. Huu ni mfano wa kuigwa kutoka kwa Mheshimiwa Rais, mwenye commitment ya kutekeleza matatizo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unaenda vizuri na muda siyo mrefu, ndani ya mwaka huu wa fedha tunaondoka nao. Imani yetu ni kwamba kwa mara ya kwanza inawezekana tukaona sasa Tanzania tunaenda kuhakikisha kwamba tunaenda kuzalisha chuma ambayo ni malighafi muhimu sana katika maendeleo ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la pili ni la Mradi wa Maganga Matitu ambapo mradi ule umesainiwa kwa mara ya kwanza vilevile unaenda kuzalisha chuma na upo Ludewa. Hii ni kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hivi karibuni kuna mradi ambao ni wa kihistoria; toka mwaka 2004, tafiti ya kwanza ilivyofanyika katika ya Taasisi yetu ya NDC na TATA Chemical Limited, mradi ule ukashindwa kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza mradi ule ambao uwekezaji wake utakuwa zaidi ya shilingi trilioni moja ambapo fidia yake ni zaidi ya shilingi bilioni 14.84, imetolewa fedha yote ya fidia. Katika eneo hili tuna kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii watu wa Engaruka, mpaka hivi sasa tumefikia takribani 64%, watu 404 wamelipwa kati ya watu 599. Ni imani yetu kabla ya tarehe 15 ulipaji wa fidia utakuwa umekamilika. Siyo hivyo tu, mradi huu umeshatangazwa tangu tarehe 27 Desemba, sasa hivi tender zinapokelewa. Imani yetu ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza tutaona nchi yetu imejielekeza katika upande wa uzalishaji wa magadisoda ambayo ni malighafi muhimu katika ujenzi wa viwanda vya vioo, na pia ni malighafi muhimu katika viwanda vya detergent zote na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba niipongeze Kamati kwa sababu toka nilivyopewa Wizara hii na Mheshimiwa Rais, Kamati hii imekuwa ni kielelezo ili tuweze kufanya utekelezaji wa miradi hii. Naomba kwa fursa ya Bunge hili, niipongeze Kamati hii, imefanya kazi kubwa ambayo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe wameeleza hoja mbalimbali hapa nami kazi yangu ni ya kuchangia, mimi sio mtoa hoja. Jambo la kwanza ni suala zima la kibajeti, hili tumelipokea na ninaomba nimhakikishie Mwenyekiti wetu wa Kamati, jambo hili Wizara tumelipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hoja mbalimbali na hasa upande wa bajeti, ufinyu wa bajeti katika taasisi zetu kama TEMDO, CAMARTEC na nyingine zote, jambo hili tutaenda kulihangaikia ili kuhakikisha kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na kwa sababu tathmini ya kina imeshafanyika kuona kwamba kila taasisi inahitaji fedha kiasi gani, ni imani yetu kubwa tutaenda vizuri katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili ni suala zima la biashara, kwamba taasisi zetu wakati mwingine zinatengeneza vifaa. Kwa upande huo, naomba nilipongeze Jeshi la Wananchi, kwa mara ya kwanza vifaa vilizalishwa kule TEMDO, tumeona yale mafriji ya kisasa sana yamechukuliwa, yamewekwa katika cell.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi Tanzania wameonesha mfano wa hali ya juu sana, mafriji yale ukienda kuyaangalia ni durable sana na value for money ipo, yanatengenezwa na Tanzania. Jeshi la Wananchi ni Taasisi ya kwanza kufanya hayo manunuzi, tunalipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yetu na taasisi nyingine zitaenda kuhakikisha kwamba zinatumia vifaa vinavyozaliswa nchini kwetu. Naomba nikuhakikishie kwamba tutaendelea kutoa elimu kwa baadhi ya taasisi zetu kuhusu nini kinapatikana katika maeneo yetu. Kwa hiyo, lengo kubwa ni kwamba nchi yetu isonge mbele na kuhakikisha taasisi hizi zinafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la changamoto ya mitaji, kama tulivyosema mwanzo kwamba ni kweli maoni haya yamepokelewa na Serikali sasa hivi inaendelea kuhakikisha kwamba jinsi ya kufanya tupate fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati walishauri mbinu mbalimbali za kufanya, hata kutumia Agriculture Development Bank kuona kwamba tunapataje fursa ili mradi taasisi zetu zifanye vizuri. Maeneo hayo tunayachukua yote nasi kama Wizara tunaendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala zima la Stakabadhi Ghalani. Kwenye hili naomba nimshukuru sana ndugu yangu Mheshimiwa Bashe. Taasisi ya Stakabadhi Ghalani ipo Wizara ya Viwanda na Biashara, lakini tumeendelea kufanya kazi vizuri sana na ndugu yangu Mheshimiwa Bashe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza, katika mwaka huo 2024/2025 mazao zaidi ya tani 810,000 yameuzwa katika utaratibu huo. Zaidi ya shilingi trilioni 2.6 zimeenda kwa wananchi, na zaidi ya shilingi bilioni 87 zimeenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie ndugu zangu, halmashauri zile takribani 62 ambazo zinatumia utaratibu mzuri wa Stakabadhi Ghalani zimeonyesha outstanding performance hivi sasa. Leo hii ukienda Halmashauri ya Mtwara, Halmashauri ya Newala na Halmashauri ya Nachingwea, hawawezi kukubali hata siku moja. Kwa mfano, mnakumbuka watu wa Manyara bei ya mbaazi ilikuwa mpaka shilingi 200, leo hii imefika kati ya shilingi 1,600 mpaka 2,000 kwa ajili ya Stakabadhi Ghalani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili mimi na ndugu yangu Mheshimiwa Bashe tutaendelea kulitolea elimu ya kutosha, kuona kwamba halmashauri nyingine zitumie utaratibu huu mzuri, lakini mwisho wa siku inaleta thamani katika halmashauri zetu kwa kupata fedha nyingi bila kutoa jasho la aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yetu kubwa kwamba jambo hili tutaenda kulifanyia kazi na kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa maeneo mbalimbali. Kwa mfano, Mheshimiwa Hhayuma alizungumza hapa kwamba wale ambao hatu-integrate tuweze ku-integrate vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Bodi yetu ya Stakabadhi Ghalani sasa hivi wamefunga utaratibu wa kamera, juzi nimezindua hapo, lakini wameweka namna ya kuandaa utaratibu wa kuwahusisha wafanyabiashara wale wengine ambao wanaonekana wanaachwa nje ya mfumo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yetu kubwa wale wadau wengine wa Kitanzania kwa maboresho yanayofanywa, kila mtu atashirikishwa vizuri, tukiwa na lengo kubwa kwamba nchi yetu isonge mbele. Ni imani yangu kubwa kwamba tukishirikiana vizuri katika hili, tutapata mafanikio makubwa sana katika upande wa uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine ni suala zima la Kiwanda chetu cha Viuadudu pale Kibaha. Naishukuru Wizara ya Afya, kwa mara ya kwanza wamenunua dawa ya shilingi bilioni 3.5, hongereni sana Wizara ya Afya. Hata hivyo, suala la kimkataba tunaendelea kulifanyia kazi. Tunamshukuru sana AG ameshafanya kazi yake ya msingi, tunaenda ku-finalize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Serikali za Mitaa tunajipanga vizuri tukiwa na lengo la kuhakikisha kiwanda kile kinafanya vizuri. Ni kweli kiwanda ni kikubwa, kina thamani kubwa lakini kazi yetu kubwa sasa, tunaendelea kuboresha maeneo haya. Ni imani yangu kubwa tutafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa scanner, tumeshirikiana na wenzetu wa TRA, sasa hivi kuna mchakato wa ununuzi wa scanner sita. Ni kweli Kamati ilienda Horohoro, maeneo mengine scanner hakuna. Ni imani yetu kubwa kwamba mchakato huo wa manunuzi kwa kushirikiana na TRA utakamilika, na mwisho wa siku tutapata mafanikio makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, na pia nawashukuru sana Wajumbe wa Kamati zote mbili, ahsante sana. (Makofi)