Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA, KILIMO NA MIFUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ili niweze kuhitimisha hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo. Awali ya yote tumepokea michango mingi sana kutoka kwa Wabunge 15. Kati ya hao, Wabunge watatu ni Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kutoka rohoni kwamba, nashukuru sana kwa michango hiyo. Tunathamini sana michango ambayo Waheshimiwa Wabunge wameitoa, michango ambayo imetoa msisitizo, imetambulisha zaidi na imetoa maelezo ambayo inaonesha wazi hoja ya Kamati katika Bunge lako, imeeleweka vizuri kwa Wajumbe walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waongeaji walikuwa ni wengi, mambo ni mengi na muda wetu hautaturuhusu kuyaongea yote, lakini nitaongea machache waliyoongea Waheshimiwa Wabunge. Wengi wameongelea suala zima la uvuvi haramu na haja ya kuhakikisha kwamba, Serikali inachukua hatua madhubuti katika kushughulika na uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni kubwa, na kama lilivyojitokeza katika maelezo hapa, limeonesha wazi kabisa inatakiwa kuwe na hatua madhubuti na za uhakika. Sasa Kamati nayo imelisema na kwa kweli tukubaliane kwamba, kwenye suala la uvuvi haramu inaonekana watu wengi wana maslahi, na kwa hiyo, usimamizi wake umekuwa hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya Kamati kulitafakari kwa dhati, imeona moja ya mambo au solution au suluhisho kwenye suala la uvuvi haramu, pamoja na kwamba ni jambo gumu, ni ipatikane mamlaka maalum ambayo itapewa jukumu madhubuti la kushughulika na suala la uvuvi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja ya mamlaka bado inabaki kuwa ni hoja ya msingi kwa Kamati yetu. Tumeisema na Wabunge wengi wamechangia kutaka mamlaka. Nimemsikia Mheshimiwa Vedastus Manyinyi, ameliongelea hilo, Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya ameliongelea hilo na Waheshimiwa Wabunge, wanakamati, wengi wameliongelea hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tuweze kuthibiti, kwa kweli iko haja ya kuacha utaratibu wa sasa ambapo Wizara yenyewe ndiyo inakuwa msimamizi wa hii sekta ya uvuvi. Ndugu zangu tuvuke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba, uvuvi ni biashara, mifugo ni biashara na Serikali siyo taasisi ambayo inaweza kuwa nyepesi au nzuri zaidi kufanya biashara au kusimamia biashara au kudhibiti moja kwa moja. Kwa hiyo, ni vizuri tukawa na mamlaka ambayo itakuwa accountable na bado Waziri atakuwa na role kubwa kwenye shughuli hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambazo zimejitokeza kwa Wajumbe ni pamoja na ile ambayo Mheshimiwa Mwijage ameiongelea kuhusu magugu katika maeneo ya uvuvi. Tuseme wazi kwamba halikujitokeza sana kwenye Kamati yetu, lakini tunalichukua kama moja ya changamoto na kama Kamati tungependa kutembelea hayo maeneo ili tuweze kujifunza vizuri zaidi ni mambo gani tunaweza kuyafanya ili kuondokananayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge, na hasa Wanakamati; Mheshimiwa Kunti, Mheshimiwa Janejelly, Mheshimiwa Khadija Aboud, Mheshimiwa Francis Mtinga, Mheshimiwa Mohamed, wameyaongelea kwa undani na wameyakazia katika kufafanua hoja ya Kamati yetu, ni mambo ambayo yamejitokeza kwenye changamoto mbalimbali za kampuni ambazo ziko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, ametoa maelezo hapa kujaribu kuelezea Kampuni kama CAMARTEC na TEMDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni kampuni ambazo zilianzishwa kimkakati miaka mingi toka wakati wa Mwalimu Nyerere. Kampuni hizi zilikuwa zifanye utafiti na uzalishaji wa zana za bei nafuu kwa ajili ya wakulima, lakini kampuni hizi zimeendelea na zimefanya makubwa zaidi, zimeingia kwenye utafiti na zimekwenda mpaka kuanza kutengeneza mitambo mbalimbali ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tunasema kwa kweli, iko haja taasisi hizi ziongezewe fedha ili ziweze kufanya kazi ambazo zilikusudiwa. Kwa kusema hili, tumetembelea CAMARTEC, TEMDO, KMTC; tuseme wazi, Serikali yetu inahitaji kuhakikisha kwamba kampuni hizi siyo tu inazipa ruzuku, siyo tu zinaomba fedha, lakini inaziwezesha zifanye biashara kwa sababu ni kampuni za kibiashara na hilo linawezekana, na baadhi ya Wajumbe wamesema hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, TEMDO wamekuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza majokofu, nasi tumeyaona na tukajaribu kulieleza kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara. Tunashukuru kwamba hata kama TAMISEMI bado hawajaweza kuingia na kuanza kuchukua majokofu hayo kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati zetu, lakini angalau Jeshi la Wananchi limeonesha mfano. Hospitali nyingi za Jeshi la Wananchi zinatumia majokofu yaliyotengenezwa na TEMDO na yanafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutoe wazo au wito kwa Serikali kuhakikisha kwamba, kupitia TAMISEMI kwa kweli, ina sababu ya kujipanga, ili TAMISEMI iweze kuwa ni moja ya wabia wakubwa wa kuzifanya kampuni hizi zifanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima ambalo limeongelewa na Wajumbe wengi kuhusu uhaba wa scanner. Hili ni jambo la muhimu sana. Kwanza, tuhakikishe kodi inalipwa; na pili, tuwe na uhakika tunapata mizigo ambayo ina usalama kwa nchi yetu. Ni vizuri tukaifahamu mizigo na njia pekee, rahisi na ya kisayansi ni kuwa na scanners. Sasa kwa jambo hili tunamshukuru Mheshimiwa Waziri, amelielezea hapa kwamba wameliingiza kwenye bajeti. Kwa kweli, tunaomba bajeti hii itekelezwe ili tuweze kupata hizo scanners.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Kiwanda cha Dawa pale Kibaha na chenyewe ni cha kimkakati. Nchi hii, moja ya maadui wake wakubwa ni maradhi, kwa maana ya Malaria. Nchi hii inahitaji kiwanda hiki kifanye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumekuwa na competing interest kwamba, labda ukiwa na vyandarua vingi unaweza ukashughulika na Malaria. Sisi, kama Kamati, bado tunaona kwamba ni vizuri kiwanda hiki kikapewa nguvu; kikapewa biashara, kikapewa mtaji, ili kiwe ni source kubwa ya ku-eliminate Malaria katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme wazi kwamba tunamshukuru Mheshimiwa Waziri kwamba, sasa wameanza, na ni kweli. Nami taarifa zangu zinaonesha wazi kwamba, wameanza, na mwaka uliopita wamenunua lita 374,999 kwa shilingi bilioni 3.5. Ni fedha nyingi, lakini utaratibu wa manunuzi bado ni ule wa Wizara ya Afya inachukua inapeleka TAMISEMI, ili wazigawanye kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunadhani ni vizuri kukawa na mikataba. Kwa mfano, mwaka 2025/2026 kwa mujibu wa National Malaria Strategic Plan itahitajika dawa lita milioni 1.6; mwaka 2026/2027 kutahitajika lita milioni 2.4. Ni lita nyingi na ni fedha nyingi zinatakiwa ziingie katika mfumo wa bajeti, ili jambo hili lifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke vyandarua vingi vilikuwa vinatolewa na wafadhili, na ndugu zangu wengi tunajua kwamba, baadhi ya wafadhili sasa wameamua kujitoa. Kwa hiyo, turudi kwenye kiwanda chetu tukiimarishe, kizalishe, tukipe bajeti, ili kiweze kufanya biashara iwaokoe Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la viwanda limeongelewa kwa kirefu sana hapa, na ni vile ambavyo tunasema kwamba tuvilinde na tuhakikishe vinafanya kazi. Kuna wachangiaji wameongelea viwanda vya sukari, dawa, viuatilifu na mchangiaji mwingine ameongelea suala la viwanda vya maziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kamati, katika maazimio mbalimbali tumeongelea haja ya Serikali kuendelea kutoa vivutio, kuendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji wa viwanda mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tuseme, kwenye sukari tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Waziri wa Kilimo, walichukua maamuzi ya haraka na madhubuti ya kuwaokoa Watanzania kwenye janga la sukari, lakini tunachosema ni kwamba, tuendelee kuongeza uwekezaji kwenye eneo la viwanda vya sukari, ili viweze kutusaidia tuweze kuondoa uagizaji wa sukari na kuokoa fedha ambazo tunatumia katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uti wa mgongo. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Bashe, wengi wamemwelezea hapa. Sisi kama Kamati tumeona ambavyo Wabunge wengi wamemwongelea, ni Waziri mahiri ambaye ameonyesha wazi kabisa anataka na anafanikiwa ku-transform na kutoa uongozi katika Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi tunajua na tunasikia hakuna Wizara ngumu kuiendesha kama ya Kilimo, lakini Mheshimiwa Bashe ameweza, tunampongeza sana. Mheshimiwa Bashe ametuambia hapa siri yake, kwamba aliyemwezesha kufika alipofika ni Mheshimiwa Rais, Jemedari Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunamshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi sana kwenye kilimo yamefanyika. Kweli, kilimo kimeshughulikiwa kama vile ni uti wa mgongo wa nchi yetu. Pembejeo za kilimo, tumesikia hususan ruzuku; tumesikia uwekezaji kwenye ugani kwa ukubwa; tumesikia vitendea kazi kwa wingi; maslahi ya wafanyakazi yameboreshwa; na tumesikia magari yamenunuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo mengi yamefanyika, nasi, kama Kamati, tunasema tutafanya kazi kwa ukaribu na Wizara hii kuhakikisha yale yote ambayo wamejipangia kama vipaumbele tunawasimamia ili yaweze kutekelezwa, lakini kuna machache ambayo, Mheshimiwa Waziri Bashe, ameyaongea katika kuchangia kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umwagiliaji ni kweli, ndiyo maana sisi tumetoa mapendekezo kwamba, fedha za umwagiliaji zitolewe kwa wakati. Jambo hili ni la muhimu na nisingependa kuliongelea zaidi kwa vile Mheshimiwa Waziri ameliongelea, na ni kwa nini tumekwenda polepole? Kuna mambo mengi yamefanyika ambayo nayo yalihitaji fedha. Kuanzisha ofisi 136 za umwagiliaji nchi nzima na kununua mitambo, vitu hivi vyote vinakwenda pamoja na ku-invest kwenye umwagiliaji wenyewe na mabwawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumekuwa na uwekezaji mkubwa hata ku-set up hiyo institution. Kwa hiyo, kama Kamati, tunapenda waongezewe fedha, lakini tunasema tutaendelea kuwa patient wakati Serikali inaendelea kujipanga zaidi kwenye suala la umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Stakabadhi Ghalani. Waheshimiwa Wabunge wengi wameongea hapa kwamba ni mfumo mzuri wenye faida na ambao tunadhani unahitaji elimu zaidi, lakini ni mfumo ambao kwenye mapendekezo yetu tumesema unahitaji miundombinu zaidi iweze kuwekwa kwenye maeneo ambayo kuna mazao. Tunaiomba Serikali iweze kutenga fedha zaidi ili jambo hili liweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ambayo imeendelea kujitokeza, Mheshimiwa Hhayuma na Wanakamati wenzangu wameielezea. Bado kunahitajika kuwa na uwazi zaidi kwenye eneo la utendaji wa Stakabadhi Ghalani. Kuna maeneo ambayo tungependa watu wapate imani zaidi na mfumo huu, lakini inaonesha kwenye utendaji kuna gharama nyingine ambazo zinakwenda kwa wananchi nao wanaamini pengine inaweza isiwe kweli. Ni vizuri kukawa na elimu na uwazi, ili stakabadhi ghalani kama mfumo ufanikiwe kwa sababu, umekuwa mkombozi wa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la chai limekuwa ni kizungumkuti. Namshukuru sana Mheshimiwa Bashe alikuja kutueleza sisi Kamati, na tulilichukua jambo hili kwa uzito mkubwa sana. Ni zao ambalo linatakiwa lifanyiwe maamuzi magumu. Namshukuru Mheshimiwa Bashe kwa aliyoyasema hapa, na kwa vile tunajua Serikali inachofikiria, sisi kama Kamati, tumeomba muda ili tuweze kutembelea maeneo yote na siyo chai peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba yaliyoachwa na wawekezaji, yako kwenye chai, yako kwenye mkonge, yako kwenye ngano. Kote huko ni maeneo ambayo yanatakiwa yaangaliwe kwa umakini. Nafurahi kwamba, Mheshimiwa Bashe na Wizara wako katika mpango kazi wa kujaribu kuona namna gani watafanya, lakini na sisi tungependa twende kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la vituo rasilimali vya kata ambavyo katika mapendekezo yetu tumeomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali. Unaweza ukahitimisha hoja.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA, KILIMO NA MIFUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nahitimisha hoja yangu, nizungumzie moja tu la mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mifugo inaonekana inaweza ikatufikisha mbali sana kiuchumi, lakini bado hatujaitumia vizuri. Kwenye sekta hii ya mifugo na uvuvi pendekezo letu kubwa ni moja kwamba, inahitaji usimamizi wa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote makubwa yaliyofanyika, pamoja na uwekezaji mkubwa uliyofanyika, sekta hii ili iweze kutoa mchango kuweza kubadilisha maisha ya Watanzania, inahitaji usimamizi wa karibu sana. Pendekezo letu ni kwamba, hata huko kunahitaji kuwa na mamlaka ambayo itasimamia moja kwa moja suala la mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nihitimishe hoja yangu jioni ya leo kwa kusema kwamba, Bunge sasa lipokee na liikubali Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo pamoja na Mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)