Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Jambo la kwanza niunge mkono hoja ya Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa yale yote ambayo yamewasilishwa na nimpongeze Mheshimiwa Mnzava, kwa kuwasilisha vizuri sana maoni ya Kamati yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitachangia mambo mawili nikiwa nimejikita kwenye suala la utalii, na pia kwenye Wizara ya Ardhi. Jambo la kwanza, kwa niaba ya wananchi wa Makete, nawapongeza sana Wagombea wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; pia Dkt. Emmanueli Nchimbi na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja, kati ya sifa ya Chama cha Mapinduzi, tuna Wagombea imara, tuna ilani inayotekelezeka, ni Chama ambacho kina wanachama wanaojitambua. Kwa hiyo, tupo tayari kwa uchaguzi na tumejipanga kweli kweli kuhakikisha mwaka huu tunashinda na hatuna mjadala.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alisema ukitaka kujua nguvu ya CCM tangaza uchaguzi. Kwa hiyo, nasi tunaamini kwamba kwenye chama chetu, mwaka huu tumejipanga kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya utalii, niungane na maoni yote ambayo yametolewa na Kamati na nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Utalii Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, na Mheshimiwa Deogratus Ndejembi, Waziri wa Ardhi kwa wanavyotuunga mkono sana kwa sababu tunafanyanao kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye Sekta ya Utalii, Serikali tuliweka kusudio la kufikia watalii wengi zaidi ya 5,000,000. Nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara na Serikali kwa sababu tunavyozungumza leo kwenye ilani yetu, yale malengo ambayo tuliweka watu 5,000,000 tumeshavuka, tumefikia watu 5,360,000 zaidi ya 107% tumeweza kufikia watalii hao. Hii inaonesha kabisa kwamba project ya Mheshimiwa Rais ya The Royal Tour imeweza ku-boost utalii kwa kiwango kikubwa sana kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na Ripoti ya Shirika la Utalii Duniani linakiri wazi kwamba Tanzania imekuwa ni namba sita kwa ongezeko la watalii katikati ya Januari hadi Septemba, 2024. Tumekuwa namba sita duniani na namba moja barani Afrika. Maana yake ni kazi kubwa sana ambayo Serikali imeifanya, na ninaunga mkono jitihada hizi na tuendelee kumshangilia Mheshimiwa Rais kwa sababu aliamua kuweka kabisa mguu wake na mkono wake kuhakikisha kwamba utalii wa nchi hii ambao unachangia zaidi ya 20% ya pato la Taifa. Ni kitu kikubwa ambacho Mheshimiwa Rais, amekifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa maoni yangu, nitachangia suala la miundombinu kwenye sekta ya utalii. Tuna takribani kilomita 6,950 ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho kwenye hifadhi zetu ili watalii wengi ambao Mheshimiwa Rais amepambana, wanapokuja waweze kuwa na maeneo mazuri ambayo yanapitika.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na changamoto sana kwenye hifadhi ya Serengeti na hifadhi zote mbalimbali nchini ambazo ukizijumlisha ni 10.2% ya ardhi ya Tanzania. Kwa hiyo, tunahitaji kuboresha miundombinu ya hifadhi zetu.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa sababu wameunda shirika ambalo linajihusisha na ujenzi wa barabara kwenye maeneo ya hifadhi na Serikali ilinunua mitambo mikubwa sana. Nami nikiunga mkono maoni ya Kamati, naomba sana Wizara na Serikali, shirika hili liweze kuwa na uwezo wa kujisimamia; pili, liweze kufuatilia maeneo yote ambapo barabara zimekuwa zikisumbua. Tufanye marekebisho haya kwa sababu sasa hivi gharama haitakuwa kubwa, kwani mitambo wanayo.
Mheshimiwa Spika, pili, vifaa mnavyo na kwa kuwa wataalamu pia wanao, waweze kujenga miundombinu ili iweze kupitika hususan barabara ambayo ni tegemeo kubwa. Tukifanikiwa kujenga barabara ya kuunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Mara, Mkoa ambao kwa kweli barabara ile ikiunganishwa, tunakuwa tumefungua lango la utalii kwenye eneo la Arusha na eneo la Serengeti yote.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kwenye Kituo cha Utalii cha DMCC. Tumetumia zaidi shilingi 1,300,000,000/= kujenga kituo hiki muhimu sana na Serikali ikalifanyia kazi kwamba hiki kituo sasa kianze kufanya kazi kwa sababu hii ni sehemu ambapo sisi tunategemea kitatupa statistics kwa maana ya takwimu nyingi za mwendelezo wa utalii kwenye nchi yetu, na baadaye kujua nini ambacho soko linahitaji?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikakifanyia kazi kituo hiki ambacho kipo pale Dar es Salaam. DMCC kwa maana ya Digital Marketing Centre cha Pale Dar es Salaam kwenye suala la utalii. Hayo yalikuwa ni maoni yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, nilikuwa natamani sana Mheshimiwa Waziri kati ya hoja ambazo Mheshimiwa Rais amekuwa nazo kubwa kwenye sekta ya utalii ni suala pia la malazi. Tumeleta watalii wengi sana na kuleta huku watalii uhitaji wa malazi umekuwa kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Spika, sasa naiomba Serikali, Kamati tulikutana na watu wa Wizara, lakini pia tulikutana na Msajili wa Hazina, ili kuzifanyia tathmini zile lodge na hoteli zote ambazo zipo kwenye maeneo potential. Bahati nzuri ni kwamba, hizi lodge na hoteli zipo kwenye maeneo mazuri ambapo zikifanikiwa kujengwa au kupata uwekezaji upya, zinaweza zikawa na tija sana kwenye Serikali.
Mheshimiwa Spika, sasa hizi lodge nyingi zimekwama na ndiyo mara nyingi nimekuwa nikitolea mfano hoteli ya Embassy iliyopo Dar es Salaam, ipo eneo zuri katikati pale Posta. Miaka 14 hoteli haifanyi kazi na pamekuwa kimya as if watu hawaoni kile kinachoendelea. Sasa ni muhimu Serikali ikazifuatilia hizi hoteli zote kwa sababu zipo kwenye maeneo muhimu, maeneo ambayo watalii wanatamani kuzitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, basi Serikali ingefuatilia kwa wale ambao wamekiuka umiliki, pia na uendelezaji, Serikali ikachukua hatua maeneo haya ya hoteli yakaweza kuchukuliwa na wawekezaji wapya wakapewa na ile nia ya Mheshimiwa Rais kwamba wawekezaji wote wanaoingia Tanzania wasikose malazi, iweze kutimia.
Mheshimiwa Spika, hili ni jambo langu muhimu sana ambalo naisisitiza Serikali, na mwone tija Embassy Hotel, Dar es Salaam miaka 14 imelala haifanyi kazi, siyo jambo zuri na haileti faida kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kwenye suala la hifadhi kwa maana Ngorongoro na hifadhi zetu za TANAPA. Sisi kama Kamati tulipeleka wazo Serikalini, kwamba hawa watu waweze kujikusanyia fedha na kuzitumia, lakini Serikali imekuwa na changamoto ya kuzuia hilo jambo. Hoja yao ni kubwa, kwamba kumekuwepo na matumizi ya mabaya kwenye suala hili kwa maana ya TANAPA na NCCA kukusanya fedha na kuzitumia wenyewe.
Mheshimiwa Spika, hoja ya Serikali imekuwa kwamba, matumizi in a record huko nyuma hakuwahi kuwa na matumizi mazuri kiasi kwamba wakafikia hatua ya kuzichukua hizi fedha. Sasa sisi tunamani haya maoni ya Kamati yangefanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika, tusihukumu taasisi nzima kwa watu wachache ambao wame-misbehave tuka-deal na hawa wachache ambao wame-misbehave, lakini tukazisaidia hizi taasisi kwa sababu ukisaidia TANAPA, NCCA watapata fedha ambazo zitasaidia kwenye sekta ya utalii, kwa sababu 80% ya mapato ya utalii zinatoka na hizi shughuli ambazo zinafanywa na TANAPA pamoja na NCCA.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vyema sana Serikali ikaangalia jinsi ya kuwawezesha hawa watu ili waweze kupata fedha, na pia waweze kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri.
Mheshimiwa Spika, wazo langu lingine ni kwenye Wizara ya Ardhi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri Ardhi kama nilivyosema, na pia Katibu Mkuu, kaka yangu Mhandisi Antony Sanga kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwenye Wizara hii ya Ardhi. Ameleta utulivu mkubwa kwenye Wizara ya Ardhi na anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa ni kuomba tu kwamba wakati anakuja kwenye Wizara, Mhandisi Antony Sanga, Waziri alisema huyu atakuja pia kutibu suala la mifumo kwenye Wizara. Sasa changamoto kubwa kwenye Wizara ya Ardhi ni mifumo kutokusomana, ndipo ambapo changamoto inajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huyu unakuta ana hati ya eneo hilo hilo, nami nina hati ya eneo hilo hilo, watu 10 tuna hati ya eneo moja. Hiyo ni kwa sababu mifumo haisomani, tunafanya analogy way. Ni vema Wizara ikachukua na ikifanya suala la mifumo kusomana, itakuwa imesaidia kuondoa duplication kwenye suala la upatikanaji wa viwanja, lakini pili itasaidia kwenye ukusanyaji wa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kitu muhimu sana Serikali ikalifanya hili ili migogoro ambayo ipo, ya wakulima na wafugaji; migogoro iliyopo kati ya wananchi kwa wananchi kwenye mipaka, itatatuliwa kwa mifumo kusomana na ujenzi wa mifumo. Hii imekuwa ndiyo kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais, mifumo ya nchi isomane.
Mheshimiwa Spika, tunamtegemea Mheshimiwa Waziri Deogratus Ndejembi, kijana mzuri kabisa ambaye anaweza kuichapa kazi kwenye hili jambo, na anaweza akafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni kwenye suala la Tume ya Mipango ya Ardhi, wanahitajhi shilingi bilioni kama 170 tu kuweza kutatua changamoto za ardhi zote zilizopo nchini. Kwa hiyo, ni vyema Tume ya Mipango ikapewa fedha ikasaidiwe ili iweze kuratibu masuala ya upimaji wa ardhi nchini na kupanga matumizi ya ardhi. Hili ni muhimu sana na sisi tuseme kama Kamati tunaiombea sana Serikali yetu na hata bajeti ijayo tunatamani sana kwenye fungu namba tatu Tume ya Mipango ya Ardhi iwezeshwe ili kutatua changamoto za mipango ya ardhi kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nami sina mengi zaidi, naunga mkono hoja. Hivyo, ninawaahidi tu Wanamakete kwamba tutaendelea kuwa pamoja kwa sababu kazi njema ya Serikali yetu imefanyika na sisi tupo tayari kwa ajili ya mapambano. Niwahakikishie kwamba nipo imara na nguvu bado ipo.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)