Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja za Kamati zilizo mbele yetu. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mdau mkubwa wa masuala mazima ya mazingira nchini. Mheshimiwa Rais ameonekana katika mikutano mbalimbali anajaribu kuchochea chachu kubwa na kuona mabadiliko makubwa ya kimazingira yanaendelea katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu ambacho kinashangaza, Mheshimiwa Rais anajitahidi kwa upande wake, lakini kwenye Wizara tunaona suala zima la bajeti la Ofisi ya Wizara ya Mazingira bado lipo chini sana. Kwa mfano, ukiangalia bajeti ya 2024/2025 fedha za maendeleo ambazo zimeletwa katika Wizara hii ya Mazingira ni shilingi bilioni 21; shilingi bilioni 18.3 ni fedha za nje, na shilingi bilioni 2.9 ndiyo fedha za ndani.
Mheshimiwa Spika, sasa unajiuliza kwa macho mawili; je, Serikali yetu ina nia madhubuti kwa ajili ya kulinda mazingira yetu? Kwa sababu haiwezani fedha shilingi bilioni 18 kati ya bilioni 21 ni fedha ambazo tunategemea wahisani. Kwa hiyo, sisi mazingira yetu yatatunzwa na kulindwa na wahisani? Kwa sababu tunaamini, wahisani wanavyotuma fedha, wanatuma na utaratibu wao na matumizi yao ya kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa haya matatizo ambayo yapo ndani ya nchi yetu yanayojitokeza ambayo kama mabadiliko ya tabia ya nchi na vitu vingine vinajitokeza kwa haraka, tunawezaje kuvi-solve kama tunatarajia fedha za miradi ya maendeleo asilimia kubwa kama hii watupe wahisani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kwenye Kamati tulishauri na naendelea kushauri hapa kwamba bajeti lazima iongezwe na fedha za maendeleo ziongezeke. Isiwepo hii asilimia ndogo ambayo inaonekana hapa. At least ifike 60% ili tuweze kuyalinda na kuyatunza mazingira yetu na kupambana na changamoto ambazo zinajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la taka ngumu. Mheshimiwa Mwenyekiti amewasilisha taarifa hapa vizuri sana, na ninampongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati. Amezungumzia kwamba wastani wa taka ngumu zinazozalishwa nchini, nyingi zinazokusanywa na kurejeleshwa, maana yake hapa ni zaidi ya hizo ambazo zinakusanywa na kurejeleshwa. Kwamba, inaonekana hakuna data maalumu ambayo inaonekana idadi ya tani ngapi tunakusanya taka kwa siku ndani ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii inaleta masikitiko makubwa sana kwa sababu taka zinazalishwa kila siku na ndiyo maisha yetu. Kama tunapumua na taka ni lazima tutake tusitake tutazizalisha; lakini inaonekana ndani ya Wizara hakuna utaratibu au mpango mzuri sana wa kuzisimamia taka hizi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano hapa wamesema, kwa Jiji la Dar es Salaam wanakusanya taka kwa 63% tu. Sasa tujiulize, hiyo 37% ya taka zinakwenda wapi? Ni nani ambaye anazikusanya? Maana haijulikani. Maana ukiangalia kwa makini zaidi, hii 37% ni taka ambazo zinaendelea kuzagaa na kutapakaa ndani ya nchi yetu. Hiyo ni kwa Dar es salaam, bado hatujachambua ndani ya mikoa mingine.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya taka ni kubwa sana, kwa sababu kila siku ni lazima taka zizalishwe, na hii inasababisha taka kusambaa na hivyo inaweza kusababisha magonjwa mbalimbali ya mlipuko kuongezeka ndani ya Taifa letu. Hali kadhalika inaweza kusababisha uharibifu wa kimazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, taka zinaweza zikabebwa na wind force. Kwa mfano, hapo Dar es salaam wapo katika kingo ya maji, na wapo katika Bahari, zina uwezo wa kuvutwa na kwenda baharini na wind force, lakini vile vile hayo mabadiliko ya tabia ya nchi tunayoyapigia kelele yanasababishwa na joto kali la ndani ya Taifa. Joto pia linatoka kwenye taka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unajiuliza, maana kama hiyo ni Dar es Salaam, huko kwingine tukija tukikaa chini tukachambua asilimia ni chache sana ya taka ambazo zinakusanywa. Sisi kwenye Kamati tulishauri Wizara na tunaendelea kushauri ndani ya Bunge lako Tukufu, kwamba ni wakati sasa wa Wizara kukaa na kutafuta wadau mbalimbali ambao wataweza kuanzisha, kama zilivyo taasisi nyingine binafsi zinazofanya kazi. Kwa mfano, ukienda nchi ya wenzetu jirani, Kenya wana kampuni inaitwa Takataka inafanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano ukija hapa ndani ya nchi yetu tuna changamoto kubwa ya mbolea. Kila siku hapa kilimo kikisimama watu wote wanapiga kelele, mbolea mbolea, ruzuku sijui inauzwa shilingi 70,000/= na kwingineko; huku ukiangalia ndani ya taka tuna uwezo wa kuzalisha mbolea nzuri ya mboji ambayo ni safi na salama.
Mheshimiwa Spika, kitu ambacho kinasikitisha, Wizara ya Kilimo inapaswa ikae na Wizara ya Mazingira ili watafute namna bora ya kutafuta wawekezaji ndani ya Taifa hili ili wawekeze viwanda vidogo vidogo, tuzalishe mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo kama mbolea inauzwa mfuko shilingi 70,000/= na kuendelea, huyo mkulima wa chini unategemea alime nini? Mabadiliko haya ya tabia ya nchi ambayo kila siku yanatokea huku na huku, ardhi zetu zimekuwa kame, mvua zimepotea, mambo ni shaghalabaghala? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ufupi mimi nashauri kwenye sekta hii kwamba ni lazima kwenye vituo vyetu vya mabasi kukatengenezwa utaratibu wa ukusanyaji wa taka, wakaweka madampo, iwe mtu akifika anakuwa na hiyo taaluma ya kwenda na kufika. Pia waanzishe radio, TV ili kuonesha jinsi gani taka zinahitaji kuchambuliwa na watu waweze kupata elimu kwa ufanisi zaidi na waweze kuchambua taka hizo na zikusanywe zipelekwe katika madampo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara pia nayo wasijibebeshe kila mzigo. Kuna mambo mengine wanapaswa wasaidiwe. Sasa wao wajenge madampo, wakakusanye taka na mambo mengine. Kwa hiyo, wanatakiwa pia watoe hizi fursa kwa wawekezaji ili wawekezaji hao wajenge vituo vya kisasa waweze kuzirejelesha taka hizo na kuweza kupata bidhaa mbalimbali ndani ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwa kumalizia, labda kwenye Wizara ya Maji. Kumekuwa na changamoto kubwa ya masuala ya taasisi za Serikali kutokurudisha fedha na kulipa ankara za bili za maji. Kwa mfano ukija katika Wizara hii ya Maji, wana miradi mingi sana ambayo haikamiliki kwa sababu hakuna fedha. Kama hakuna fedha, lakini mbona kuna hizi taasisi wana fedha wamezizuia? Kwa nini hawalipi maji? Kwa nini mwananchi wa chini aweze kulipa maji wao wasilipe maji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaani wanatakiwa nao wawe na utaratibu wa kulipa maji. Hayo madeni ambayo wameyalimbikiza ambayo hapa tukisoma taarifa yanakaribia shilingi bilioni 80, fedha ambazo zipo kwenye taasisi za Serikali, watu hawataki kulipa maji. Sasa walipe ili miradi ya maji ikamilike kwa wakati na wananchi wa Taifa hili wapate maji wasilalamike.
Mheshimiwa Spika, walipe ili fedha kwenye Wizara hii ziongezeke waweze kuchipua na miradi mingine. Mheshimiwa Mama Samia amesema ana nia ya dhati ya kumtua mwanamke ndoo kichwani. Sasa, anamtuaje ndoo ikiwa fedha wamezikalia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, nije kwenye suala la uvunaji wa maji ya mvua. Tunashukuru Wizara imekuja na mpango mzuri na imetuonesha kwamba wapo tayari kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua, hususani mijini na vijijini.
Mheshimiwa Spika, ushauri wetu kwa Serikali, kwa sababu tunaona changamoto kubwa inayoonekana hapa ni Wizara kwa Wizara kutokusomana. Maana hakuna mifumo maalumu.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Wizara ya Maji watachimba mabwawa ya maji; Wizara ya Kilimo watachimba mabwawa; na wao wanataka hayo hayo maji. Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji, wote wanachimba maji; wavuvi nao wanachimba mabwawa ili waweze kupata maji wafuge samaki au waweze kulishia wanyama wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza hizo gharama, yaani fedha kwenda huku kwenda huku, walipaswa wakae meza moja waweze kutafakari namna nzuri ya kuchimba hayo mabwawa ya kisasa ili watu wa maji waweze kuchepua maji kutoka kwenye hayo mabwawa, watu wa kilimo wachepue maji kutoka kwenye hayo mabwawa na watu wa mifugo wachepue maji kwenye hayo mabwawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimalizie kwa kusema tutunze mazingira ili na sisi yaweze kututunza. Ahsante sana. (Makofi)