Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo Mezani. Kwanza kabisa, niunge mkono hoja zote mbili. Nitumie fursa hii pia kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maji na Mazingira; na kwa kweli naomba nijikite kwenye eneo moja kwa sababu muda ni mchache. Natambua kuwa kumefanyika kazi nzuri sana kwenye maji, hongera sana kwa Mheshimiwa Rais na Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu maji na mazingira, na hasa kwenye taarifa iliyowasilishwa leo, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ambaye ni kinara wa mazingira duniani. Hili wote tunatambua na limedhihirishwa kwanza kwa ule mkutano wa hivi karibuni uliohusu nishati ambao uliofanyika Dar es Salaam. Kwa kweli amekuwa ni kinara wa nishati safi ya kupikia; na hata kwenye taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni ya Kamati ya Nishati tumeona.
Mheshimiwa Spika, kwenye Kamati yao walisema takribani mitungi zaidi ya 400,000 ilishasambazwa, lakini tunaona namna ambavyo Mheshimiwa Rais amesimamia vyema maazimio ya Cope 28, hilo wala halina ubishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ule Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliofanyika, na yale maazimio, tunaona namna ambavyo Mheshimiwa Rais ameendelea kuwa kinara. Hotuba zake nyingi, za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakuna hotuba ambayo hajagusa suala la mazingira. Hata ile ya mwaka mpya alipozungumza na Waheshimiwa Mabalozi, alisisitiza suala la mazingira. Mheshimiwa Rais amekuwa pia akisisitiza suala la mabadiliko ya tabia ya nchi kuwekewa mikakati na namna ambavyo tunaweza tukadhibiti. Pia suala la taka ngumu, namna ambavyo pia tunaweza tukadhibiti; vilevile na masuala mengine kimsingi ambayo yanaweza kuathiri mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hapa pia Serikali yake, hata katika rasimu ya Dira ya Taifa ya 2025 – 2050 ambayo sasa tunaitarajia izinduliwe suala la mazingira limepewa kipaumbele. Sasa nina uhakika kwamba Chama changu cha Mapinduzi katika ilani yake inayokuja ya 2025 – 2030 suala la mazingira na utunzaji wake litakuwepo. Hii ni kwa sababu hayo yote niliyoyasema yanaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, nina uhakika kuwa chama changu kitaweka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kazi nzuri hiyo na namna ambavyo sisi Wana-CCM tumeridhika, ndiyo maana Mkutano Mkuu ulimpitisha. Ninayo sababu ya kumpongeza yeye pamoja na mgombea mwenza pamoja na mgombea Urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, kwamba naunga mkono maazimio ya Kamati. Haya mambo yote ambayo Kamati yetu imewasilisha katika Bunge lako leo, naona ipo changamoto ambayo ni ya msingi sana ingewekewa mkazo. Hata katika mkutano uliopita kwenye sehemu ya maazimio ya Kamati, kuna jambo ambalo pengine linaendelea kutekelezwa, lakini naweza kusema pia bado halijatekelezwa, na lenyewe ndilo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati iliagiza mara kadhaa na kwenye taarifa pia limekuja, suala la kuharakisha mchakato wa kuleta mabadiliko makubwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira. Hili ni la msingi sana. Katika mabadiliko hayo makubwa ya sheria itakayobadilisha Sura Namba 191 ili iendene na sera mpya ya mazingira, tunaomba suala la NEMC, Baraza la Mazingira libadilishwe kuwa mamlaka. Hiyo itawezesha kuendana kwanza na sera mpya pamoja na kuifanya hilo baraza iwe mamlaka, iwe na meno au kuipa nguvu ya kuweza kusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Baraza linasimamia mambo ambayo yanaanzishwa na Wizara nyingine. Kwa mfano tunapozungumzia labda masuala ya taka, au mifuko ya plastiki, ni suala ambalo pengine linasimamiwa na TBS, lakini wao wanakuja kudakia huku nyuma, na wakati mwingine masuala ya kelele. Kwa mfano, inaweza ikaweka katazo halafu mimi ni kiongozi nikawakataza. Kwa hiyo, ni vizuri hii sheria ikabadilika ili tuiondoe NEMC kuwa mamlaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo imeonekana kwenye nchi za jirani, hata wenzetu wa Zanzibar tayari wanayo mamlaka. Ukienda Kenya wanayo mamlaka; ukienda Burundi wanayo mamlaka; Visiwa vya Shelisheli wanayo mamlaka. Sisi kizungumkuti kipo wapi ilhali tunaona political will, ama utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais upo wazi, dhahiri? Hili nadhani imebakia kwenye Wizara tu. Kwa hiyo, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba kulikuwa na marekebisho madogo ya sheria ambayo pia na leo hayapo. Kwa hiyo, tunaamini itakapokuja, kutakuwa na mabadiliko hayo makubwa ya kuitoa NEMC kutoka kuwa baraza na kwenda kuwa mamlaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, ni muhimu Wizara iharakishe mchakato wa kutunga Sheria ya Usimamizi wa Uchumi wa Buluu ili iweze kuendana na Sera mpya ya Uchumi wa Buluu ya 2024. Tukifanya hivyo, ni dhahiri pia kwamba tutakuwa tunafungamanisha masuala ya shughuli za kiuchumi hasa maliasili na utalii kama ambavyo imewasilishwa leo hapa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Tufungamanishe na Uchumi wa Buluu ili mambo yaweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu pia kwamba masuala yote hayo mawili yatawasilishwa katika Bunge lako Tukufu siku siyo nyingi ili Waheshimiwa Wabunge wote tuweze kuchangia vizuri, na ambapo tutaweza sasa kubadilisha sheria hiyo. Tunatambua kwamba iliyopo sasa inafanya kazi, lakini bado haiwezi kukidhi masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi, masuala ya hewa ya ukaa (carbon) na masuala haya ya mamlaka kutoka kuwa baraza.
Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali Sikivu. Sasa kama kuna mahali pengine kwenye ngazi ya Wizara hayo mambo yalikuwa hayajakaa vizuri, Bunge lako litafanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha mambo hayo yote yanaharakishwa na yanafanyiwa kazi sawasawa.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, kwa kweli naomba nitumie fursa hii kuamini kwamba katika eneo la tatu ambalo ninalipendekeza ni kuanzisha kituo mahususi na thabiti kitakachosimamia shughuli za hewa ya ukaa kuliko ilivyo sasa, kwa sababu tunajua kwamba kuna miongozo na mambo kama hayo.
Mheshimiwa Spika, tunatamani wote tuingie kwa nguvu kwenye halmashauri, kwenye vijiji, ili kwa kweli tunapozungumzia masuala ya hewa ya ukaa, basi ijulikane kuwa kituo kipo mahali fulani, na hapo tutapata nyenzo zinazohitajika, na litasimamiwa pia kisheria ili kuhakikisha kuwa biashara hiyo inakuwa katika mikono salama.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sitaki nigongewe kengele. Naomba nikushukuru tena, nirudie tena kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa kinara wa nishati na kuharakisha. (Makofi)