Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia hii nafasi, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia sisi sote kupata afya njema tukiwa katika hali ya usalama na amani katika nchi hii, Mwenyezi Mungu atubariki sana.
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ujasiri aliokuwanao, Mwenyezi Mungu amempa kadari kubwa sana. Hii yote inatuonesha wanawake tuna uwezo mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe, kwa ujasiri uliokuwanao, unanitia nguvu na moyo sana, Mwenyezi Mungu azidi kukulinda. Tunakuiga katika mambo mengi, mifano mingi tunaipata, hasa kwetu sisi wanawake kwa kupitia wewe. Mwenyezi Mungu akuongoze zaidi na hayo unayoyafanya huko duniani, yawe tija na faraja kwa wanawake Tanzania nzima, kuwa wanawake tunaweza bila kuwezeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuja katika hoja tuliyokuwanayo mbele yetu. Mimi ni mdau, kwanza mimi ni balozi wa utalii, balozi wa maliasili, na pia mimi ni Mama Mjusi. Mimi ni balozi wa Selous, nimeisimamia Selous kwa muda mrefu, lakini vile vile ni Mama Tembo. Kwa hiyo, nitaondoka katika Bunge hili nikiwa na majina hayo matatu na yawepo katika rekodi, kwamba kulikuwa na Mama Mjusi, Mama Tembo, na Mama Selous, ni mimi Riziki Said Lulida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitazungumzia hasa hali ya uchumi na hii Wizara ya Maliasili. Wizara ya Maliasili inahitaji kuongezewa fund za kutosha ili iweze kuiletea uchumi ambao utasaidia katika sekta za kiafya. Sekta zote za maendeleo ya jamii na elimu tunategemea fedha nyingi kutoka katika Wizara hii mojawapo.
Mheshimiwa Spika, naona katika tarakimu kwamba Wizara ya Maliasili inachangia pato la Taifa kwa 22.5%, lakini hii fedha ni ya kigeni. Ina maana Wizara hii ikiboreshwa na ikipewa fund ya kutosha, kama tulivyosikia kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati, ina maana tutaweza kupata faraja kubwa na huyu ng’ombe ambaye anakamuliwa maziwa atakuwa na maziwa ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, mimi ni mwanaharakati wa mjusi, tangu mwaka 2005, nikiwa na mgombea mwenzangu Mama Mikidadi. Tulikuwa tunasimama tunaitwa Mama Mjusi, na mjusi huyo nimeongelea humu Bungeni kwa miaka 20, lakini hakuna kinachoendelea. Kila anayekuja ananipa taarifa ambazo hazina matumaini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikupe taarifa. Mjusi huyu ambaye yupo Ujerumani, anafanyiwa biashara, na fedha zinazopatikana Tanzania hatupati revenue ya aina yoyote. Je, ni kwa faida ya nani? Kwa nini hatuonyeshi uzalendo wa kuhakikisha kuwa mapato yale yanaleta faida kwa Serikali Kuu, na yanaleta faida kwa Halmashauri ya Lindi?
Mheshimiwa Spika, hata pale lilipotoka jusi, hata shule hatujapata hadi leo, inasikitisha sana. Ninaondoka katika Bunge nikiwa na masikitiko kuwa masuala ya mjusi na faida ya mjusi haikupatikana mpaka leo. Kila anayekwenda inakuwa kama ngoma. Inachezwa ngoma, akirudi hakuna jibu linalopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina imani hili utalisimamia ukishirikiana na Wizara ya Maliasili, Wizara ya Mambo ya Nje na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Hii fedha Tanzania tunaitaka tuifanyie kazi. Kuiachia hela iwe inatumika na Wajerumani, sisi tutapata nini kule kwetu?
Mheshimiwa Spika, wale wazee ambao wamechukua jusi kutoka Tendaguru, lilikuwa na tani 225, mpaka kule baharini, kilometa 120, wengine wamekufa na hatukupata faida yoyote, lakini wenzetu Namibia walidai mapato ya mafuvu na wamepata karibu shilingi trilioni nne. Sisi tunafanya nini hapa?
Mheshimiwa Spika, tufike mahali sisi tusiwe eneo la kuonewa. Tunataka fedha za mjusi ziingie hapa. Mwenyezi Mungu ajalie, nataka nikitoka hapa, mwezi wa Sita, revenue collection inayofanyika Ujerumani itengenezewe sheria kabisa, ili iweze kuwasaidia wanakijiji wa pale, hata watoto wa pale wapate shule. Hakuna shule, hakuna maji na hakuna chochote kinachoendelea kwa ajili yao ili kufaidika na mjusi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la maendeleo ya urithi wa dunia. Katika urithi wa dunia, Kilwa haikuwa namba 21, lakini Kilwa ilikuwa na fedha yake ambayo iko Australia, ina zaidi ya miaka 1,000 haikufanyiwa kazi. Fedha nyingine ya Kilwa iko Zimbabwe, lakini leo Kilwa tukiangalia urithi wa Kusini, Lindi, Mtwara na Ruvuma tuna uwezo wa kuzalisha mapato makubwa na kuifanya nchi hii iweze kuibuka kiutajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utalii wa mikoa hiyo mitatu ya kusini unatosha kuweza kuongeza kutoka 22.5% mpaka hata kufikia 40% kwa vile ina uwezo mkubwa. Kwanza, vivutio vilivyoko kusini, tuna beach sand ambazo hakuna kabisa duniani. Alikuja balozi mmoja akasema beach sand ambayo inapatikana Mkoa wa Lindi na Mtwara hakuna duniani, lakini zile beach sand hazijatumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, asilimia mbili kwa tatu ya Selous yote unayoiona inapatikana Lindi, lakini leo kuna nini kinafanyika Lindi, Mtwara na Ruvuma? Bado utalii.
Mheshimiwa Spika, fedha za World Bank zilitengwa kusaidia Mikoa ya Kusini, lakini lugha inayotumika hapa ni kuitenga kusini. Unaposema Kusini ni Lindi, Mtwara na Ruvuma, ile fedha imekwenda Kusini Nyanda za Juu. Mnapoipeleka Kusini Nyanda za Juu, Liwale, Namtumbo, Lindi; na wote katika hiyo mikoa mitatu hatukufaidika na fedha zile. Je, tuko tayari kuusaidia utalii? Nina imani na Katibu Mkuu na Mheshimiwa Waziri wake wana kazi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Abbas, alifanya kazi kubwa sana kwenye michezo. Hivyo, ameingia huku. Nina imani kazi anayoifanya ni kubwa na Mwenyezi Mungu amlinde sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kuyapongeza mashirika yao, TANAPA na Ngorongoro, hayana mjadala. Haya mapato yote yanayopatikana in forex yanapatikana katika taasisi hizi. Je, kama hamjawasaidia hawa watu wakaweza kujikwamua kiuchumi, wakalipeleka hili gurudumu vizuri, tunategemea mabadiliko ya kipato yatakuwa makubwa na nchi hii itakwenda vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaizungumzia Royal Tour. Mheshimiwa Rais ametuvalisha nguo katika Royal Tour. Nchi zote duniani zimetambua Royal Tour ya Tanzania, lakini kuna kipengele inabidi kifanyiwe kazi kwenye Royal Tour kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 Umoja wa Mataifa uliridhia na kupitia Sheria ya Watu wenye Ulemavu katika suala la utalii. Narudia, mwaka 2014, Sheria ya Utalii kwa Watu Wenye Ulemavu iliridhiwa na Tanzania. Kama mwanachama, inabidi na sisi tuifanyie kazi Royal Tour kwa watu wenye ulemavu, ili nasi tuonekane tumekubali maridhiano ya Umoja wa Mataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpaka mwezi wa Sita, at least Waheshimiwa Mawaziri wangu wasikivu wa Maliasili, wote wawili, naomba waifanyie kazi Royal Tour kwa watu wenye ulemavu. Ipite na sisi turidhie, ili tunapokwenda katika event ya mwezi wa Sita, tuwe tumemalizana na masuala ya Royal Tour kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna vivutio vikubwa katika mikoa ya kusini. Tanzania ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kwa ajili ya kusimamia ukombozi wa Afrika. Wilaya ya Nachingwea iliweza kuwaweka Waheshimiwa Marais wakubwa ambao waliingia kwa kuwekwa katika Kambi ya Nachingwea.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwao walikuwa ni Mondlane, Samora Machel, Augustino Netto na Savimbi. Morogoro na Mazimbu waliwekwa watu wa ANC ambao tumeona walikuwa Marais wa huko South Africa. Je, kumbukumbu zile ambazo zipo katika maeneo hayo tumezifanyia kazi?
Mheshimiwa Spika, kama hatujayafanyia kazi, basi tutengeneze network ya kuja kuyaona maeneo ya Mazimbu ambayo tumewatoa Marais kwenda kwao na eneo la Nachingwea ambalo sasa hivi yamekaa kama magofu. Tunaomba, fedha ambazo zinawekwa zipelekwe kusini, ziangaliwe vizuri, ili utalii endelevu wa kumbukumbu za wapigania uhuru uwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, Putin amezungumza, alikuwa anakaa Bagamoyo kuisaidia nchi hii. Je, kumbukumbu zile ziko wapi?
Mheshimiwa Spika, kumbukumbu hizi tuziweke katika archives, tuna mengi ya kuzungumza na tuna faraja kubwa ya kuishukuru nchi hii, lakini kwa sasa tunaomba zipatikane fedha za kutosha ili haya mabadiliko tunayoyataka ya urithi wa utalii kusini, yafanyiwe kazi. Nina imani fedha itakayopatikana ni kubwa na Mwenyezi Mungu atajalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sina mengi ya kusema, ila haya machache ya mjusi. Wewe unanijua mimi nilikuwa mwanaharakati niliyewaita Waheshimiwa Wabunge humu ndani tukawa wanaharakati wa mjusi, Katibu wangu akiwa Mheshimiwa Omari Kigua na Mweka Hazina wangu alikuwa Mheshimiwa Reuben, lakini je, kwa nini mnatuacha hivi hivi, hatusimamii mjusi wetu?
Mheshimiwa Spika, huyu mjusi anatoka Lindi. Mimi natambua anatoka Lindi, na kama anatoka Lindi, tunahitaji Lindi yenye mabadiliko ya utalii ionekane. Isiwe Lindi ambayo inaonekana mjusi yuko Ujerumani, anafaidi Mjerumani, lakini ukienda pale hakuna shule. Natamani angalau twende Tendaguru ukaone.
Mheshimiwa Spika, Tendaguru imevamiwa na wafugaji na matokeo yake miti yote mizuri, kama mipingo, ambayo ilikuwa pale, inaisha. Mimi ni champion nasema, tungesimamia haya.
Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu awabariki. Naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)