Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.

Mheshimiwa Spika, nazishukuru Kamati zote mbili na hasa Kamati ya Maliasili na Utalii. Kwa kweli, sisi Waheshimiwa Wabunge tunakaa humu tunaangaliana mambo mengi sana. Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Utalii, yule kijana anaitwa Mheshimiwa Mnzava yuko makini sana kwa kweli. Tumpigie makofi, kwani ni mmoja kati ya vijana wenye talent kubwa sana katika Bunge hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, katika Kamati ya Maji na Mazingira, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, amewakilisha hapa pamoja na Kamati nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kuzungumzia maliasili na utalii. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu wake na viongozi wengine wote wa Kamati hiyo, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la fedha za TANAPA, TAWA, TFS na Ngorongoro kubaki kwenye maeneo yao, ni lazima Waheshimiwa Wabunge tufike humu ndani tuweke maazimio. Nafikiri Bunge lijalo, kwenye bajeti inayokuja, kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii kabla hatujaeleza hiyo bajeti, tuweke maazimio.

Mheshimiwa Spika, ni lazima tutoe mwongozo wa kutaka kujadili, kwa nini Waheshimiwa Wabunge tumesema hizi fedha zibaki kwenye hizi taasisi ambazo ni taasisi mama kwenye Taifa letu?

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge ndio wasemaji na ndiyo tunatimiza majukumu ya Serikali. Katika Bunge lililopita tulifanya maazimio humu ndani, tukasema fedha zibaki. Kwa nini hazijabaki?

Mheshimiwa Spika, nadhani kwenye Wizara hii, wakati tunakuja kwenye bajeti tutaambiwa kwa kina, kabla hatujaijadili, ni kwa sababu gani tuna hifadhi 22, mapori ya akiba karibu 49 na mambo mengi? Katika hifadhi zenyewe 22, hifadhi zenye fedha ni tano tu. Hivi kweli tunaweza kufanya mzaha katika kulinda mbuga na hifadhi zetu? Kwa sababu, mlolongo wa kupata fedha kutoka Hazina ni mkubwa sana, hivi kweli tembo atasubiri fedha zitoke Hazina ndiyo aje kulindwa? Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesikia Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa anasema ilitokea kwamba hatukuiamini Wizara, Hapana. Lile tatizo la kupeleka zile fedha lilitokana na COVID – 19. Baada ya kuonekana kwamba watalii hawapo na hifadhi zinatakiwa kulindwa, basi zikapelekwa kule ili Serikali isaidie kulinda.

Mheshimiwa Spika, sasa COVID ilishaisha, mama alishatangaza, na sasa hivi watalii wamejaa Tanzania, kwa nini fedha zibaki? Hapana, nafikiri hili, Wizara inavyokuja kwenye bajeti, tutajadili ni kwa nini sisi Wabunge tukitoa maazimio hayatekelezwi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba sasa Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kufanya mahusiano na majirani zao, waendelee kufanya mahusiano na vijiji Jirani. Zamani ilikuwa watu wanaenda kufanya makongamano na semina. Kwa mfano, sasa hivi Serikali za Vijiji zilizochaguliwa 2024 zote ni mpya. Inatakiwa TANAPA, TFS, Ngorongoro na TAWA waende wakafanye semina kuwapa elimu na mafunzo juu ya mahusiano na Serikali za Vijiji ambazo ni mpya. Waende huko wakajenge mahusiano, lakini pia, wakaone namna ya kufanya ulinzi wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo tabia sasa ambayo imetokea, tunasema Wizara ya Maliasili ilinde, lakini kuna kitu kinaitwa WMA, wanapata mabilioni. Kwenye halmashauri kuna watu wanaitwa Maafisa Wanyamapori, wapo. Twende tukashirikiane kwa pamoja tuweze kulinda wanyama waharibifu. Tushirikiane wote kwa Pamoja, hili ndilo agizo ambalo tunatakiwa kulifanya na pia, Maliasili na Utalii waendelee kujenga miradi ya majirani zao.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mimi pale Bunda kuna mradi wa jengo la upasuaji, wametoa shilingi milioni 55, wameliezeka, lakini sasa halina madirisha, milango na halina finishing yoyote. Kwa hiyo, naiomba ile shilingi milioni 50 ambayo tumeomba, ili waende wakamalize lile jengo kwa sababu, kituo cha afya kimejengwa, wametumia shilingi milioni 55 kujenga, lakini hawajamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jengo la kuzalia la Zahanati ya Maliwanda ambalo watu wamekuja mpaka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tulizungumza na watu wa TANAPA kwenda kujenga lile jengo, wananchi wameweka viashiria vyote kwenye jengo la mama na mtoto la kujifungulia la Maliwanda. Waende wakajenge ile miradi. Kwa hiyo, naomba mahusiano ya Wizara ya Maliasili na Utalii yawe makubwa kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwenye Wizara ya Ardhi. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri wake ambaye ni mpya kabisa, na Mheshimiwa Naibu wake. Katibu wake ni mtu maarufu sana, anaitwa Sanga, ni mtu mzuri sana, aendelee. Nawaomba sasa kwenye Wizara ya Ardhi, Kamishna wa Ardhi achangamke.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani mimi Mbunge nimeshaenda kwao mara mbili, mara tatu. Kuna mgogoro uko pale Mikomarilo ambao labda pengine ilitakiwa Mheshimiwa Waziri angefika au hata mtu mwingine angefika. Wananchi wanapokuwa na migogoro viongozi wafike, wakaenao, wawaulize mgogoro ni wa nini? Waweze kutatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mgogoro mwingine umejitokeza hapo Kiumbu, kuna mwekezaji amekaa pale na wananchi hawana mahusiano naye. Nimekwenda ofisini kwao, lakini hakuna mtu aliyefika; hakuna Mheshimiwa Waziri wala kamishna aliyefika.
Mheshimiwa Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri Ndejembi, sina lawama naye, lakini Wizara ni ya kwake, tumezungumza sana. Atakapotoka hapa, nadhani kabla ya bajeti yake, awe yeye au Mheshimiwa Naibu wake au mtu yeyote, aje kule Bunda. Haiwezekani tukawa tunazungumza hapa na kila siku tunakwenda ofisini kwao, lakini hawatekelezi. Kwani Mheshimiwa Rais amewateua wafanye kazi gani? Amewateua watusaidie sisi Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati fulani huwa najiuliza maswali mengi sana. Mtu akiwa Mbunge wa kawaida anakuwa na akili nyingi sana, lakini akiwa Waziri anajisahaulisha. Kwa nini inakuwa hivyo? Tuwe pamoja, wanakuwa pamoja na sisi wakiwa Wabunge wa kawaida, kwa nini wakiwa Mawaziri wanajisahaulisha? Nawaomba sasa tulimalize hili tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Bunda kuna suala la matumizi bora ya Ardhi ya Unyari, Kihumbu, Maliwanda na Sarakwa. Kwenye matumizi bora ya ardhi humo ndani kuna kitu kinaitwa WMA na kuna mashirika yanaitwa, sijui, Frankfurt, wanajiingiza humo kuwashawishi wananchi watengeneze WMA ambayo ni hewa. Tunaomba matumizi bora ya ardhi yabaki kama matumizi bora ya ardhi, tusiingize vigezo vingine vya kuwanyang’anya watu ardhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la Unyari, Maliwanda, Kihumbu na Sarakwa kuna mgogoro unaingia ingia humo ndani; waende wakafikirie, nataka kusikia maneno kama hayo.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru kwa sababu wanaendelea kupima. Naomba Serikali iwape fedha kwa kweli, kwa sababu matumizi ya ardhi hii ni makubwa sana. Tunaomba Serikali iwape fedha za kutosha ili kutusaidia katika kupanga matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni Wizara ya Maji. Nilikuwa Mbunge wa kipindi kilichopita 2015 - 2020 na nimekuwa Mbunge mpaka sasa hivi. Katika jambo ambalo nimeondolewa aibu ni suala la Wizara ya Maji. Namshukuru sana Mheshimiwa Aweso, ambaye kwa kweli Mheshimiwa Dkt. Samia alimteua akijua kwamba huyu kijana atafanya kazi. Ametoa maji ya Ziwa Victoria kutoka Butiama kuyaleta kwenye Jimbo langu la Nyamswa. Ametenga shilingi bilioni 8.7 ambazo tayari hizi fedha zinatafutwa ili ziende zikafanye hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ilikuwa ni aibu, unatoka hapa Dodoma unaambiwa maji kutoka Ziwa Victoria yanakuja, unafika Tabora unaambiwa maji yamefika Tabora, unafika sijui wapi unaambiwa maji yamefika. Sisi Mkoa wa Mara, kilometa 20 kutoka Ziwa Victoria, hatuna maji. Yaani ilikuwa ni aibu kama vile Wabunge ni wapiga debe tu.

Mheshimiwa Spika, namwombea Mheshimiwa Aweso Mungu ambariki sana na ninamwombea wananchi wake wamrudishe na Mheshimiwa Rais aendelee kumteua aendelee kuwa kwenye Wizara hiyo, kwani amefanya kazi nzuri sana, na Katibu wake ni mzuri sana.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaiomba Serikali iwape fedha. Wanafanya miradi mikubwa ya maji, lakini fedha hakuna. Tunaiomba sana Serikali iwape fedha za kutosha ili waweze kumaliza kazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, palepale Bunda wametumia shilingi milioni 67 kutengeneza utafiti wa kujenga mabwawa sita. Wametumia 1.5 billion shillings kujenga Bwawa la Nehingo, lakini halijakamilika, liko pale...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa malizia, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba na yale mabwawa sita ambayo wamejitayarisha kuyajenga, Wizara ya Maji, iende ikayakamilishe. Ahsante sana. (Makofi)