Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024


MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, naanza kwa kukupongeza wewe mwenyewe kwa kazi nzuri sana unayoifanya ya kutuongoza ndani ya hili Bunge, na kwa kazi nzuri sana unayoifanya huko kwenye Mabunge ya Dunia. Nawaomba Wanambeya, jamani msimwache Mheshimiwa Spika wetu, anafanya kazi ya nchi, mpeni kura nyingi sana ili aendelee kutuwakilisha kimataifa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, pia, naendelea kuwapongeza Wenyeviti wote wawili waliowasilisha ripoti zao katika Bunge leo hii. Vilevile, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maji na Mazingira, naomba nitoe pongezi kubwa na kutambua mchango mzuri kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Naibu wake, Mheshimiwa Eng. Kundo, na Katibu Mkuu wake, Mwajuma Waziri. Tunashukuru sana Katibu Mkuu, Mwajuma kwa kweli, wamemwingiza jikoni. Hii sera anaitekeleza ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Masauni, Naibu wake, Mheshimiwa Chillo, Katibu wake, Cyprian Luhemeja, pamoja na watendaji wote wa Wizara hizi mbili; Wizara ya Maji na Mazingira, kwa kazi nzuri sana ambayo wamekuwa wakiifanya, bila kuwasahau Mwenyekiti, Makamu na Wajumbe wa Kamati yetu ya Maji na Mazingira. Kwa kweli, wamekuwa wakishauri vizuri sana na ndiyo maana Wizara ya Maji inafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza mchango wangu, niomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Sera ya Kumtua Mwanamke Ndoo Kichwani. Pia, nawapongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Dkt. Nchimbi na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi wa kule Zanzibar kwa kuchaguliwa kuendelea kupeperusha bendera ya Chama chetu cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaomba Watanzania wote, bila kujali itikadi ya vyama vyetu, tuunge mkono na tumchague kwa kura nyingi sana kwa kazi nzuri ambazo amekuwa akizifanya katika nchi hii. Naomba tusigombanie fito, mama anaweza na anaupiga mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaanza mchango wangu sasa kwa kuendelea kuunga mkono sera ya Mheshimiwa Samia ya kumtua mwanamke ndoo kichwani. Hali ya huduma ya maji vijijini hadi kufikia Desemba, 2024 idadi ya watu wanaopata maji ni 37,812,123 sawasawa na 83%. Ni vijiji 10,532 kati ya vijiji 12,318 ambavyo mpaka sasa hivi vinapatiwa maji, ambayo ni sawasawa na 36%, siyo kazi ndogo. Tunapongeza sana kwa kazi nzuri inayofanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto ambazo zinasababisha Serikali kutokufanya vizuri sana. Naishukuru Kamati yetu, imetoa sababu na changamoto nyingi sana ambazo zimekuwa zinasababisha kutofikiwa mapema au kutokumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kata zile ambazo bado hazijafikiwa. Kwa hiyo, labda nitachangia changamoto chache. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya kwanza ni madeni ya maji kwa taasisi za Serikali. Tumekuwa tukilizungumzia jambo hili kwa muda mrefu sana kama Kamati. Tunaomba sasa lichukuliwe kwa umuhimu wake. Kufikia Juni, 2024 deni lilikuwa shilingi 45,109,478,157, tunashukuru ilivyofika Desemba tuliongea sana angalau deni la shilingi 5,573,026,726 liliweza kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona ulipwaji huu wa deni kama vile hauchukuliwi maanani sana, kutoka shilingi bilioni 45 zilipwe shilingi bilioni tano! Hizi taasisi ningeweza kuzitaja humu ndani, lakini kwa sababu ni Taasisi za Serikali zinajitambua, Waheshimiwa Mawaziri wapo humu, Makatibu Wakuu wanaelewa, walipe haya madeni ili Wizara yetu ya Maji iweze kufanya kazi vizuri na miradi ya maji iweze kutekelezwa kwa wakati ili kusiwepo na changamoto kubwa katika utekelezaji wa hii miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sasa Wizara ya Maji kupitia Mamlaka za Maji iendeleze na lile zoezi lake la kufunga dira za maji za malipo kabla ya kutumia (prepaid meter) hasa kwa hizi taasisi ili zisiendelee kuwa na madeni makubwa. Pia kwa wananchi hizi prepaid meter zifungwe ili wananchi waweze kulipa bili zao kama ilivyo TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ambayo ipo kuhusiana na madeni ya wakandarasi wa miradi ya maji, mimi kwanza naipongeza Serikali, imeendelea kulipa madeni ya wakandarasi wetu nchini, lakini pia nitoe pongezi nyingi sana kwa Serikali ikishirikiana na Benki ya CRDB kwa kuanzisha Samia – Bond.

Mheshimiwa Spika, hii Samia Bond sasa tuna imani kabisa kwamba wakandarasi wetu watalipa kwa wakati na sasa miradi ya maji itakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito wangu mkubwa kwamba wananchi wote wakiwepo Waheshimiwa Wabunge wote, hebu tujiunge na hii bond, huu mfuko uweze kutuna zaidi ili tuendeleze kulipa wakandarasi wetu na miradi yetu ikamilike kwa wakati. Kwa sababu hii bond kwanza ina riba nzuri sana, hata mimi tayari nimeshajiunga, hivyo itaisadia sana Serikali yetu, wakandarasi wetu kukamilisha miradi yao kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza haya, basi namshukuru Mwenyezi Mungu na ninaomba, kwa kweli tunaenda kwenye uchaguzi tuombeane neema ili tuweze kurudi tena hapa Bungeni, ahsante sana. (Makofi)