Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja za Kamati mbili ambazo zimeweka taarifa zake za mwaka siku ya leo. Nami ni Mjumbe kutoka Kamati ya Maji na Mazingira na hivyo nitapenda kuzungumzia maeneo mawili tu katika taarifa yetu ya mwaka ya Kamati yetu.

Mheshimiwa Spika, natangulia kusema kwamba moja ya eneo ambalo Serikali yetu imefanya vizuri sana, napenda kuamini kwamba ni eneo ambao litaipeperusha vizuri bendera ya chama wakati wote, ni eneo la usambazaji maji mijini pamoja na vijijini.

Mheshimiwa Spika, taarifa yetu ya Kamati inaonesha kwamba, hadi sasa kati ya vijiji 12,318 vijiji 10,532 vimefikiwa na huduma ya maji. Haya ni maendeleo, na ni hatua kubwa sana na kwa kweli, Wizara yetu ya Maji pamoja na mamlaka zote za usambazaji maji zinapaswa kupewa hongera na heko kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo Serikali yetu imefanya vizuri sana ni katika ongezeko la nishati ambalo limetokana na kukamilika kwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Pamoja na kwamba siyo mitambo yote imewashwa, lakini pia na ule mradi wa Rusumo unaotoa Megawatts 80 na kugawanywa katika nchi wanachama watatu, hawa nao wamefanya kazi nzuri sana ya kuongeza nishati. Hao pia kwa kweli wanastahili pongezi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawaomba Wizara ya Nishati waendelee sasa na kazi kubwa kuendeleza vyanzo vingine vya nishati kama upepo, jotoardhi kule katika maeneo ya Tukuyu, nishati ya jua na hata makaa ya mawe ambayo vyote kwa pamoja vikijumuishwa, nchi yetu itapata nishati ya kutosha; na nchi inapokuwa imepata nishati ya kutosha pia huwa ni kigezo kikubwa cha hatua kubwa ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kujenga hoja yangu juu ya mafanikio haya katika sekta ya maji pamoja na sekta ya nishati. Tunaona kwamba pamoja na mafanikio haya makubwa, gharama za uzalishaji maji bado ni kubwa na sababu zinaleta ukubwa wa gharama katika uzalishaji maji ni pamoja na gharama kubwa za umeme, kodi ya ongezeko la thamani kwa uzalishaji huo na pia kwa vipuri, mabomba na madawa ya kusafisha maji.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni hivi, kwa sababu tumepata ongezeko kubwa la nishati, tunatamani tupate matunda ya nafuu iliyopatikana kwa sababu ya ongezeko kubwa hili la nishati katika nchi yetu. Sipo hapa kusema kwamba leo tupunguziwe gharama ya unit kwa kila mwananchi, huko siko ninapotaka Kwenda, lakini hoja yangu ni kwamba kwa sababu maji ni huduma, na kwa sababu maji yanapokuwa yamewafikia wananchi yanaleta furaha kwa wananchi, na ni kwa sababu pia ni kigezo chetu cha maendeleo, tumependekeza katika Kamati yetu kwamba hebu Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati, tunaelewa wameshaanza vikao lakini vikao vifikie mahali vikamilike na wakubaliane. Makubaliano tunayoyapendeleza ni kwamba, Wizara ya Nishati itoe bei maalumu kwa uzalishaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliongea wakati uliopita, tunaendelea kuiongea tena, ni pendekezo letu la Kamati kwamba mamlaka za uzalishaji maji zipewe special tariff ili huduma ya maji iweze kutolewa kwa unafuu na kwa msingi huo maji yaweze kusambazwa na hatimaye tufikie malengo yetu ya kusambaza maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, gharama hizi zinapaswa zisihusishwe; kwa sababu huwa wanachaji bei inayotokana na kuwasha mitambo KVA, pia wanatoa na kodi ya ongezeko la thamani hapo hapo na hata kwa ile mitambo pamoja na mengine yote yanayohusu gharama za uzalishaji maji.

Mheshimiwa Spika, tulitamani kwamba VAT isiwe sehemu ya gharama inayochajiwa, pia gharama isichajiwe ile ya KVA wakati wa kuwasha mitambo. Kwa msingi huo, tunaomba Wizara ya Nishati iwakubalie, isiseme kwamba tuna hoja zetu, nasi tunatafuta fedha, hapana, tunatafuta unafuu ambao utakwenda kwa wananchi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya makubaliano baina ya Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati, tumeweka katika mapendekezo yetu, na tunaomba yafikiwe haraka. Katika mwendo huo huo wa kupunguza gharama za uzalishaji maji, tunaiomba Wizara ya Maji iendeleze na kujiekeleza katika manunuzi ya pamoja (bulk procurement) ya mabomba, madawa ili kwamba iweze kufanikiwa katika kupunguza gharama za uzalishaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya mwisho ambayo natamani kuiongea, taarifa yetu inaonesha kwamba kumekuwa na uhujumu wa miundombinu ya maji na hasa ile mifuniko ya chuma katika mamlaka mbalimbali za maji na mamlaka nyingine zimefikia mahali zinatafuta kuweka mifuniko ya zege ili kuepuka kuibiwa ile miundombinu ya chuma.

Mheshimiwa Spika, sasa hawa wanaoiba mifuniko ya chuma baada ya miradi kuwa imekamilika, wanaipeleka katika chuma chakavu. Katika mwendelezo wa biashara ya chuma chakavu ndiyo hao hao wanaoiba mafuta vya transformer, ni hao hao ambao wanakwenda kuvuta nyaya za SGR, ina maana hawa watu wanaturudisha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi inakamilika, anaiba mifuniko ya chuma; miradi inakamilika anavuta nyaya ya SGR; hawa wanaturudisha nyuma. Maana yake hawafurahi kuona wananchi wanafurahia na kupata raha ya maendeleo yanayotokana na Serikali yao. Hawa sio wa kuvumiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pendekezo letu katika Kamati, tumesema kwamba, Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi wakae Pamoja, waje na mkakati wa pamoja wa kudhibiti wizi wa miundombinu katika sekta hizo. Pia wanapokuwa wamekamatwa hawa watu, tunaamini kwamba Wizara tano zikikaa haziwezi zikakosa njia ya kudhibiti wizi wa miundombinu. Udhibiti huu pia uelekezwe katika biashara ya chuma chakavu hapa nchini, kwa sababu ndiko wanakojificha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaamini kwamba watakapokuwa wamefanya hivyo, biashara ya chuma chakavu itadhibitiwa, pia tutakuwa tumedhibiti uhujumu wa miundombinu yetu katika Wizara ya Maji, katika Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, na ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)