Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai, leo tupo mahali hapa kwa ajili yake.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nichukue fursa hii kukupongeza sana kwa kazi kubwa unayoendelea kuifanya na kusimamia majukumu ya Bunge. Vile vile una majukumu mengine ya dunia, unasimamia vizuri, unatufundisha sana, sana. Maana leo unakuta uko huko, lakini kesho uko Bungeni. Unatufundisha, tunapata somo kubwa kutoka kwako. Mwenyezi Mungu akusimamie kwa haya majukumu, nasi kazi yetu ni kuendelea kukuombea ili Mungu aendelee kukuimarisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii ya kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, na Mgombea Mwenza Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi. Vilevile naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mwinyi kwa kuwa Mgombea kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi kwa upende wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wetu wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa kazi kubwa na nzuri, pamoja na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa sana kupitia miradi mbalimbali ya maji. Tusimsahau Katibu Mkuu wa Wizara Eng. Mwajuma, Naibu wake, pamoja na Menejimenti yote ya Wizara kwa kazi kubwa. Tusiwasahau pia Watendaji wakuu wa RUWASA pamoja na Mfuko wa Maji kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Tunaona jitihada zao, wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mapendekezo yetu ya Kamati, naomba nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Wajumbe wote wa Kamati yetu ya Maji na Mazingira kwa kazi kubwa ya kuendelea kuchambua utekelezaji wa Ilani ya mwaka mzima wa Wizara zote mbili; Maji pamoja na Mazingira.

Mheshimiwa Spika, naenda kwenye kipengele cha magari. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kurahisisha kuwa magari yananunuliwa katika mikoa yote nchini, kuhakikisha visima vya maji vinachimbwa wakati wowote na muda wote. Naomba niipongeze Wizara kwa usimamizi wake pamoja na RUWASA ambao ndiyo waliopewa majukumu makubwa ya kuhakikisha kwamba visima vinachimbwa katika maeneo yetu ya vijiji pamoja na vitongoji katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi ni nzuri na Mheshimiwa Rais alinunua magari haya kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Watanzania wote na akina mama wanatuliwa ndoo kichwani. Ni jitihada kubwa ya Mheshimiwa Rais, lakini kutokana na mfumo ambao ulikuwepo wa bajeti, kidogo hatuunganishi bajeti pamoja na visima.

Mheshimiwa Spika, visima vinachimbwa, lakini vinakaa muda mrefu ndipo vinakuja kujengwa na wananchi kupata maji. Sasa tunavyochimba vile visima tunawapa matamanio wananchi. Maji yanatoka kwa wingi, lakini yanafunikwa na tunakaa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba niishauri Serikali kuwa sasa hivi twende sambamba; uchimbaji wa visima na bajeti kwa sababu tunachimba visima, halafu tunakuwa hatuna bajeti, hatimaye tukipata bajeti yake ndiyo tunajenga miundombinu.

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali kwamba sasa hivi twende kwa bajeti pamoja na kisima. Tukichimbe kile kisima na tukijenge ili yale matarajio ya wananchi yaweze kutimia. Vile vile, ile hatima ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama iweze kutimilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya kupitia Wizara ya Maji. Wanafanya kazi kubwa, wanahakikisha usiku na mchana wanatafuta fedha kuhakikisha ile miundombinu inatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze sana Mkurugenzi wa Mfuko wa Maji. Tuna Mfuko wa Maji ambao tunautegemea sana, lakini ule Mfuko wa Maji, fedha inayokusanywa na matarajio ya kwenda kwenye mfuko ni fedha ambayo haikidhi mahitaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukusanyaji mzuri ambao Serikali inaendelea kukusanya kupitia TRA, tulikuwa tunaomba kupitia yale malengo ambayo yalikuwa yamekadiriwa kupelekwa kwenye mfuko wa maji, yapelekwe ili ule mfuko uweze kufanya kazi vizuri, wakandarasi wetu waweze kulipwa na mambo yote yaweze kufanyika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina Wizara mbili, naomba nimpongeze sana Waziri wetu wa Mazingira, Mheshimiwa Masauni, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Menejimenti yote ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kazi kubwa nzuri ambayo wanaifanya, na leo hii tumeona jitihada kubwa ya Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mazingira; jitihada ambayo itawezesha sheria kubadilishwa na kuboresha sekta mbalimbali za mazingira kule ambako kulikuwa kuna tofauti, au ambako mwenendo ulikuwa siyo mzuri. Kutokana na hii sheria itakayokuja, tutapata mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona na mapitio ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesema kwenye carbon, hewa ukaa ambako hakukuwa na sheria, lakini tunatamani sheria ikija ielekeze ili mambo yaweze kuwa vizuri. Naomba tumpongeze sana Mheshimiwa Waziri Masauni kwa kutuletea sheria ambayo itakuja humu Bungeni kuhakikisha tunaboresha zaidi.
Mheshimiwa Spika, nisiache kuzungumzia Wizara ya Maliasili. Mimi nina mbuga kule ya Katavi. Naomba nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuisimamia Kamati, lakini nilikuwa naomba nimpongeze Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Pindi Chani.

Mheshimiwa Spika, Mbuga yetu ya Katavi bado haijatangazwa vizuri. Mbuga hii kwa sababu ni kubwa na ina wanyama wakubwa, tukiitangaza vizuri tutapata mafanikio makubwa sana. Tunaona jitihada za Mheshimiwa Rais, alitangaza nchi yetu kupitia utalii, na leo tunaona manufaa makubwa. Sasa naomba Wizara itangaze utalii wa mbuga ya Katavi ili tuweza kuendelea kupata mafanikio makubwa ya mapato katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)