Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Kasalali Emmanuel Mageni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima.

Mheshimiwa Spika, kabla sijasema sana, nikipongeze Chama cha Mapinduzi kwa mkutano bora kabisa kuwahi kutokea na ambao umeonesha ni namna gani Chama cha Mapinduzi kimejipanga kuendelea kuwaongoza Watanzania na kuwatumikia.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Mgombea Mwenza Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa na Mkutano huo bora kabisa wa CCM kuipeperusha Bendera ya Chama cha Mapinduzi. Pia nampongeza Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kwa kishindo na Mkutano huo kupeperusha Bendera ya Chama cha Mapinduzi kule Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niko kwenye Kamati ya Maji na Mazingira, lakini kabla sijasema sana kwenye Kamati ya Maji na Mazingira, katika Kamati zote zilizowasilisha leo, Wenyeviti wameonesha umahiri mkubwa sana. Mheshimiwa Mnzava na Mheshimiwa Kiswaga wamewasilisha vizuri maoni ya Kamati zao; na kwa kweli hiyo ni dalili njema ya kwamba viongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi ni wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Waziri wa Ardhi, ndugu yangu Mheshimiwa Deo. Nilimwona pale anateta na Mheshimiwa Jerry Silaa; najua amepokea kijiti kutoka kwake. Mazuri aliyoyafanya Mheshimiwa Jerry Silaa bado anaendelea kuyafanya, na kazi anaifanya vizuri sana. Mungu ambariki, aendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye michango ya Kamati niliyomo ya Maji na Kamati ya Mazingira. Tunayo mambo mengi ambayo tumeyazungumza hapa. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye sekta ya maji na mazingira, lakini yapo mambo ambayo nilitamani Bunge hili sasa tuyajadili na tuishauri Serikali namna ya kuyafanya yawe mazuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, historia inaonesha Kamati imekuwa ikiishauri Serikali zaidi ya mara tatu hadi mara nne kuhusu Mamlaka ya Mazingira, kuhusu NEMC kuwa mamlaka kamili. Kamati imekuwa haishauri jambo hili, kwa bahati mbaya, imekuwa ikilishauri kwa makusudi kwamba tupate mamlaka ambayo itasimamia mazingira kwa ubora na bila kuingiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mazingira ni jambo la muhimu sana, lakini kwa bahati mbaya tumekuwa tukilichukulia poa, tunachukulia kama jambo la kawaida, lakini mazingira ni jambo ambalo linahusu uhai wetu na usalama wa nchi yetu, na ni jambo ambalo tusipolipa ukubwa wake na umuhimu wake tunaweza tukaishia pabaya sana. Sasa naomba kupitia nafasi hii kuishauri Serikali ielewe kwamba upo umuhimu wa kuja na sheria nzuri ambayo inaifanya NEMC kutoka kuwa chombo tu cha kuzungumza kuhusu mazingira, sasa kiwe chombo chenye mamlaka kamili inayosimamia mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa na NEMC ambayo, na sisi sote ni mashahidi. Mimi sijakuwepo muda mrefu lakini nilikuwepo; wakati ninakua kulikuwa kuna vitu vinaitwa night clubs. Wakati nasoma UDOM hapa tulikuwa tunaenda Club Fifty-Four, Club la Aziz, Club Seven; yaani ukitaka kwenda Club unakwenda kwenye chumba ambacho kimefungwa, unapigiwa kelele wewe mwenyewe mwenyewe mle, ukimaliza unatoka nje.

Mheshimiwa Spika, tumebadilika ghafla kutokana na kutokuwa na mamlaka, na sasa hivi clubs ziko nje. Yaani mtu akiamua kupiga muziki, anapiga muziki mpaka asubuhi, na majirani wote hamlali, na yeye halali. Sheria ipo, lakini kwa sababu NEMC haina meno, leo inafunga club, kesho Mkuu wa Wilaya anasimama anafungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakuwa tunatengeneza Taifa la watu ambao hawalali; watu ambao siyo kwamba hawalali kwa sababu wamekwenda club, ila hawalali kwa sababu kuna watu wameamua wasilale, na nchi ipo, na mambo yapo. Sisi tunawaambia tengenezeni NEMC ambayo ita-regulate hivi vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, duniani kote haya mambo yanasimamiwa vizuri. Hatuwezi kuwa na nchi tunasema kwamba tuna miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza kuna uchafu tunaukusanya. Yale magari yanayobeba uchafu na yenyewe ni uchafu.

Mheshimiwa Spika, nafikiri wote ni mashahidi na mnaona. Yaani suala la mazingira tunalichukulia poa. Ni lazima tupate mamlaka kamili inayosimamia suala la mazingira. Nadhani nchi yetu itakuwa na nafuu sana kuanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye suala la maji. Mimi naweza kuwa shahidi dhahiri wa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kwenye suala la maji. Mimi ni Mbunge wa Sumve, ninatoa mfano wa Sumve ili tuelewane vizuri. Mimi Mbunge wa Sumve kabla Mheshimiwa Dkt. Samia hajawa Rais wa nchi yetu, kulikuwa kuna vijiji sita tu kati ya 60 kwenye Jimbo la Sumve ambavyo wananchi walikuwa wanaweza wakaenda kwenye bomba wakafungua maji yakatoka.

Mheshimiwa Spika, leo ninapozungumza, vijiji ambavyo tukienda tunafungua maji yakatoka viko 26 ndani ya huo muda mfupi. Vijiji ambavyo wakandarasi wako site ili na vyenyewe tufungue maji, acha kupampu hivi, kufungua, ambavyo wakandarasi wako site na wanaendelea na kazi ni vijiji 13. Kwa hiyo, ukiangalia katika muda huu kutoka vijiji sita mpaka 39 ni mafanikio makubwa sana ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakumbuka nilisimama hapa nikasema Jimbo la Sumve liko Mkoa wa Mwanza, lakini ni jimbo pekee ambalo ladha ya maji ya Ziwa Victoria hatuijui. Hivi ninavyozungumza ipo miradi miwili; mradi wa kwanza una thamani ya shilingi bilioni 32, uko 30%, utekelezaji unaendelea. Mheshimiwa Rais ametupa shilingi bilioni 32 sisi watu wa Sumve. Mradi wa pili Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 20.5 na wenyewe uko 25% ya utekelezaji, ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Aweso, Naibu wake mdogo wangu Mheshimiwa Eng. Kundo pamoja na Katibu Mkuu Mwajuma, wanamsaidia vizuri sana Mheshimiwa Rais kwenye sekta ya maji. Wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, ambacho nataka niiombe Serikali ili tuendelee na hatua hii na mafanikio haya, kwanza fedha za mfuko wa maji zisichezewe, yaani fedha ya Mfuko wa Maji iende kwenye maji ili miradi ya maji iende vizuri. Vilevile tuongeze fedha kuwalipa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii miradi mingi ya maji pia kwa asilimia kubwa kwa sababu ndiyo mingi, imechangia sana kufilisi wakandarasi wazawa wa Kitanzania kwa sababu wakandarasi wanakwenda kujenga miradi, wanakomea kuikopesha Serikali na inawalipa baada ya miaka kadhaa, wakati huo huo wana mikopo kwenye mabenki, wanadaiwa riba.

Mheshimiwa Spika, sasa ni wakati Serikali, fedha ya maji ipewe kipaumbele na bajeti ya maji inapopitishwa na Bunge lako Serikali itekeleze kama tulivyoelekeza; na fedha Mfuko wa Maji tunayoitunza ambayo inaelekezwa inatoka wapi na ikatumike na na kadhalika, iendelee kutumika inavyopaswa. Vinginevyo, tunaweza kupunguza speed ya Mheshimiwa Rais ya kuwaangalia Watanzania kwenye suala la maji, ambayo imeonekana dhahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya mazungumzo hayo, naomba kuunga mkono haoja, nakushukuru sana. (Makofi)