Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia taarifa za Kamati hizi mbili. Niungane na wenzangu kuwapongeza Chama cha Mapinduzi kwa kufanya maamuzi ya busara na makini kabisa ya kuwapitisha wagombea wetu.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kwa kura 100% kuendelea kuwatumikia wananchi wa nchi hii. Vile vile nampongeza Mgombea Mwenza, Mheshimiwa Balozi Dkt. Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kuwa Mgombea wa Urais Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Mawaziri wa Wizara hizi zote mbili, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote ambao wamesababisha haya mazuri tunayoyaongea katika Wizara hizi; Wizara ya Ardhi, Maliasili, na Maji kwenda vizuri kama ambavyo wote tumeona Wizara hizi zimefanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuipongeza Wizara ya Maliasili kwa kuendelea kuboresha mapato, lakini kuendelea kutimiza lengo la watalii. Wote tumejionea, sasa tumefika lengo la watalii milioni 5.3 kuingia nchini. Hii ni kwa sababu ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia picha ya Royal Tour; amekuwa kinara wa utalii na matokeo tumeyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona Wizara hii inachangia pato la Taifa kwa 22.5%, kwa kuingiza Dola za Kimarekani bilioni 3.6 kwa mwaka. Haya ni mafanikio makubwa sana, hatupaswi kuyafumbia macho, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, nitatoa ushauri kidogo kwenye Wizara hizi. Wote tunafahamu umuhimu wa kupanga matumizi bora ya ardhi ya vijiji vya nchi hii. Kupitia taarifa ya Mwenyekiti wetu makini, Mheshimiwa Timotheo Mnzava, mmeona vijiji 65% bado havijafanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, hali inayochangia migogoro ya ardhi kwenye mipaka ya vijiji, mipaka ya wilaya, lakini migogoro ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi imepokea shilingi bilioni tano kwa ajili ya fedha za maendeleo, ambayo ni 42% tu ya pesa ambazo walizitegemea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali iendelee kupeleka fedha kwenye Tume ya Mipango, ili iweze kupanga vijiji vya nchi hii, 65% ambayo bado.

Mheshimiwa Spika, Tume hii inahitaji shilingi bilioni 120 tu kuipanga nchi nzima. Kwa hiyo, naomba niishauri Serikali iipelekee Tume shilingi bilioni 120, ili vijiji vyetu viweze kufanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, ili kuepusha migogoro hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunayo programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kupitia Wizara yetu ya Ardhi. Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi bilioni 50 kwenye halmashauri 57 ili ziweze kufanya mpango huo.

Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha kabisa, fedha zile zilitakiwa zirejeshwe. Fedha hizi zimetolewa mwaka 2018, lakini ni zaidi ya miaka sita sasa halmashauri hizi hazijaweza kurejesha fedha. Halmashauri zilizorejesha ni halmashauri 17 tu. Tunaiomba Wizara ya TAMISEMI isimamie halmashauri hizi ili ziweze kurudisha hizi fedha. Kiasi cha shilingi bilioni 22.5 bado hakijarudishwa.

Mheshimiwa Spika, hizi fedha ni kwa ajili ya kurudi kwenye mfuko ambao uliandaliwa na Wizara ili ziwe zinazunguka, ili sasa halmashauri zote ziweze kupimwa. Tunaomba TAMISEMI itusaidie, tukishirikiana na Wizara ya Ardhi fedha hizi ziweze kuja, kwa sababu kwa kweli Wizara hii jukumu lake kubwa ni kupanga na kupima ardhi yetu, na bila fedha hawataweza. Kwa hiyo, fedha hizi shilingi bilioni 22 zirudishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa Serikali iangalie Wizara yetu ya Ardhi iweze kuipatia fedha ili iweze kupanga nchi hii na kupunguza migogoro, ili Mawaziri badala ya kushinda na kutatua migogoro, basi waendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naounga mkono hoja. (Makofi)