Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, kwa dakika hizi zilizopunguzwa, naomba Mungu anijaalie angalau niweze ku-cover machache niliyokuwa nimepanga kuyasema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono mada zote mbili, au hoja zote mbili zilizoko Mezani. Nawapongeza Wenyeviti, wamefanya kazi nzuri pamoja na Wajumbe wao. Pia, naomba kupongeza Wizara zenyewe husika, ambazo zinahusika kwa kazi nzuri walizofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la changamoto ambazo zimeonyeshwa na Kamati ya Ardhi na Maliasili kwamba, pengine wanashindwa kufikia bajeti zao walizowekewa katika utendaji kutokana na mwingiliano wa kazi kama ambavyo imeonyeshwa na Kamati yenyewe.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ardhi pamoja na TAMISEMI kuna mwingiliano mkubwa katika suala zima la utendaji. Matokeo yake sasa inakuwa ni ngumu, nani umkamate, nani ambaye amefanya vibaya, na nani kafanya vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mchakato wa kugatua madaraka, hasa pale walipofanya kwenye Wizara ya Maji, wakaanzisha RUWASA, na kwenye miundombinu TARURA ikatengwa peke yake, na ardhi ilitakiwa kuwa pia imetengwa kwa ajili ya kuwa na Wakala atakayesimamia Sekta ya Ardhi mwanzo mwisho, na mchakato ulikuwa umeshaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani tunafikiria pengine Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi ingeweza kuongezewa majukumu, na ikapewa jukumu hilo la kuhakikisha ardhi ya nchi hii inasimamiwa vizuri, kwa sababu Tume inafanya vizuri. Watalaamu walikuwa wanafanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa Serikali iangalie suala zima la kugatua madaraka katika suala zima la usimamizi wa ardhi, na kuweka Wakala atakayefanya kazi nzuri kama wanavyofanya TARURA pamoja na Maji, kwa sababu Serikali tayari ilishatoa Waraka wa kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili lilikuwa ni hatua nzuri ya kuwa na ule Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki, ambapo nasikitika kwamba mradi huo umesimama. Mradi huo ulikuwa unakwenda kuimarisha hasa miundombinu katika idara nzima, au Wizara nzima, kuanzia wilayani, mikoani, na mpaka Taifa, lakini naona kama mradi ule umeondolewa, pamoja na kusitishwa kwa kurasimisha viwanja 1,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale tulikuwa tunakwenda kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapa umiliki wa maeneo yao. Sasa unapositisha maana yake mwananchi huyu alishajenga bila utaratibu, lakini tulimwachia akajenga mpaka akafikia hapo alipo. Leo hii anataka kumilikishwa ili angalau hata katika uboreshaji awe na kitu ambacho atasimama nacho. Leo tunasema wasiwezeshwe hivyo. Kwa kweli katika kusimamisha miradi ile ni makosa makubwa ambayo sijui kwa nini ilifanyika hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia watu tunakwenda katika halmashauri zetu. Tunaangalia Idara za Ardhi jinsi zilivyo na ofisi duni katika utendaji, ukiacha zile ambazo wamejenga majengo, lakini unaingia kwenye ofisi mpaka unasikitika. Chumba kimoja wamekaa watu saba au nane, halafu leo tunasema wasijengewe ofisi, na pesa ilikuwa imepatikana. Hata nyaraka nyingine zinapotea kwa sababu ya namna ya kulundikwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba ku-declare interest kwamba wakati niko Wizarani tulikwenda Tabora. Tulikuta wamekaa kwenye chumba kimoja kama corridor, na mafaili yamejaa mle. Kutafuta tu faili la mtu mmoja linachukua muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, sasa kama leo tunasema hatuwezi kuwapa nafasi ya miundombinu wakawa na ofisi nzuri, sijui tunataka nini kifanyike pale? Nadhani katika hilo tumekwenda vibaya katika suala zima la kuwawezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mradi wa KKK ambao ulikuwa umepangwa, Kupima, Kupanga na Kumilikisha, nao naomba pia tuangalie vizuri. Serikali iangalie namna ambavyo pesa za Serikali zinatoka. Mwaka 2018/2019 zilitoka zaidi ya shilingi bilioni sita kwa halmashauri 24, lakini zilizokamilisha kulipa ni halmashauri 13 tu. 10 zote hazijalipa, na moja haijalipa kabisa. Halmashauri ya Nzega haijalipa hata senti tano. Sasa sijui wana mpango gani? Maana yake zile fedha zingeweza pia kwenda kwa wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zile pesa zinakuwa ni seed money kwao, lakini ukizitumia vizuri unaweza ukajikuta umepima wilaya yako kwa 100%, kwa sababu zinazalisha fedha nyingi kuliko hata maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2021/2022 zimetoka shilingi bilioni 50 kwa halmashauri 57. Kati ya hizo ni halmashauri 19 tu zimelipa 100%; halmashauri 38 zimelipa nusu, nyingine hazijalipa. Kama fedha ya Serikali inatoka kwa utaratibu huo, halafu hairudishwi, na mpango wa Serikali ni kuhakikisha nchi nzima inapimwa, sasa kwa style hii hatuwezi kumaliza.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme, kama fedha hizi zikitumiwa vizuri, ni mradi mmoja mzuri ambao unawezesha kupima ardhi hii kwa haraka sana. Naweza kutolea mfano wa wilaya ninayotoka, Manispaa ya Ilemela. Hii imebakiza kama 12% kuipima kwa 100%, kwa sababu ya kuwezeshwa na Mfuko huu, na walilipa kwa 100% na halmashauri nyingine zilifanya vizuri. Kwa hiyo, nasema mradi huu usimamiwe vizuri ili uweze kuona ni jinsi gani ambavyo tunaweza tukaipima ardhi hii. (Makofi)
(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, upande wa Tume ya Matumizi ya Ardhi, naomba kusema wamefanya kazi vizuri.
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ni ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilifikiri ya kwanza. Ahsante, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)