Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chwaka
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuweza kunipatia nafasi hii. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutupatia uzima wa kuweza kufika katika Bunge letu Tukufu.
Mheshimiwa Spika, aidha, nawapongeza viongozi wetu wakuu wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia, Dkt. Nchimbi na Mheshimiwa Dkt. Hussein, kwa kuteuliwa kwao. Hii inaonyesha wazi kwamba wamefanya kazi ipasavyo, na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wakaridhika kwa kazi yao ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawaomba Watanzania, kazi zao zinaonekana, hazikujificha, wawaone na wawatambue, ikifika mwezi wa Kumi mwaka huu wawape tu kura zote za Ndiyo viongozi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepata bahati ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maji na Mazingira. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, Kamati zote ambazo leo zimeweka ripoti zao za mwaka, naunga mkono hoja zote ambazo zimezungumzwa na Kamati zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze na kusema bajeti ndogo ya Wizara ya Maji. Maji ni uhai. Maji ni muhimu sana katika shughuli zetu za siku zote. Maana yake hakuna siku ambayo utakosa maji ukafurahi. Maji yanatakiwa kupatikana kila siku, lakini bajeti ambayo inatengewa na Serikali ni ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2024/2025 haikuridhisha, na tulisema sana wakati wa bajeti. Kwa hiyo, tunaikumbusha Serikali mapema, kuona Bajeti ya mwaka 2025/2026 iweze kutimiza angalau zile ndoto za Wizara na Kamati.
Mheshimiwa Spika, sisi Kamati tunaishukuru sana Wizara kwa sababu inafanya kazi kubwa sana. Kwa ushauri wangu, kipindi hiki wapewe fedha nyingi ili tuwaone wanafanya kazi zaidi, kwa sababu muda ambao wanafanya kazi hautoshi kutokana na fedha wanazopewa. Tuwape fedha nyingi ili watimize shughuli ambazo wamepangiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kulionyesha hili, nimekuja na bajeti za miaka mitatu, kuonyesha kwamba badala ya kuwa tunaenda mbele, bajeti iongezeke, lakini bajeti imepungua. Tukiangalia mwaka 2022/2023, bajeti ya maendeleo ilikuwa shilingi bilioni 657.9. Bajeti ya maendeleo ya mwaka 2023/2024 ilikuwa shilingi bilioni 695.8. Bajeti ya mwaka 2024/2025 ilikuwa shilingi bilioni 558. Hapa imepungua, na mahitaji yameongezeka (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yetu inaongezeka mahitaji kila siku. Watu wanaongezeka kila mwaka, maana yake bajeti iweze kuongezeka. Tunapokwenda kupunguza bajeti, maana yake hatujawafanyia vizuri wananchi; kwa sababu wananchi wanaongezeka, lakini sisi tunapunguza bajeti. Kwa hiyo, tunashauri bajeti ya mwaka 2025/2026 iongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuzungumzia suala la upotevu wa maji. Suala hili limezungumzwa na wadau wenzangu, lakini suala la upotevu wa maji, mara nyingi yanapotea katika mitazamo miwili tofauti. Kuna ule wa kibinadamu ambao watu wanatumia maji isivyo halali, lakini kuna ule wa miundombinu, ambayo yote ukiiangalia inarudi nyuma kwenye bajeti ndogo.
Mheshimiwa Spika, unapokuwa na bajeti ndogo, na huku una miundombinu chakavu, maana yake huwezi kwenda kutatua matatizo ya miundombinu chakavu. Kwa hiyo, maji yanapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitazama upotevu wa maji unavyotakiwa Kitaifa na Kimataifa, maana yake usizidi 20%, lakini leo maji yanapotea kwa 36.2%. Maana yake maji yanapotea kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na muda, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)