Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. SOUD MOHAMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia ripoti za Kamati zetu mbili hizi. Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na ripoti ya Maji na Mazingira.

Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi katika ripoti ya Kamati ya Maji na Mazingira, na nitaanza na Mazingira. Kwanza, nakushukuru na nawashukuru Wenyeviti kwa kuwasilisha vizuri ripoti zote. Hata hivyo, napenda vilevile kuwashukuru sana Watendaji wa Wizara hizi mbili zikiwemo Wizara ya Maji na Mazingira pamoja na Wizara ya Mazingira kwa ujumla, wamefanya vizuri sana katika uwasilishaji na utayarishaji wa kazi ambazo zimesababisha sisi kuandika ripoti hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza tu, Mheshimiwa Mwenyekiti amezungumza hapa kuhusu masuala ya maazimio ambayo yamefanyiwa kazi na yale ambayo hayakufanyiwa kazi vizuri. Sasa nitajikita zaidi katika maazimio ambayo hayakufanyiwa kazi, na Azimio hili moja kubwa ambalo halikufanyiwa kazi, ni Azimio la kuifanya NEMC kuwa mamlaka.

Mheshimiwa Spika, hili ni agizo la Bunge lako Tukufu hapa na tulikaa kwa pamoja na tukakubaliana kwamba kutokana na changamoto za kimazingira, ambazo hivi sasa zinaathiri nchi yetu, basi ni vyema NEMC itoe neno ili iweze kufanya kazi vizuri. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri alikuja hapa na akaahidi japo siyo Mheshimiwa Waziri huyu ni yule ambaye ameondoka.

Mheshimiwa Spika, hivyo, aliahidi kwamba katika marekebisho makubwa yanayokuja ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, basi suala la NEMC kuwa mamlaka litazingatiwa. Kwa hiyo, tunategemea sana kwamba sheria itakayokuja, basi italizingatia hili.

Mheshimiwa Spika, kuna suala zima la sheria hizi ambazo zimekuja kurekebishwa na kuweza kuzisaidia hizi kampuni za kufanya wa Environmental Impact Assessment kuweza kuwa na masharti ambayo yatazingatia uwepo wao.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna shida ambayo vilevile imejitokeza kwa sababu makampuni ambayo hapo mwanzo yalikuwa yamesajiliwa kuweza kufanya kazi za Environmental Impact Assessment, mengi yao kutokana na masharti ambayo yameletwa, yamefanya kwa kiasi fulani, yasiweze kuzingatiwa, na hili limesababisha kusitisha baadhi ya kampuni, ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu ambavyo vina wanafunzi wanaofanya kazi katika makampuni hayo kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari ya mazingira (Environmental Impact Assessment).

Mheshimiwa Spika, naomba tu kwamba, kwa sababu ilikuwa ni takwa la Azimio kwamba waje na kanuni wazipitie, kanuni ambazo zina ukakasi na zinakwamisha makampuni haya kufanya usajili, basi naomba sana Mheshimiwa Waziri zile kanuni ambazo zilikuwa zimeainishwa na Bunge na zikaonekana zina ukakasi na mpaka leo hazikufanyiwa marekebisho, basi zikafanyiwe marekebisho ili turuhusu hizi kampuni hasa za Vyuo Vikuu na zile kampuni ambazo vijana wetu ndio wanatafuta ajira kutokana na shughuli hizi, basi waweze kufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala zima la hii Sheria yenyewe ya Usimamizi wa Mazingira ambayo vilevile ilikuwa ni miongoni mwa maazimio ya Bunge.


Mheshimiwa Spika, pia tulitegemea kwa sababu imeshasomwa kwa mara ya kwanza, hivyo, tunategemea itakapokuja, hapa vilevile itazingatia yale mambo muhimu ambayo Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba yatakuwemo katika hii sheria.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, ni suala zima la kufanya uratibu wa hewa ukaa au carbon itazingatiwa kwa kuwa na Mamlaka ya hewa ukaa, hili nafikiri litazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi. Kuna Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi ambao upo sasa hivi, lakini hauzingatii mabadiliko ya tabianchi, unazingatia tu masuala ya mazingira.

Mheshimiwa Spika, sasa tulitegemea kwamba sheria hii itakaporekebishwa, itakuja na marekebisho ambayo mfuko huu utakuwa umeongezwa element ya mabadiliko ya tabianchi ili tuweze kusaidia kupata rasilimali fedha za kusaidia shughuli mbalimbali za mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambazo hivi sasa nyingi zinakwama kutokana na uchache wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie la mwisho katika suala la sekta ya maji. Kama tunavyofahamu kwamba sekta ya maji, ni sekta muhimu na zaidi ya miradi 1,000 hivi sasa inaendelea kutekelezwa katika nchi yetu na kutokana na uwasilishwaji, wenzetu wanasema kwamba ni miradi 240 tu ambayo ndiyo imekamilika na zaidi ya miradi 700 bado haijamalizika, iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri na hasa Waziri wa Fedha awapatie fedha ili miradi iweze kukamilika, kwa sababu kutokana na bajeti kuwa ndogo inaonekana wazi kwamba hii miradi inasuasua.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)