Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika taarifa za Kamati zilizopo Mezani. Nami niungane na Wabunge wengine kuwapongeza Wenyeviti wote kwa uwasilishaji mzuri wa ripoti za Kamati. Nitachangia katika maeneo matatu. Kwanza ni kwenye sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana umuhimu wa sekta ya utalii katika nchi yetu, kwa maana ya kukuza uchumi wa nchi, lakini kuingizia nchi fedha za kigeni. Siyo hilo tu, katika sekta hii pia tumeona utayari wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais, ambaye kwa yeye mwenyewe kujitolea kutoka ofisini na kwenda uwandani, katika maeneo ya vivutio, na kutengeneza filamu maarufu ya Royal Tour ili kutangaza Tanzania huko duniani, kuelezea tuna nini na nini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa utayari huu wa Mheshimiwa Rais, kama Mkuu wa Nchi, maana yake sekta hii ni muhimu sana na inapaswa sasa wale ambao ni wasaidizi wake wahakikishe kwamba sekta hii inakua. Pia, kwa sababu sasa tunaona kuna ongezeko kubwa la watalii, maana yake nasi tuwe na mazingira ambayo tayari tumeshayaandaa kuwapokea watalii hawa.
Mheshimiwa Spika, jitihada hizi zinaenda kuongeza utalii. Hivyo, baada ya ile filamu, tutarajie baada ya miaka miwili mitatu ijayo ambayo sasa ndiyo tunaanza kuifikia hili ongezeko, litakuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, pia tutarajie kwamba mtalii huyu atakapofika, anapokwenda kwenye hiyo miundombinu iliyoko kule, iwe rafiki na imfikishe kwa urahisi ili aone kile ambacho amekiona na Mheshimiwa Rais ameitangazia dunia kwamba Tanzania tuna nini na nini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa miundombinu yetu hasa kwenye hifadhi ambayo inajulikana kama hifadhi bora Barani Afrika ambayo ni hifadhi ya Serengeti na imepata tuzo miaka sita mfululizo kwamba ni hifadhi bora iliyoko barani Afrika. Barabara za kule kwa kweli ni mbovu, na nyakati za masika, kupita ni changamoto.
Mheshimiwa Spika, tunaomba na kuishauri Serikali, ilichukulie jambo hili kwa uzito kuhakikisha kwamba tunaimarisha hizi barabara hasa hii ya Serengeti na barabara nyingine zote zilizoko katika hifadhi zetu, ili hizi jitihada zilizofanywa na Mheshimiwa Rais zisiende bure, watalii hawa wakija waweze ku-enjoy na kuona yaliyomo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tuhakikishe utoaji wa huduma pia uwe bora. Siyo tu utoaji wa huduma, upungufu wa malazi tuliyonao leo tuone namna gani ya kuimarisha na kuboresha na kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa vyumba vya malazi kwa ajili ya wageni kwa mwaka mzima bila kuwepo na changamoto yoyote. Kwa hiyo, huo ni ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tulishauri mara nyingi, kwenye hizi taasisi zetu, lazima wabakiwe na fedha, kitu kinachoitwa retention. Hii ni kwa sababu hizi taasisi zinafanya kazi za operation, wakati mwingine doria mara kwa mara ni muhimu, kuliko fedha zote zikusanywe ziingie kwenye mfuko mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana baadhi ya fedha wakabakiwa nazo ili pale panapotokea na mambo ambayo yanatakiwa kufanyika kwa haraka, hizi fedha waweze kupatiwa na kubaki kufanya kazi. Kwa mfano, hawa wanaofanya operation wakisikia kuna ujangili umetokea mahali, hawawezi kusubiria fedha ziletwe kutoka Hazina wakapambane na ujangili mahali fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muhimu wawe na hizi fedha. Tumesema mara nyingi na tumeshauri mara nyingi, tunaomba hili lifanyike. Hizi taasisi zetu TANAPA, Ngorongoro, TAWA na wengineo waweze kubakia na hizi fedha kwa ajili ya kufanikisha majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, pamoja na faida za kiutalii, kuna changamoto kwa upande wa wananchi. Wanyama hawa wanaenda kuvamia maeneo ya wananchi, wanaharibu, na wananchi hawapewi fidia. Tunapongeza kwamba kuna jitihada zimefanyika, angalau wananchi wamepewa fidia.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ni vema mkaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wale ambao tayari wako kwenye list ya kupewa fidia kwenye baadhi ya maeneo, kwa maana ya nchi nzima, waweze kulipwa fidia zao kutokana uharibifu walioupata kwa wanyama kuvamia kwenye mashamba yao, kuwajeruhi, wengine kufariki na vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kazi nyingine kubwa ya Wizara hii ni kulinda shoroba. Tumeona na kupitia ripoti mbalimbali huko nyuma shoroba zinaendelea kuvamiwa. Kwa hiyo, ni muhimu sana hizi shoroba zikaendelea kulindwa na kutunzwa kwa kiwango kinachotakiwa ili wanyama wanapohama kutoka eneo moja kwenda lingine, basi wahame bila kuwa na usumbufu wowote. Muda umeisha?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa, kengele imeshagonga.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)