Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuyafanya haya, lakini pia nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati hizi mbili kwa uwasilishaji wao mzuri sana.
Mheshimiwa Spika, hata yale yaliyoandikwa humu kwa kweli yamegusa maeneo mazito ambayo wananchi wengi wangetamani kuyasikia.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na mchango wangu, nami niungane na Watanzania wenye mapenzi mema, na wanachama wa Chama cha Mapinduzi, kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa katika kinyang’anyiro cha kugombea Urais itakapofika muda 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Balozi Dkt. John Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza. Sisi wana Nyasa, wana Ruvuma tumefurahi na kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili yake kwamba nasi sasa tunaenda kuchukua nafasi ya kuisaidia nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tumefurahi kwa sababu mwanzo alikuwa Makamu wa Rais ambaye hakuwa kama Mgombea Mwenza, lakini Makamu wa Rais alitokea kule Kigoma na sasa imekuwa Magharibi, tena kule Kusini, hususan Wilaya ya Nyasa. Tunashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Dkt. Hussein Mwinyi, naye pia kwa kupata nafasi yake ya kuendelea kuwa Mgombea kwa ajili ya Urais Zanzibar. Pia siyo kwa udogo wake, nampongeza sana mzee wetu Mheshimiwa Stephen Wasira, kwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, hakika tumeona cheche zake, siku hizi chache alizokaa, anatosha, yaani kwenye Kiti ametosha na kujaa. Kweli mji bila wazee unapwaya, lakini pia mwenyewe ametuhakikishia kuwa yeye ni injini yenye uhai, nguvu na siyo bodi. Kwa hiyo, tunategemea atakisaidia Chama chetu na atamsaidia sana Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, kwanza nawapongeza hawa Mawaziri wote waliowasilishiwa taarifa kupitia Kamati zetu. Suala la mazingira limeitwa ni suala mtambuka (cross-cutting issue) na lipo katika kila Wizara. Linapokuwa halina chombo madhubuti cha kusimamia, kuna maeneo tunakuwa kama hatuendi vizuri. Ndiyo maana Kamati yetu imekuwa ikisimamia sana suala hilo, na tunalizungumza wote mara kwa mara. Hadi humu maazimio yamepitishwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuweka sauti yangu ya kusisitiza, na bahati nzuri Waziri wa Wizara ya Mazingira amekuwa msikivu pamoja na Katibu wake Mkuu tulipowashauri kwenye Kamati yetu, na hivyo kuwaahidi kuleta sheria hii mapema iwezekanavyo. Tunaomba atusaidie kuwezesha hilo ili kweli chombo hicho Madhubuti kiweze kupatikana na mazingira yaweze kusimamiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tungetamani kuona sasa wataalamu wa mazingira na wenyewe wawe na bodi yao ya utaalamu kama ilivyo Bodi ya Wahandisi. Bodi mbalimbali sasa hivi zipo nchini za kusimamia utaalamu, na kwenye mazingira tungehitaji iwe hivyo.
Mheshimiwa Spika, pia tumezungumzia masuala yanayohusu maji. Hivi tunavyoenda kwenye uchaguzi, wanawake wanafurahi, wanamshukuru Mheshimiwa Rais, kwa miradi ya maji mingi ambayo imetekelezwa katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, bahati mbaya miradi mingine haijaweza kutoa maji, matenki yameshajengwa, njia zake kuu za maji zimeshajengwa, nyingine ndiyo zinangoja hizo njia, lakini fedha hazipo za kutosha. Tunaomba sana fedha zipelekwe na mfuko wa maji upewe fedha zake zote ili maji yaweze kuwafikia wananchi hasa wanawake wanaoteseka kutafuta maji mbali. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa, kengele imeshagonga.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, mwisho namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kuwasadia watu wangu waliokufa kwa kukamatwa na mamba ili waweze kulipwa fidia.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.