Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia kwenye Taarifa ya Kamati mbili. Hata hivyo, nitajikita katika Kamati ya Maji na Mazingira.
Mheshimiwa Spika, vilevile nawapongeza sana Wenyeviti wote wa Kamati kwa mawasilisho mazuri, lakini hasa Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na mazingira Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga na Makamu wake Anna Lupembe, Mbunge wa Nsimbo kwa kazi nzuri pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Maji na Mazingira kwa kuendelea kutushauri na kutoa maoni na kuhakikisha kwamba sekta hii inaendelea kuimarika kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, nami niungane na Watanzania kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa Mgombea kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi na Mgombea Mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi pamoja na Dkt. Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja, na vilevile mapendekezo ya Kamati yetu ya Mazingira na Maji. Sisi kama Serikali tunapenda kuyatekeleza kwa kadiri ambavyo Kamati hii imeshauri.
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo machache ambayo ningependa kutoa ufafanuzi kidogo. Kwa upande wa kuwezesha wakandarasi wetu wa ndani na wakandarasi wengine, Serikali imeendelea kutoa fedha kuhakikisha kwamba wakandarasi hawa wanaendelea kulipwa.
Mheshimiwa Spika, pia wakandarasi wa ndani wameendelea kulipwa hadi kufikia 2024, tayari Serikali ilikuwa imeshapokea kiasi cha shilingi bilioni 285 kwa ajili ya kulipa wakandarasi, lakini shilingi bilioni 87 hizi zimelipwa kwa kipindi cha mwezi Januari. Katika fedha hizi, zinaendelea kuhakikisha kwamba local content tunaizingatia, wakandarasi wetu kuwawezeshwa ili waweze kuondokana na madeni ambayo yanawasumbua katika mabenki, kuwa na mwendelezo mzuri katika utekelezaji wa majukumu.
Mheshimiwa Spika, vilevile tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Tutakumbuka mwaka 2021 Mheshimiwa Rais wakati anaingia madarakani, upatikanaji wa huduma ya maji ulikuwa 72% kwa vijijini, na hivi tunavyoongea sasa, upatikanaji wa maji umefikia 87%.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mjini upatikanaji wa maji ulikuwa 86% hivi tunavyoongea ni 91.6%. Upatikanaji wa maji vijijini tulikuwa na vijiji takribani 9,737, hivi tunavyoongea, kuna vijiji 10,532 tayari vimefikishiwa huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba upatikanaji wa maji unaendana pia na kudhibiti namna bora ya kuhakikisha kwamba upotevu wa maji usiwe changamoto kwa Watanzania. Tunaelewa kwamba maji yanaweza yakapotea kwa watumiaji, maana yake wateja kutumia mbinu ambazo siyo salama ambazo haziruhusiwi, lakini vilevile kuna miundombinu inaweza ikasababisha upotevu wa maji, kuna miundombinu ya utunzaji wa maji ambayo inaweza ikasababisha uvujaji wa maji.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba sisi Wizara ya Maji tunakuja na mfumo wa kidijiti kuhakikisha kwamba tunaenda kudhibiti upotevu wa maji nchini. Mfumo huu unaenda kutengenezwa na wazawa kupitia Chuo chetu cha Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfumo huu utaweza kutoa taarifa ya kwamba maji yanavuja katika eneo la tenki au katika eneo la usambazaji wa maji au katika usomaji wa dira au kuna mtu ambaye amechepusha maji ambayo yanaweza kutusababishia upotevu. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba mfumo huu utaweza kutoa taarifa ya namna gani tunaweza kwenda kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti upotevu wa maji, tunaenda kuongeza mapato kutokana na maji ambayo yanawafikia wateja. Napenda kusema kwamba Serikali tumeendelea kujipanga kuhakikisha kwamba lengo kubwa tuweze kuwa na uendelevu katika ujenzi wa miundombinu, lakini tukiwa tunadhibiti upotevu wa maji kwa sababu ni hasara kubwa kwa Taifa iwapo tutaruhusu maji yaweze kupotea.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele imegongwa.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kwamba tumeshaujaribisha mfumo huu na kuna maeneo ambayo tayari tuna 33% tumeshusha mpaka 10%. Sasa tunaendelea kuhakikisha kwamba upotevu wa maji unaenda kukomeshwa kabisa katika Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)