Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, naomba nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuzidi kuniamini na kunipa majukumu mengine ya kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Spika, pia, nichukue fursa hii kuishukuru Kamati ya Maji na Mazingira pamoja na Kamati ya Katiba na Sheria ingawa leo ni kwa sababu tunazungumzia Kamati ya Maji na Mazingira. Naomba kipekee nimshukuru Mwenyekiti, Mheshimiwa Kiswaga na Mheshimiwa Mwakamo; Mwenyekiti Mheshimiwa Lupembe na Wajumbe mahiri kabisa wa Kamati hii ambayo nimeweza kukutana nayo kwa muda mfupi sana toka nipewe dhamana hii.
Mheshimiwa Spika, naipongeza kwa sababu kwa kweli ni Kamati ambayo inaoneka kwanza kuwa na ushirikiano mkubwa. Pia, ni Kamati ambayo ina maono sana na kutaka kuona mabadiliko ya kweli katika sekta ya mazingira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuthibitisha hayo, ni kwamba wakati nilivyokwenda kwenye kikao changu cha kwanza cha Kamati pamoja na timu yetu ya Wizara kwa ujumla wake waliweza kunipa ushauri mzuri sana na leo hapa nimedhihirisha hapa yale ambayo walikuwa wametushauri wameyarudia tena hapa na tuliwaahidi kwamba tutayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumewaahidi kwenye Kamati, naomba mbele yako na mbele ya Bunge hili Tukufu niwaahidi kwamba yale yote ambayo wametushauri tutayafanyia kazi kama ambavyo tumeahidi na hakuna kitu kitabadilika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ufupi niseme yale maoni yote ambayo yametolewa leo hapa kupitia Taarifa ya Kamati na michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ikiwemo Wajumbe wa Kamati na Wabunge wengine ni kwamba tumeyapokea na tutakwenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, katika maoni mengi yaliyotolewa hapa, yamejikita zaidi katika maeneo makubwa matatu. Naomba niyagusie kwa haraka haraka ili kuonesha kwamba kama Serikali, tumedhamiria kuweza kushughulika na hizi changamoto ambazo zimezungumzwa.
Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza na Kamati imeliwasilisha, ni jinsi ambavyo wanakerwa sana na utaratibu wa mabadiliko ya sheria katika maeneo makubwa matatu. Moja, ni eneo la Baraza la Mazingira (NEMC), wamezungumza kwa sauti kubwa sana kuhusu umuhimu wa kutaka kulifanya Baraza letu la Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka. Hii ni hoja ambayo kwa kweli imesisitizwa sana hapa leo na ni hoja ya kipaumbele ya Kamati.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo wameizungumzia sana leo na wameizungumzia kipindi chote tangu nimeanza kuielewa Kamati hii na Wabunge hapa, ni juu ya umuhimu wa kutunga Sheria ya Uchumi wa Buluu. Hoja nyingine ambayo wameizungumzia ni kuhusiana na namna ambavyo Kituo chetu cha Kaboni kitaweza kutambulika kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wamewasilisha hoja hizi mara ya kwanza, nilipokutananao nami niliwaahidi kwamba tutazichukua kama ndiyo kipaumbele changu cha kwanza. Kiukweli tumefanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeshaandaa mpango kazi kabambe toka siku ambayo tumetoka kwenye Kamati. Mpango kazi ule mpaka leo hii tunapozungumza hakuna kipengele hata kimoja ambacho hatujakitekeleza kama tulivyojipangia. Kwa hiyo, tunakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili, nataka nikupongeze sana wewe binafsi, kwa sababu kulikuwa kuna mabadiliko madogo ya sheria ambayo yanahusu mabadiliko ya Sheria ya Mazingira ambayo yalipangwa kuwasilishwa katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya mabadiliko haya madogo hayakuwa yamegusa kwa upana wake matarajio ya Waheshimiwa Wabunge, lakini baada ya kazi ya kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi maoni ya Waheshimiwa Wabunge, ambayo tumeifanya kwa muda mfupi, tuliona kuna mambo mengine ni vema tukayapenyeza kabisa sasa hivi bila kukiuka taratibu za Kibunge.
Mheshimiwa Spika, kwa mwongozo wako, tunakushukuru sana, na leo hii tutaweza kukaa na Kamati ya Bunge kuipitisha ili uone seriousness yetu kama Serikali kwamba hata yale mambo ambayo tumedhani hayahitaji kusubiri tuweze kuyawahisha kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunakushukuru sana na tunaamini kwamba mpango wetu ambao tumejiwekea na dhamira yetu kama Serikali ambayo naizungumza hapa hadharani ya kuhakikisha haya mabadiliko yote makubwa ambayo Waheshimiwa Wabunge wanayataka katika maeneo haya matatu, ikiwezekana katika Bunge lijalo bila kukiuka taratibu zozote nyingine zilizopo katika misingi ya uendeshaji wa Bunge letu na Serikali, tuweze kupitisha na kukidhi matarajio ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, naamini kwa jinsi ambavyo umetupa ushirikiano mkubwa katika kufikisha haya mabadiliko madogo na makubwa, utatusaidia kuweza kutimiza azma hiyo, kwa yale ambayo yanahusu mamlaka yako. Yanayohusu mambo ya Kiserikali tutayapeleka kwa mamlaka husika.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla nimalizie kwa kusema kwamba, hoja hizi ni za msingi sana.
Mheshimiwa Spika, hoja za Uchumi wa Buluu, hoja za Kituo cha Kaboni, na hoja za Baraza la Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka ni hoja zenye maslahi mapana ya Taifa na zitasaidia sana kuleta mabadiliko makubwa sana hususan katika sekta ya mazingira na sekta mtambuka ya Uchumi wa Buluu ambayo inakwenda kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato ya nchi hii na kuongeza mchango katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)