Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika kuhitimisha hoja yetu, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia. Takribani Wabunge 22 wamechangia hoja za leo; na katika hao Wabunge 12 wamegusa Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Waheshimiwa Wabunge tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri sehemu kubwa ya michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge imeendelea kusisitiza mambo ambayo kwa ujumla wake ndiyo tumeyaweka kwenye maazimio ya Kamati. Kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuna mambo makubwa manne yamesemwa. Moja, ni utaratibu wa makusanyo wa taasisi zetu zile za uhifadhi, pia suala la miundombinu kwenye hifadhi.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana na Waheshimiwa Wabunge na tunashukuru wenyewe wamelisema vizuri sana kwamba, shughuli za uhifadhi kwa asili yake zina namna ya tofauti kidogo. Ukisema taasisi zikae kwa kutegemea OC kutoka Serikalini, ikichelewa ni changamoto. Kwa hiyo, ndiyo maana tumeweka azimio lile na tunashukuru kwamba Waheshimiwa Wabunge wameonesha kuliunga mkono.
Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana na tunampongeza Mheshimiwa Rais, amefanya kazi nzuri sana. Mafanikio makubwa tunayoyaona kwenye sekta ya utalii sasa huwezi kumwondoa Mheshimiwa Rais. Tunasema huwezi kuuboresha utalii, ukaongeza watalii halafu miundombinu ikawa hai-support ongezeko hilo la watalii wanaoongezeka. Ndiyo maana tumesema, ni vizuri tuweke azimio hili ili kuhakikisha kwamba taasisi zetu, Wizara na Serikali kwa ujumla zinaendelea kufanya ukarabati wa miundombinu ili iendelee kufaa kwenye maeneo yetu na watalii waendelee kufurahia kutembelea maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, limezungumzwa jambo la mazao mapya ya utalii, amesema vizuri Mheshimiwa Lulida na Mheshimiwa Waziri amesema na kwenye Taarifa pia tumeweka azimio la kuitaka Serikali kuendelea kuvigundua, lakini kuendelea kuvitangaza vivutio vyetu. Tunaamini Serikali ikitekeleza azimio hilo, mipango, ndoto na matamanio haya ya Waheshimiwa Wabunge yatakuwa yamefikiwa.
Mheshimiwa Spika, liko moja hili la hoteli limesemwa vizuri. Tumeweka azimio kwa namna tulivyoliweka na tunashukuru kwa Wabunge wameliunga mkono kwa sababu jambo hili ni la kisheria na lina taratibu zake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba tutahitaji hoteli zirudi Serikalini, lakini hatuhitaji kuiingiza nchi kwenye changamoto ya kisheria. Kwa hiyo, tunaamini likitekelezwa hili azimio kwa namna tulivyoliweka kwenye taarifa yetu tutakuwa tumeisaida Serikali, na nchi kwenye kutatua changamoto hii ya maradhi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya ardhi, jambo kubwa ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelichangia ambalo pia kwenye taarifa yetu limeoneshwa ni migogoro ya ardhi. Sisi kama Kamati tunajua suluhisho pekee la migogoro ya ardhi, moja, ni kuwa na mfumo wa ku-manage ardhi ya nchi yetu, kwamba leo mtu popote alipo akitaka kiwanja au eneo, anajua kwamba nikiingia hapa najua hiki ni kiwanja cha mtu au hiki hakina mtu. Management ya ardhi ikiwa kwenye mfumo, ni rahisi kuzuia migogoro ya ardhi, kwa sababu ni rahisi kutotoa viwanja kwa mtu zaidi ya mmoja, lakini pia na mambo ya namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine la kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi ni kwenye kupanga mipango ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo yetu hasa kwenye maeneo ya ardhi ya vijijini. Ziko tafiti nyingi zinaonesha hivyo kwamba moja ya njia ya kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi hasa kwenye maeneo ya vijijini ni kupanga mipango ya matumizi ya ardhi. Ndiyo maana kwenye taarifa yetu tumetilia mkazo na msisitizo sana kwenye jambo hili na tumeweka azimio na tunaamini kama Serikali ikitimiza na ikitekeleza azimio hili, itatusaidia sana kupunguza changamoto tuliyonayo kwenye migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha, naomba nitumie fursa hii kukushukuru sana wewe kwa namna unavyotuongoza kwenye Bunge lako Tukufu, na sisi wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kweli tunajifunza mengi sana kwako na tunanufaika sana na uongozi wako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee niungane na wengine wote, mwisho lakini siyo kwa umuhimu kuendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Leo tunasherehekea mafanikio makubwa kwenye sekta ya utalii kama nilivyosema, huwezi kumtoa Mheshimiwa Rai, na ninaamini kwa hili na mengine mengi makubwa yaliyofanywa kwenye nchi yetu. Ndiyo maana Chama cha Mapinduzi kilimpitisha kwa kauli moja kuwa mgombea wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha Mapinduzi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika tunampongeze Dkt. Balozi Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi na Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa Urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi. Tunaamini kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali zetu viongozi hawa wanastahili kuchaguliwa tena ili kupata nafasi ya kuiongoza nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naendelea kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kupokea na kujadili taarifa yetu.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)