Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA (MWENYEKITI WA KAMATI YA MAJI NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuja kuhitimisha hoja ambayo tuliileta Mezani leo mapema. Kwanza, nawashukuru Wabunge wote waliochangia. Nilikuwa nafuatilia michango, katika wachangiaji wote tangu tumeanza Kamati, Kamati yangu ya Maji na Mazingira ndiyo imepata wachangiaji wengi zaidi. Imepata jumla ya wachangiaji 15, inaonesha umuhimu wa Kamati hii ya Maji na Mazingira kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, mambo mengi yamezungumzwa. Kwanza nami nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupitishwa na Chama chetu cha Mapinduzi kuwa Mgombea wa Urais. Pia, mwenza wake Dkt. Nchimbi na Makamu Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Wasira pamoja na Mheshimiwa Mwinyi pale Zanzibar kwa kuwa Rais kwa kupitia CCM katika eneo lile la Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, pia, nawashukuru Mawaziri wangu wawili, kwanza kwa kukubaliana na hoja za Kamati. Kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Masauni, amekuwa mgeni, ana wiki chache, lakini amekubaliana na mambo yote na ameielewa Kamati inataka nini kwa muda mfupi sana. Mheshimiwa Dkt. Masauni nakushukuru kwa kuielewa Kamati na kujua inataka nini kwa maslahi mapana zaidi ya nchi yetu ya Tanzania na mustakabali mzima wa mazingira yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna Mawaziri wawili ambao ni wasikivu sana, wenye heshima, wanyenyekevu na watii kwa Kamati. Huwa tunasigana, lakini mwisho tunaelewana na mambo yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, sasa nakuja kwenye hoja. Yamezungumzwa mambo mengi, lakini kwa sababu ya muda ambao tumepewa, nitakwenda kuyafupisha. Kikubwa ambacho kimezungumziwa ni ulipaji madeni kwenye miradi yetu ambayo inaendelea nchini. Wizara ya Maji inatekeleza miradi ipatayo 1,342. Kwa kipindi cha miaka miwili imetekeleza miradi hiyo. Ni miradi mingi, ukiijumlisha kwa pamoja, fedha zake zinafika shilingi trilioni na zaidi.
Mheshimiwa Spika kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba, ni kazi kubwa ambayo inafanywa na Wizara ya Maji. Sasa, kwa miradi hii yote ni ngumu wakati mwingine kuwa na resources za kutosha kuweza kulipa madeni katika miradi hii yote.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, RUWASA peke yake kuna miradi 1,095 ambapo miradi 247 imekamilika. Kwenye miji miradi 218 na 68 imekamilika, ni miradi mingi, kwa hiyo, inahitaji fedha nyingi. Sasa, kwenye eneo hilo tunachoiomba Serikali kwa kweli, pamoja na nia nzuri ya kuendelea kuwapatia maji wananchi ni vema ikaona umuhimu na tunamwomba Waziri wetu wa Fedha, kama alivyoaminiwa na Mheshimiwa Rais kuitafutia Serikali fedha, basi hata hili eneo la maji huko tunakokwenda atutafutie fedha, ili angalau tukwamue miradi kadhaa ambayo bado haijaweza kulipiwa.
Mheshimiwa Spika, tumezungumzia suala la NEMC kuwa mamlaka. Siyo tamaa ya Kamati, hapana. Tumejaribu kuangalia kwa mapana yake namna mazingira yanavyosimamiwa, na pia tumeangalia hata wenzetu wa nchi za jirani wanaotuzunguka, hata Zanzibar hapo.
Mheshimiwa Spika, vilevile hata matakwa, wakati mwingine ya wale ambao tunashirikiana nao, hawa ambao pengine tunawaita wafadhili, wanatamani sana kuona tuna taasisi imara zenye nguvu na wanapenda zaidi wakati mwingine kufanya kazi moja kwa moja na hizi taasisi kuliko Wizara.
Mheshimiwa Spika, tumeiona hiyo mara nyingi, kwa hiyo, tulitamani sana tuwe na hii taasisi ambayo ni imara, ambayo pia inaweza ku-access fedha ambazo ziko huko duniani na zipo zinatakiwa.
Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwenye kituo cha usimamizi wa biashara ya carbon, nacho kinatakiwa kitungiwe sheria. Kikiwa na sheria ni rahisi hata wale wanaokuja kuona, ni taasisi ambayo inaeleweka na kutambulika na Serikali. Pia, kwenye eneo la Uchumi wa Buluu, ni eneo kubwa ambalo Serikali inaweza kupata fedha nyingi.
Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengi yanaweza kufanyika. Kuna madini kwenye bahari kule, kuna mazao ya mwani na mengine yote na pia, kuna uvuvi kwenye bahari kuu. Kule nako tukiwa na chombo imara ambacho kinaweza kusimamia, nchi hii tutakuwa na vyanzo vingi za kuweza kupata fedha za kukwamua shughuli zetu nyingi za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, pia, tumezungumzia masuala mengine ambayo wenzangu hapa wameyasema kwenye upande wa mazingira. Tumezungumzia kushirikiana katika kupanga miji. Kwa mfano, unakuta miji inafanyiwa mpango, lakini hawaweki mpango wa kuhakikisha mabomba ya majisafi na majitaka yanapita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukasema kwamba, ni vizuri sasa, wakati tunaweka mipango miji, wenzetu waweze kushirikiana na Wizara ya Maji, TAMISEMI na watu wa mipango miji waende pamoja, ili tusiwe na sababu wakati mwingine ya kuendelea kuharibu mipango miji na miundombinu ambayo tayari imeshawekwa. Kwa hiyo, tukasema jambo la ushirikiano ni muhimu.
Mheshimiwa Spika, yapo mengi yamezungumzwa, lakini naunga mkono hoja zote ambazo zimetolewa na wenzangu, ziko nyingi. Kwa kuwa, wenzetu katika Serikali wamesema wamepokea, basi waende wakayafanyie kazi, ili tuwapatie Watanzania mazingira mazuri na pia tuwape maji kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache naomba kutoa hoja, ahsante sana. (Makofi)