Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa (National competitiveness).
Mheshimiwa Mwenyeiti, bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026. Katika kipindi chake akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kusababisha Taifa letu la Tanzania linafanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapitio ya kipindi cha bajeti 2024/2025, Serikali kupitia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya utumishi na hasa kurudisha uwabikaji kazini na kuleta ufanisi mkubwa hasa kwenye utekelezaji wa miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbeya Vijijini limenufaika kupitia miradi ya TASAF ambapo imebadilisha maisha ya wananchi katika vijiji husika. Pia kwa kusimamia vizuri rushwa na upendeleo umepungua kwa kiasi kikubwa na kuleta ufanisi mkubwa sehemu za kazi na hata miradi kukamilika kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa, napendekeza kuendeleza mafunzo ili kuboresha weledi wa watumishi ikiwemo upanuzi wa Chuo cha Watumishi Mbeya na eneo muafaka kwa ujenzi wa chuo kipya na cha kisasa ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambapo kuna maeneo mazuri ikiwemo yaliyokuwa mashamba ya Tanganyika Packers Mbalizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mahitaji makubwa ya elimu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa ngazi mbalimbali. Napendekeza Serikali irudishe utaratibu wa mafunzo maalumu ya viongozi kwa kushirikiana na vyuo vikuu ikiwemo Mzumbe, UDSM, IFM na hata nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo yanayohitajika ni kama vile Executive Development Pragrammes kwa viongozi kulingana na ngazi zao. Mafunzo nje ya nchi ni muhimu kwa kuleta ujuzi kutoka nje hasa nchi zilizoendelea na hata zile zinazoendelea na zinazofanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta mbalimbali, napendekeza Serikali iendelee kutoa ajira zaidi hasa kwenye maeneo ya kuchochea uchumi na pia sekta ya afya, elimu na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na idadi kubwa ya wahitimu kukosa ajira na wametapakaa kila kona ya Tanzania hasa vijijini, napendekeza Serikali kuhakikisha ajira zinatolewa kwa usawa wa maeneo yote ya Tanzania kulingana na sifa. Serikali iangalie kuboresha sera za kikodi ili zichochee kuongeza ajira pamoja na kukuza uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majukumu na unyeti wa mashirika ya kadhaa ya umma ikiwemo ushindani wa kupata watalaamu wazuri, mashirika haya yaruhusiwe moja kwa moja kutoa ajira ili yaendane na mahitaji yao na Tume ya Ajira wawe na jukumu la ushauri na udhibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi kama CAG kisheria anatakiwa awe huru ikiwemo uhuru wa kuajiri; na hata taasisi kama mabenki, TANESCO, Bandari, TRA ni muhimu wakapewa uhuru wa kuajiri kulingana sifa ili kupata watalaamu wazuri kiushindani na pia kulingana na bajeti za mashirika husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maboresho ya mfumo wa TASAF, napendekeza pia kuboresha zaidi mfumo huo ikiwemo msukumo wa miradi, ilenge maeneo yatakayochochea uzalishaji wa mali ili zisaidie jamii kwa upana mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maeneo ya uzalishaji, msukumo ujumuishe kuimarisha masoko ya bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo ya mradi. Miradi ilenge kuboresha elimu na hata kusomesha watoto wanaotoka kwenye kaya maskini ya maeneo husika. Serikali iboreshe taratibu za kupata maeneo ya miradi ya TASAF ili kupunguza malalamiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.