Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia machache juu ya Mpango huu wa Serikali ambao umeletwa mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Silinde kusema kwamba tunayo maneno mengi na mipango mingi lakini utekelezaji ndio umekuwa tatizo kubwa sana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye gharama za uendeshaji wa miradi katika nchi yetu. Kwa muda karibu wa miaka miwili ndani ya Bunge hili tumekuwa tukiishauri Serikali kufanya marekebisho katika Sheria ya Manunuzi. Ukitazama tangu Naibu Waziri wa Fedha alipotusomea hapa mwelekeo lakini katika vitabu vyote hivi ambavyo vimeletwa na Waziri malalamiko yao na maoni yao yamegusa namna ya kudhibiti manunuzi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya tatizo kubwa ni Serikali kushindwa kuleta sheria hii ili tuirekebishe. Tumelalamika sana, Wabunge wamepiga kelele kuhusu namna sheria inavyosababisha ukiritimba na kuifanya Serikali miradi yake kuwa ya bei kubwa, miradi mingi inashindwa kukamilika na inayokamilika inakuwa na gharama ambazo zimeifanya Serikali iwe na madeni makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize ni lini sasa Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Manunuzi? Wakati mwingine nakuwa na wasiwasi kwamba mnashindwa kuleta sheria hii kwa sababu wako watu ndani ya Serikali ambao wananufaika na matumizi ya sheria hiyo. Mmeongelea suala la kudhibiti mtadhibitije kama sheria bado ni ileile. Kwa sababu sasa imekuwa ni kawaida ya Serikali manunuzi yake hayaendani na soko. Kalamu ambayo inauzwa kwa shilingi 200/= wao watainunua kwa shilingi 1000/=. Mradi wa Serikali ambao ungeweza kutekelezwa kwa shilingi 50,000,000/= unatekelezwa kwa shilingi 100,000,000/=. Naiomba Serikali ibadili sheria hii na iilete haraka sana ili tuweze kuifanyia marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu elimu. Yako mambo mengi na Waziri wa Elimu ametuambia kwamba atakuja na mipango hasa ya upande wa ukaguzi, lakini mimi naomba niongelee kuhusu mgawanyo sawia wa walimu katika nchi yetu. Unaweza kukuta kuna shule ambazo zina walimu 30 na shule nyingine zina walimu wawili.
Naomba nitolee mfano katika Jimbo la Bukoba Vijijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba. Halmashauri hii katika Mkoa wetu imekuwa ya mwisho kielimu, lakini hata shule ambayo imekuwa ya mwisho kiwilaya na kielimu inatoka katika Halmashauri hii inaitwa Kamkole ipo katika Kata ya Rukoma, ina wanafunzi 215 ina walimu wawili tu. Mwaka jana Halmashauri ya Wilaya iliomba walimu 280, haikupata mwalimu hata mmoja. Mwaka huu tunakwenda kuomba walimu 300, tunaomba Wizara ifikirie namna ya kupeleka walimu katika Halmashauri hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnakumbuka siku za nyuma yuko Mkuu wa Wilaya ambaye amewahi kupiga baadhi ya walimu viboko 20 lakini tatizo hakuna walimu katika Halmashauri hii, wanapoomba walimu hamuwapi, shule ina walimu wawili au watatu. Kama Waziri wa Afya alivyotuambia kwamba anakwenda kufanya sensa ya kuona kwamba madaktari wanakwenda sawia hata katika mikoa ya pembezoni, tunaomba walimu nao wagawiwe kwa usawa siyo shule moja inakuwa na walimu 300 na hasa shule za mijini. Pamoja na kwamba tunatetea wanawake lakini na wanaume nao wawe wanaomba uhamisho kufuata wake zao ili waende katika shule hizo isiwe kila siku sisi wanawake ndiyo tunawafuata wanaume ifike mahali na ninyi mtufuate huko tuliko. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maoni yangu kuhusu hii retention. Kamati ya Bajeti imekubaliana na mapendekezo ya Serikali. Inawezekana Serikali ina jambo ililoliona labda kuna matumizi mabaya ya fedha hizo lakini naomba niwakumbushe. Mwaka 1972 wakati Serikali imefuta Local Government ikaleta utaratibu wa madaraka mikoani, baada ya miaka kumi Serikali ilishtuka kwamba imeondoa huduma kwa wananchi na ikarudisha Local Government. Hata hivyo, baada ya kurudisha Local Government, Serikali imekwenda kufuta vyanzo vya mapato ambavyo vilikuwa vinasaidia halmashauri hizi kuweza kujiendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kilichopita mimi nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI, katika kupitisha bajeti, Wakuu wa Mikoa wote wamelia jinsi Serikali inavyoshindwa kurudisha ruzuku ya vyanzo hivi. Ukipitia bajeti ya mwaka jana, karibu mikoa yote Serikali ilishindwa kupeleka fedha mpaka wengine walipata asilimia 28 – 30, hii imesababishwa na Serikali Kuu kubeba pesa zote. Mimi nina wasiwasi na naungana na wale wanaosema Serikali inakwenda kuuwa mashirika haya. Serikali kwanza ituambie imeona mpaka ikaondoa retention? Hata ndani ya Halmashauri, kwa mfano, Idara ya Ardhi, vyanzo vyote vya mapato vinakwenda Wizarani lakini Wizara ya Ardhi imeshindwa kurudisha pesa hizo na unakuta halmashauri zinashindwa kupima viwanja kwa sababu hawana fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii retention ina maana gani? Ina maana kwamba pesa yote itakusanywa Hazina na tujue hii Serikali ina wakora, kuna watu wengine ni wakora huko, wanaweza kutumia mwanya huu kuhakikisha kwamba hizi fedha hazirudishwi inavyotakiwa. Serikali itueleze, ina mpango upi sasa ambao utawezesha fedha hizi kutoka Makao Makuu Hazina kuzirudisha katika wilaya ikiwa ni pamoja na Halmashauri. Halmashauri zinalia na mmekwenda kuziua na zinakwenda kufa. Serikali ifikirie namna ya kurudisha baadhi ya vyanzo. Kama inashindwa kupeleka fedha za bajeti irudishe vyanzo vile ambavyo vilikuwa vinawezesha Halmashauri kuweza kupata mapato yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya chama chetu cha CHADEMA ya 2010 tulikuwa tumepanga kurudisha Serikali za Majimbo, CCM ikapiga kelele na kusema ni ukabila siyo ukabila, hii nchi ni kubwa. Ndiyo maana watu wanaiba mpaka CAG atambue wizi umetokea mahali fulani inakuwa imepita miaka mitano. Nchi hii ni kubwa, inahitaji chombo kingine hapa katikati ambacho kitahakikisha wananchi wanapata huduma zao na kudhibiti mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele ya kwanza imeshalia, naomba niongelee juu ya utawala bora. Nitaongelea Wilaya ya Kyerwa, mimi ni Mbunge wa Viti Maalum naruhusiwa kuongelea mkoa mzima. Utawala bora ni pamoja na mambo ambayo mmeona yanafanyika katika uchaguzi. Mtu anashinda kiti chake lakini anatangazwa ambaye hakushinda. Wasimamizi wa Uchaguzi ni Wakurugenzi, Mkurugenzi anatangaza matokeo halafu anapitia dirishani. Tume na ninyi mnafanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachotaka kuwaambia haya mambo yanaweza kuwa ni kung‟ang‟ania kupata madaraka sawa lakini mnalea kizazi ambacho hakiwezi kuvumilia mambo haya. Kizazi cha sasa hivi hakina siasa za mwaka 1947, tunao watoto na vijana wapya. (Makofi)
MHE. CHONCHESTA L. RWAMLAZA: Msifikirie kung‟ang‟ania madaraka ni jambo jema. Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa CHADEMA ilipata Madiwani 13 wakati CCM ilipata…
MWENYEKITI: Ahsante, kwaheri.
MHE. CONCHESTA L. LWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)