Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi na Naibu wake, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa majukumu makubwa waliyonayo na utendaji wao mzuri ambao wameanza katika kipindi hiki cha uteuzi wa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Mafuguli. Nawapongezeni sana kwa kazi nzuri pamoja na changamoto kubwa ambazo mnakabiliana nazo za migogoro ya ardhi iliyopo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Kamati yetu imesema, Serikali imekuwa haitoi fedha zilizoombwa katika bajeti ambayo ilikuwa imetengwa ya Wizara ya Ardhi. Kutotoa fedha kwa wakati na kutotoa fedha zote, kumechangia Wizara hii kutotekeleza majukumu yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kwamba Wizara hii ina majukumu makubwa, imebeba mambo makubwa yanayohusiana na wananchi juu ya migogoro ya ardhi. Kwa hiyo, kutowapa fedha, kutopeleka fedha kwa wakati na kutopeleka fedha zote kunachangia kutotekeleza majukumu yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwamba katika bajeti itakayokuwa imetengwa safari hii, wapewe fedha zao zote na kwa wakati ili waweze kutimiza majukumu yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuonyesha masikitiko yangu ambayo yamefanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuchelewesha mchakato wa maamuzi ya usimikaji wa Mfumo wa Utunzaji wa Kumbukumbu. Ucheleweshaji huu umekuwa ni wa miaka miwili na nusu. Tulipokuwa kwenye Kamati, tuliwaita Ofisi ya Waziri Mkuu tukataka watuambie, ni kwa nini wamechelewesha tender kwa ajili ya usimikaji wa mfumo huu wa kumbukumbu za ardhi? Majibu yaliyotolewa pale, yalikuwa ni ya ubabaishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Ofisi ya Waziri Mkuu ifanye haraka suala la mchakato, ikamilishe mchakato huu haraka ili kusudi suala hili la usimikaji uweze kufanya kazi mapema ili kusudi matatizo yaliyopo ya ardhi yaweze kutatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni. Naungana na maoni ya Kamati yetu kwamba wenzetu waliopo pale katika ofisi ile ya uendelezaji wa mji wa Kigamboni hawana kazi ya kufanya. Hata ukiangalia kwenye bajeti safari hii hawana fedha za maendeleo. Hata kipindi kilichopita, hawakuwa na fedha za maendeleo. Watu hawa wanapewa bajeti ya mishahara tu. Kwa hiyo, wanalipwa mishahara pasipo kazi. Hakuna haja ya kuendelea kuwepo na ofisi kule Kigamboni ya uendelezaji wa eneo lile wakati watu hawafanyi kazi. Ni vizuri watu hawa wakarejeshwa basi kwenye maeneo mengine wakaendelea kufanya kazi zao. Walipwe mshahara wakifanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamepanga jengo kubwa lenye gharama kubwa, wanakwenda wanasaini, wanatoka zao. Hata Biblia imesema asiyefanya kazi na asile. Iweje hawa wenzetu wanakuwepo katika kipindi cha miaka nane hakuna kazi inayofanyika pale na wala hakuna fungu la maendeleo! Tulipokuwa tunauliza, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alikuwa anawatetea kidogo, anasema waacheni tu, tutaangalia, tutatafuta fedha; utatafuta wapi wakati humu ndani ya bajeti hii ya maendeleo haipo? Fedha za kutafuta kuokoteza, zinatafutwa wapi? Ni vizuri watu hawa wakasambazwa kwenye maeneo mengine kwa sababu Wizara hii ina upungufu wa watumishi katika maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iweke utaratibu sasa wa kuweka mabaraza ya ardhi kwa kila Wilaya. Ipo shida, pale kwangu Korogwe kuna Baraza la Ardhi, ni kero kubwa. Kesi za mabaraza ya ardhi haziishi, zimesongamana, ni nyingi. Baraza la Korogwe pale, linachukua Handeni, Kilindi, Lushoto na Korogwe yenyewe. Kuweka mlundikano wa kesi nyingi katika baraza lile, kunasababisha rushwa kubwa. Wananchi wanalalamika. Naiomba sana Wizara, ihakikishe kwamba kunafunguliwa mabaraza mengine, ikiwezekana kule Kilindi na Handeni wawe na baraza lao, Korogwe wawe na baraza lao na Lushoto wawe na baraza lao ili kuondoa usumbufu ambao wanaupata wananchi kuja kutoka Handeni kuja Korogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu mashamba makubwa ya wawekezaji. Naomba hawa wawekezaji ambao wanapewa maeneo kwenye vijiji, basi waone umuhimu wa kuchangia masuala ya maendeleo kwa wananchi wa vijiji vile ambavyo wanaishi. Hiyo itajenga mahusiano mazuri na wanavijiji. Kutowasaidia kufanya hivyo, ndiyo unasikia migogoro mingine kwenye maeneo hayo, wawekezaji mara wanafukuzwa na wanavijiji, mara wanaingiliwa kuchomewa mali zao. Ni vizuri wakajenga mahusiano mzuri na wana vijiji ili kusudi wakiwasaidia kwa mfano miradi ya maji, ujenzi wa shule na mambo mengine mengi, hakutakuwa na matatizo na kero ambazo zinatokea sasa hivi kwa wawekezaji na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Wizara ianze kuangalia namna ya kuwapa wawekezaji maeneo. Tuangalie maeneo ambayo yako wazi, tusiende kuwapa wawekezaji maeneo ambayo ni mashamba wa wananchi na makazi ya wananchi ili kuondokana na migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali yangu sasa waanze kuona umuhimu wa kuanza kuwapatia wawekezaji maeneo ambayo sio makazi ya wananchi na siyo mashamba ya wananchi ili kuondoa migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana.