Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Nianze kwa kuunga mkono hoja na nimpongeze Mwenyekiti wetu kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupitishwa na Mkutano Maalum kuwa mgombea pekee wa Chama Cha Mapinduzi, na Dkt. Nchimbi kuwa mgombea mwenza. Nawapongeza sana, na sisi Kakonko wametutendea makubwa, tunasubiri tu tarehe maalum tuweze kulipa deni letu kwa kumpigia kura za ‘Ndiyo’ Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mambo ni mengi, nitachangia mambo machache na eneo ambalo nitachangia sana ni ajira ya walimu. Naipongeza sana Serikali kwamba imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa madarasa, ujenzi wa nyumba za walimu na kadhalika, lakini haijafanya kazi kubwa ya kuajiri walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa madarasa, uwepo wa nyumba za walimu, kwa hoja yangu ni mapambo. Kwangu mimi ninachoona ni muhimu kwa ajili ya utoaji wa elimu ni upatikanaji wa walimu. Napongeza sana kwamba kuna juhudi zinafanyika na usaili unafanyika, lakini usaili huu unafanyika kwa walimu waliomaliza mafunzo ya ualimu karibu miaka 10 iliyopita, lakini unafanyika sambamba na Mwalimu mwingine aliyemaliza masomo yake mwaka 2024 (mwaka jana), hii siyo sawa. Kwa hiyo, ninachoshauri, Serikali iajiri walimu. Narudia kusema, Serikali iajiri walimu. Nirudie tena nasema kwamba, Serikali iajiri walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni ukweli kwamba walimu hasa katika shule za msingi hali siyo njema. Nawapongeza walimu kwamba unakuta wakati mwingine wapo walimu kwa 50% lakini wanafaulisha kwa 80%. Maana yake ni kwamba hawa walimu ambao ni wachache, wamelazimika kufanya kazi ya ziada ya walimu ambao hawapo. Nawapongeza sana walimu wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usaili unafanyika na tuliwashawishi walimu kwamba someni sisi tutawaajiri, na bado tukawapelekea fedha za mikopo lakini sasa wana miaka 10 nyumbani, naiomba sana Serikali sasa ifanye kazi ya ziada, iwaajiri hao walimu hasa wale ambao walianza masomo na wakamaliza mafunzo siku nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katikati nadhani ilikuwa mwaka 2024, Wabunge walishauri kwamba kwa kuwa walimu wengi wapo mitaani, ni vizuri tuanze na wale walimu walioanza siku za nyuma. Hii itapendeza kwamba wale walioanza wa awali wawe wa kwanza kuajiriwa. Tunao walimu wa mwaka 2015, 2016, na 2017. Kwa nini wasianzwe hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia hata sisi Wabunge kuwa na majibu sahihi kwa wananchi wetu. Muda mwingine unaombwa Mbunge, usaidie kupata ajira, lakini muda mwingine huna jibu sahihi. Tungekuwa na uhakika kwamba waliomaliza labda 2015 au 2016 watakuwa wa kwanza kuajiriwa, hii itatusaidia hata katika majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nirudie kushauri kwamba tuanzie kule kwa wale walimu walioanza 2015 au 2016. Pale tutakapoishia ajira nyingine ikiingia tutaanzia pale ambapo tuliishia kuendelea mbele. Kutokuwaajiri walimu hawa wakati huo wana mkopo, lini sasa fedha hizi za Serikali zitarudi? Maana yake kama walimu tumewapa mkopo, hawajaajiriwa, uwezekano hata wa kupata mkopo maana yake hizo fedha ambazo tuliwapa siyo rahisi kuzipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana walimu hao ambao walianza mapema waajiriwe na fedha ambayo Serikali iliwakopesha iweze kurudishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kwenye eneo la kuwarudisha vijana ambao waliacha shule za sekondari kwa sababu mbalimbali. Wapo watoto wa kike ambao waliacha shule kwa sababu ya ujauzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa nafasi tena kwa vijana hawa, lakini shida iliyopo kwangu, naona kwamba ni shida kwa sababu wameangalia tu watoto wa kike, lakini hawaangalii watoto wa kiume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa kiume kuna uwezekano mkubwa wakawa na changamoto nyingi. Hawa ndio wanaofanya biashara stendi, hawa ndio wanakwenda kwenye uvuvi, hawa ndio wanaokwenda kwenye kuchunga ng’ombe lakini hawajapewa nafasi sambamba na watoto wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, nafasi inayotolewa kwa watoto wa kike itolewe vilevile kwa vijana wetu wa kiume. Hawa watoto wa kike ambao tayari wana Watoto, unamrudisha shuleni, alikuwa peke yake, sasa ana mtoto, akienda shule huyu mtoto anamwachia nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwe na uangalizi wa ziada kuona kwamba ni kwa kiasi gani tutamsaidia huyu binti ambaye ana mtoto, lakini anarudi shuleni. Hiyo iende sambamba na kuwatafuta waalimu maalum wa kuja kuwasaidia hawa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa vijana wetu walikuwa na changamoto peke yao, sasa wana Watoto, kwa hiyo, inafaa kuwe na uwezekano wa kuwa na walimu maalum wenye saikolojia ya watu wazima, wanaojua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuweza kuwahudumia hawa watoto na vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa sababu ya muda, ahsante sana. (Makofi)