Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mada ambazo zipo Mezani. Nifanye mambo mawili; la kwanza, ni kupongeza Taarifa za Kamati zilizowekwa Mezani, na kwa niaba ya Wizara niseme tumepokea maelekezo na mapendekezo ambayo yamewekwa kwenye taarifa hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yaliyotolewa na Kamati kwa niaba ya Bunge Zima ambayo yameungwa mkono na Bunge Zima, ni maelekezo ambayo Serikali haina pingamizi nayo na hii ndiyo kazi ambayo tumeendelea nayo mara zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala hapajatokea ulegevu katika eneo lolote. Nilisema katika kipindi kilichopita na ninarejea tena kusema, kilichojitokeza ni kweli bajeti yetu imeathirika katika kipindi cha kuanzia mwaka 2024 na 2025. Kwa kuwa bajeti imeathirika, Serikali imekuwa ikipambana kuhakikisha kwamba, shughuli zote hazikwami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano michache, mwaka 2024 katika muda ambao Bunge litakumbuka, tulipitia muda ambao barabara zote za TARURA na TANROADS zikiwa zimeharibika. Hii iliathiri sana bajeti yetu na mtiririko wake wa kawaida. Kama vile hiyo haitoshi, tulipitia kipindi ambacho mgao wa umeme ulienda kutunyemelea katika hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge litakumbuka mgao wa umeme ulishashika kasi yake. Tulikuwa na njia mbili za kushughulikia jambo hilo, ambapo ilikuwa ama tutafute mitambo ya dharura ya kukodi au tuharakishe ukamilishaji wa bwawa la umeme. Ilifika wakati tulikuwa tunalipa certificate zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa mwezi kwenda kwenye mradi mmoja wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya aina hiyo siyo ndogo, na huwezi ukafanya hivyo bila kuathiri bajeti, maana yake kikapu ni kile kile. Tulikuwa tunagusa hapa, tunagusa hapa, ili tutekeleze lile badala ya kukodi mitambo. Jambo lile limefanyika kwa haraka na mradi ule umekamilika. Sasa sisi ndani ya Serikali tulijua inawezekana tukapoozesha mahali, lakini baada ya mradi ule kukamilika, tumepumua na ndiyo maana unaona sasa tunarejesha kasi ya utekelezaji wa shughuli hizo nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kule TARURA, fedha hizi ambazo tumezitoa hivi juzi, ni vile tu wakandarasi walikuwa site na walikuwa wanadai. Kwa hiyo, tumepeleka na zimekwenda kulipa madeni. Hivi sasa pia tunapeleka tena na hicho ndicho ambacho tunakubaliana na wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujakaa tu tukaacha, lakini tulisema kwenye hili ambalo tunaweza tukatatua kwa kukamilisha bwawa letu wenyewe, fahari ya Watanzania, tulisema tu tufunge mikanda, tutabanabana, kuna sehemu pata-slow, lakini tutakamilisha, na jambo hilo limekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, utakumbuka pia maelekezo ya Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema tumeshaumia sana katika kutekeleza Lot mbili za reli, twendeni tujibane kuhakikisha reli inaanza kufanya kazi. Hata hilo, tulijibanabana kuhakikisha linakamilika, na yenyewe imeshaanza kufanya kazi kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma. Hata hiyo, tulijibanabana na kufunga mkanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, pia tulikuwa tunakimbizana na Daraja la Kigongo – Busisi. Kazi ilikuwa inaendelea na ilishafanyika kwa kiasi kikubwa, ilikuwa inakaribia kumalizika lakini na kwenyewe tulisema tuikamilishe ili wale wananchi wasipate shida. Hivi tunavyoongea, Waziri wa sekta aliniarifu kwamba alitembelea pale, almost imeshakamilika. Nadhani inaweza ikazinduliwa muda wowote kuanzia sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimkakati, kuliko kugusagusa kaeneo haka na haka halafu utumie mitambo ya dharura, tuliona tufunge mikanda ili tuwe na miradi ambayo imekaribia kukamilika ili tuhesabu hii imekamilika na hilo Rais wetu amefanya na limekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia hata Mama yangu na rafiki yangu kipenzi sana Mheshimiwa Dkt. Ntara, akisema hata masuala ya VETA. Hata hili suala la VETA inawezekana Serikali kwa kuwa na matumaini na matarajio makubwa zaidi na yenyewe imetupa shida ya kuweza kuhakikisha kwamba labda speed ikawa ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya ni zile zile tangu Uhuru, zinaongezeka kidogo kidogo, lakini kama mpaka Serikali ya Awamu ya Sita imekuta kuna mikoa na wilaya zaidi ya 60 hazina VETA, na Serikali ikaamua kuzijenga zote kwa mpigo. Mimi ninadhani haipaswi kunyooshewa kidole, bali inatakiwa kutiwa nguvu na kupongezwa. Tumekwenda kuzibeba wilaya na mikoa yote iliyosalia kwa mpigo na fedha zinakwenda, siyo kwamba tumeacha tu hivi hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira ya sasa ya msukosuko wa kiuchumi duniani, kila jambo ni kipaumbele na kila jambo linahitaji fedha. Tumekwenda kubeba tarafa zote ambazo tangu Uhuru hazijawahi kuwa na vituo vya afya na baadhi ya kata ambazo zilikuwa zinahitaji vituo vya kimkakati, tumekwenda kuzibeba zote kwa mpigo. Kama hiyo haitoshi, tumekwenda kuweka kila jimbo lipate kituo cha kimkakati na fedha hiyo itatoka kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kikapu ni kile kile, unaweza ukaona kwamba Serikali ina nia ya dhati sana kuhakikisha inatekeleza masuala ambayo Watanzania wanahitaji, sambamba na Wabunge ambao ni wawakilishi makini wa wananchi wanavyoshauri humu ndani ya Serikali. Hatujafanya makusudi kwenye jambo lolote, na wala hatujalegalega kwenye jambo lolote. Tumeongeza kasi na nguvu na tunafanya kwa jitihada kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemshuhudia kwamba mama yetu ni mama jemedari sana. Kwa mazingira ya dunia inayopitia ya kiuchumi, kila mchumi angemwelewa kwamba, “ninaondoa hii miradi kwa sababu dunia inapita kwenye msukosuko.” Tena siyo Tanzania inapitia, ni dunia nzima inapita kwenye msukosuko. Fuatilieni nchi za jirani, nchi zote za SADC na EAC, fuatilieni na mnitajie nchi moja inayotekeleza miradi mingi na mikubwa ya kimkakati na yenye mtawanyo kama Tanzania inavyotekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye kujibu kwamba fedha zitatoka ama hazitatoka? Fedha zitatoka na hiyo ndiyo kazi niliyotumwa, na bado naipenda. Fedha zitatoka zinazokwenda kwenye vituo vya afya na vituo hivi vyote ambavyo Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameahidi kwenda kwenye kila jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia fedha ambazo zimetajwa kwenye sekta ya elimu, kwa upande wa miundombinu, maboma ya madarasa na mitaala mipya, zitatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshakamilisha taratibu, na keshokutwa kuna andiko ambalo tutalitoa, ambalo ninyi wenyewe mtatufungulia twende kutekeleza haya mambo ambayo mmeishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fedha za maeneo mengine ambazo zimeongelewa, na kwa ajili ya muda sitataja zote. Nikimaliza kikao hiki, na hata asubuhi nilikuwa na kikao na wenzetu ambao tunashirikiana nao DMDP na maeneo mengine, tumekuwa na vikao ambavyo tunakamilisha taratibu za kuweza kutoa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wajue nia ya dhati ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan haijabadilika, na tena anatekeleza kwa nguvu zaidi. Nia ya dhati ya Serikali ya CCM kuendelea kujitambulisha kupitia kutekeleza mambo ambayo yanawasaidia wananchi kupiga hatua katika shughuli za maendeleo, haijabadilika na inatekelezwa kwa nguvu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tutaendelea kutoa taarifa kwenye Kamati jinsi ambavyo tunatekeleza haya mapendekezo ambayo yametolewa na Bunge lako Tukufu. Yote tunakwenda kuyatekeleza na tunaongeza kasi zaidi kwa sababu tumeona jinsi ambavyo wawakilishi makini wa wananchi wa Tanzania, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi wanavyosimama kidete kuisimamia Serikali na kutetea maslahi ya wananchi ili kuweza kuhakikisha kwamba Tanzania inapiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko committed na hii kazi. CCM inaiweza, Mheshimiwa Dkt. Samia anaiweza na sisi wasaidizi wake tutakuwa naye bega kwa bega ili kuweza kuhakikisha kwamba hakuna jambo ambalo linarudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)