Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika bajeti hii ya Wizara ya Fedha na mimi nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa hii na neema ya uhai, lakini kipekee niseme moja kwa moja naunga mkono hoja ya bajeti hii ya Wizara ya Fedha na kwa kuwa mimi ni sehemu ya Kamati ya Bajeti naunga mkono Taarifa yetu na mapendekezo yetu ya kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri - Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri - Mheshimiwa Chande, Katibu Mkuu - Dkt. Natu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wote wa taasisi chini ya Wizara hii ya Fedha, wakuu wote wa vitengo na watumishi wote wa Wizara ya Fedha kwa namna ambavyo wamefanya kazi yao nzuri katika kipindi chote sisi tulipokuwa tunahudumu Kamati ya Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ulitupa kazi kwenye Kamati hii wametupa ushirikiano wa kutosha, Serikali imekuwa sikivu, mapendekezo yetu yote wamekuwa wakiyatekeleza ninasimama hapa nikiwa nafahari kubwa kwamba kwa kweli kwa kipindi cha miaka mitano Wizara hii imetekeleza wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jumamosi iliyopita kama Bunge tumefanya tukio kubwa la kutoa Tuzo ya Heshima kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imetokana na kazi nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita, lakini kwa kadri ambavyo uliwasilisha taarifa ile na sababu zilizopelekea Bunge kutoa tuzo ile ni utekelezaji wa miradi ya kisekta ya kimkakati na ya huduma za jamii, lakini kazi ile imetokana na uratibu wa Wizara hii ya Fedha ya kutekeleza majukumu yao ya utafutaji wa vyanzo vya fedha vya ukusanyaji na ugawaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kupitia kazi nzuri waliyofanya hususani ya utafutaji na ukusanyaji, nasimama hapa nianze kwa kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kipindi chote cha miaka hii mitano tumeona kila mwaka kulikuwa na ongezeko la makusanyo ya mapato, lakini kipekee kwa miezi hii tisa ambayo taarifa rasmi iliwasilishwa niipongeze mamlaka hii kwa kuweka rekodi kwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kila mwezi kwa kipindi chote cha miezi tisa mpaka saa hivi na miezi 11 ambayo imewezesha kuifanya Serikali yetu ya Awamu ya Sita kuvuka malengo kwa zaidi ya 78% kulinganisha na mwaka 2020/2021. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapoipongeza Mamlaka hii ya Mapato chini ya uongozi wa Kamishna Yusuph Mwenda, makamishna wote, lakini na watumishi wote wa TRA kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuongeza ukusanyaji wa mapato lakini napongeza jitihada zao za ubunifu, napongeza jitihada zao za kuwahudumia wafanyabiashara, napongeza jitihada zao za kuweka mazingira wezeshi, lakini kipekee pia hata ziara za Kamishna Mkuu ambazo kweli tumeona kwa mara ya kwanza kupitia mikoa yote ya Tanzania, kuwasikiliza wafanyabishara. Sisi Kamati ya Bajeti tuna matumaini Finance Bill ijayo itakuwa nyepesi zaidi kwa sababu mwenyewe Kamishna amesikiliza wafanyabiashara, lakini kupitia think tank ya Wizara ya Fedha tunaamini kabisa itakuwa ni Finance Bill ya 4Rs - maridhiano, utahimilivu, itazingatia maboresho, itazingatia na vyanzo vipya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jambo hili ni endelevu na tunazungumzia bajeti ya mwaka 2025/2026 napenda niishauri Wizara ya Fedha kwa namna ya kuongeza mapato zaidi kwa kuwa sisi tulitembelea Bandari ya Dar es Salaam tumeona namna gani maono ya Mheshimiwa Rais ya kukaribisha sekta binafsi pale kupitia kampuni ya DP World na ada zilivyoongeza mapato kupitia mamlaka hii. Sasa nilikuwa napendekeza TRA iendelee kuzitazama hata bandari hizi ndogo ndogo zile zingine zirasimishwe kupitia ushirikiano na Serikali bandari bubu kwa mfano hapa ninaposimama sisi Mkoa wa Pwani tuna Bandari ya Kisiju, tuna Bandari ya Nyamisati, lakini tuna Bandari ya Bagamoyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye Bandari ya Bagamoyo pale nataka nimshukuru na kumpongeza meneja wetu mpya wa Wilaya - Bwana Baraka lakini nataka niseme pana malalamiko naiomba TRA ikae na wadau pale kuhusu tozo au kodi ya kuingiza madumu ya mafuta katika Bandari ya Bagamoyo kwa kiwango ambacho kiliwekwa pale ni shilingi 10,000 lakini maeneo mengine Bandari ya Mbweni, Bandari ya Kunduchi, Bandari ya Pangani inaonekana kama kiwango ni bei shilingi 8000 mpaka shilingi 7000. Kwa hiyo inaonesha Bandari yetu ya Bagamoyo inakuwa si shindani na hivyo kupungua kwa mizigo inayoingia kwenye Bandari ya Bagamoyo ambayo inasababisha pia kupungua hata mzunguko wa fedha kwenye bandari yetu pale na Mji wa Bagamoyo, lakini hata kwa wafanyabiashara wa eneo la Bagamoyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe Kamishna Mkuu ajaribu kuangalia na kuja atutembelee Bagamoyo na kukaa na wafanyabiashara na kusikiliza ili kuweza kupata mfumo mpya wa utozaji kodi katika biashara hii ya mafuta, lakini tuiombe pia Serikali iendelee kurasimisha biashara zingine kuingia kwenye Bandari yetu ya Bagamoyo kwa sababu ni bandari ya kimkakati kwa sasa na tunafurahi kwamba ilani inayokuja Serikali imepanga kujenga Bandari mpya ya Bagamoyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tunapendekeza pia uboreshaji wa miundombinu pale kwenye Bandari ya Bagamoyo Ofisi ya TRA kulikuwa na Jengo la Customs zamani lina miaka zaidi ya 100 ni jengo la urithi wa dunia, lakini tunatamani sasa TRA iangalie inaweza kuboresha vipi miundombinu ya pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee pia niimpongeze Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali; CAG Ndugu Kichere, ofisi yangu ya zamani kwa kazi nzuri waliyoifanya na namna pia Serikali ilivyoiwezesha ofisi hii maana yake ninapozungumza hapa zaidi ya 90% ya bajeti yao wameshapewa, kwa hiyo ni wazi kwamba kazi nzuri ya CAG imetokana uwezeshaji huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilishauri Serikali, Mheshimiwa Waziri kwenye Kamati kupitia hizi TRAT na TRAB tulikushauri kwa namna ambavyo mashauri ya kesi yapo kwenye mamlaka hizi walau ulitekeleza mwaka wa fedha wa mwaka jana umefanya uteuzi na nisimame hapa kupongeza TRA na TRAB na Mahakama ya Rufaa walau kwa kupunguza kidogo kwa sababu mwaka wa fedha 2023 tuliona kwamba mashauri yalikuwa zaidi shilingi trilioni 10. Ni mashauri siyo kama fedha inaibiwa ni mashauri shilingi trilioni 10.49 lakini kwa mwaka wa fedha huu 2024 kwa mujibu wa taarifa ya CAG mashauri sasa yamefika shilingi trilioni 9.8 lakini bado CAG amependekeza Serikali iziwezeshe hizi mamlaka kwa fedha, kwa rasilimali watu ili wasikilize mashauri haya kwa haraka na hii kodi inayobishaniwa iweze kukusanywa na kuleta tija na kuweza kufanya kazi ambayo imekusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru na wewe binafsi kwa kutupa heshima ya kuwa Wajumbe wa Kamati hii ya Bajeti, kwa maelekezo yako ya mara kwa mara, kwa namna ambavyo tumeweza kuisimamia Serikali ambapo leo tunajivunia pengine mwaka huu wa fedha tutaona rekodi mpya kwamba Serikali imevuka lengo iliyojiwekea ya kukusanya mapato yote na kwa kuweka rekodi ya mwezi Desemba shilingi trilioni 3.5 makusanyo ya juu kabisa tangu mamlaka hii imeanzishwa mwaka 1996. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kupongeza pia Serikali kwa kusikiliza kilio cha wastaafu wa nchi hii kwa kuja na mifumo ya uboreshaji wa uhakiki, lakini pia kuanza mchakato wa kuhuisha viwango vya malipo ya wafanyakazi wastaafu wanaolipwa kupitia Hazina. Huu ndiyo usikivu wa Serikali yetu, mmesikiliza mengi ya ushauri, mmeimarisha Kitengo cha Internal Auditor katika Serikali na ulikuwa ushauri wa Kamati yetu, mmeanzisha mamlaka ya Tax Ombudsman ya kusikiliza walipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kunipa heshima ya kuwa balozi wa kodi binafsi na kwa kuitumikia nafasi hii kwa Bunge hili kwa kuendelea kuhamasisha wananchi wadai risiti na wafanyabiashara waendelee kutoa risiti, lakini kipekee kwa kutuwezesha kuona namna kodi inayokusanywa matumizi yake tumepata kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati na ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nina furahi kwamba nimepata fursa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali hii kutembelea miradi mingi sana katika awamu hii kuliko awamu yoyoye ambayo nimepata kuhudumu kwenye Ubunge huu wa Viti Maalum na niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Pwani kwa fursa hii waliyonipa ya kuwa Mbunge wao wa Viti Maalum kwa vipindi kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii naunga mkono hoja na kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiweka nchi yetu kwenye ramani ya maendeleo, ahsante sana. (Makofi)