Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru na Mwenyezi Mungu nimshukuru zaidi kwa kutujalia kupata afya njema na kutuwezesha kuwepo hapa.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa sana ya kuhakikisha nchi inakwenda katika utulivu na amani na kutulia kwake na uvumilivu na ukimya ambao ameamua, basi hili ni jibu tosha kuwa yeye anapenda amani ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitazungumzia njia kuu za mapato ambazo inabidi zisimamiwe na Wizara. Tunahitaji mapato zaidi, sasa hivi Tanzania tujifunze kwa wenzetu baadhi wanaofanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi, hatutaki tena kuchukua mahela kutoka nje ambayo inakuwa kama ni kukopakopa nako kama ni masimango, lakini Mwenyezi Mungu kutokana na trend wanayokwenda nayo ya kiuchumi, nasema Mwenyezi Mungu azidi kuwabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nchi hii tuna maeneo manne ambayo tunabidi tuyasimamie, katika kilimo tunaingiza fedha za kigeni hasa katika mazao kama ya korosho. Korosho tunaita ni green gold lazima yapewe kipaumbele ili tuzidi kuzalisha na kupata mapato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uchukuzi hizi bandari zetu zinatuletea pesa za kigeni kwa meli zinazoingia na kwa kweli hali ya kiuchumi ndani ya uchukuzi nayo inakwenda vizuri, lakini nitaizungumzia Wizara ya Maliasili.

Mheshimiwa Spika, mimi ni balozi na katika kuwa balozi nina balozi mwenzangu ambaye ni Mwigulu Nchemba huyu ni balozi wa watu wenye ulemavu. Hii Wizara naomba na balozi mwenzangu na wewe unisikilize kwa makini na uje unipe majibu mazuri, kwanza wewe ni msikivu, nilikushauri suala la watu wenye ulemavu na kupata gawio lao katika kupitia Wizara na pamoja vijana hatuna cha kusema zaidi ya kukuombea Mwenyezi Mungu urudi tena katika Bunge hili mwezi wa 11 na kujiombea sisi sote tuweze kurudi katika wakati huo na hili ninaloliomba kwako naomba ukalifanyie kazi na nina imani utaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili inaingiza Pato la Taifa 22.5% lakini katika hii Wizara, Utalii peke yake unaingiza 17% lakini katika eneo la utalii inaingiza fedha za kigeni 30%. Hili eneo ninataka liboreshwe ili hizi pesa za kigeni badala ya kupata 30% tuna uwezo wa kupata hata 50%. Tujifunze tuona wenzetu wa Seychelles utalii peke yake inawaingizia karibu 75% ya uchumi wa nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nazungumza hivi? Mheshimiwa Rais alileta Royal Tour, hii Royal Tour imeleta wageni wa kutosha, watalii wanaoingia Tanzania ni wa kutosha wengi na watalii hawa wamevutiwa na spirit aliyokuja nayo Mheshimiwa Rais ya kuitangaza Tanzania duniani kote. Sasa tuna cha kujifunza hapa, watalii wanataka kuja hapa wakiwa na pesa zao za kigeni, wanahitaji malazi bora, wanataka barabara bora, miundombinu bora, mawasiliano bora ili na wao wazidi kuja wengi na wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuko katika vita ya kiuchumi, nchi zote za jirani zinafanya utalii, lakini utalii wa Tanzania umetukuka. Sasa nakuomba balozi wangu wa watu wenye ulemavu mimi ni mlemavu mwenzio, ninakuomba kitu kimoja angalau ukakifanyie kazi na ukiletee majibu. Leo pesa zote makusanyo yanayokusanywa na Ngorongoro, TANAPA yanakuja Mfuko Mkuu, zikija huku kurudisha kule inakuwa ni issue, bahati mbaya mimi ubalozi wangu lazima niusemee humu ndani tunahitaji wakusanye na watoe gawio kwenu, hapa msiwe na kigugumizi na tutahakikisha pato unalolitegemea la 30% la forex litaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilioni clip moja watalii wamekuwa stuck katika daraja huko kipindi cha mvua na walipofika pale wanaongea wanaomba duniani wasaidiwe wako katika mazingira magumu, leo ndani ya mbuga ni sehemu ambayo ni hatarishi, kuna wanyama wakali ikiwemo simba na tembo. Sasa ukiwaacha watalii wakiwa katika mazingira yale kwa kweli balazi mwenzangu naomba uniheshimieshe kwa hili nakuomba tafadhali na bahati nzuri mkae chini tu muwe na MOU tunataka sisi hela hii mtupatie, watawapeni at the right time. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Sheria ya Ununuzi kuna kitu kinaitwa you have to buy at the right time, with the right quality, quantity and price with the environment. Sasa kama tunakaa tunagemea watalii wanakuja, lakini barabara mbovu, wenzetu wata-take advantage ya kutuangamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kiwambie nilikuwa balozi wa kuhakikisha Geti la Gologonjwa halifunguliwi kwa kutaka Serengeti ipate mapato, leo Serengeti inapata mapato makubwa, lakini nakwambia hili kwa vile nimelifanyia tafiti. Katika kulifanyia tafiti nina imani kuwa hela mnazozihitaji kwa kupitia mashirika yetu TANAPA, Ngorongoro zitakuwa kubwa. Mashirika yako mengi, lakini haya mawili kwa vile hela zinakwenda Mfuko Mkuu zinakwenda kwa kusuasua kurudishwa kule kwao kwa kweli inawapa shida kubwa. Imani yangu umenisikia na utaifanyia kazi na bado nakwamini balozi mwenzangu kuwa utalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili Tanzania tuna NGOs 9840 na katika hizi NGOs 9840 wanasema wanaingiza pesa ambazo ni shilingi trilioni 2.4. Mimi maswali yangu Mheshimiwa Waziri na Gavana wa Benki Kuu ambao ninyi mnadhamana ya kusimamia pesa za Tanzania zinazoingizwa nchini, je, mnazikagua hizi pesa? Lakini vilevile je, zinaingia katika mpango mkakati wa matumizi bora ya nchi? Maana yake leo tunavyopata pesa kama zile tunataka tujue kilimo zimekwenda kiasi gani, tunataka tujue uvuvi zimeenda kiasi gani maana yake kama hamzisimamii hizi hela zinaingia katika movement na tumeona hizi pesa zinaingia katika movement, Congo wametengeneza M23. Hii M23 sasa hivi inaifanya nchi haitawaliki kwa vile hela za kutakatisha zimeingia kule na zinafanya vitu ambavyo havina maendeleo na mashiko ya nchi. Nina imani katika hizi pesa ambazo zinaingia kama hamzifanyii tathmini na kujua zinakwenda wapi na mkazifanyia ukaguzi zitaingia no reforms, no election. Watatumia nguvu kubwa ya kufanya matumizi hayo kwa vile nini wanajua hapo ndiyo eneo ambalo tutaigusa nchi hii na kuingiza katika tafaruku. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu Mheshimiwa Rais aweze kusimamia hili na ninyi sisi watendaji sote kwa pamoja tusiruhusu kuileta mianya ambayo itatufanya nchi hii iingie katika machafuko. Imani yangu mimi ninapenda sana nchi iwe na amani. Watu wa kwanza wanaoathirika katika machafuko ni walemavu. Mimi siwezi kukimbia, hivyo, nitakuwa mimi ninahangaika, wanawake na watoto watahangaika hapa. Hivyo, watu wanaotaka kuleta machafuko kama hayo tusikubali. Watanzania lazima tuungane kwa pamoja tusimame na amani na utulivu na hili Mwenyezi Mungu ninaamini itawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia maendeleo ya Mikoa ya Lindi na Mtwara, kwa nini? Mikoa mingine ninaona inakimbia katika maendeleo, lakini hata mipango ya pesa ambazo zinakwenda katika mikoa hiyo zinakuwa chache. Sasa sisi sote tunazungumza ni kama watoto wa familia moja, watoto wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaomba katika maeneo ambayo tunayazungumzia kila siku lazima yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, kwanza, tunahitaji barabara ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara mpaka Namtumbo ziimarishwe, kwa nini ninazungumza? Hii sasa hivi barabara ya kutoka Lindi mpaka Mozambique ni barabara ya kimataifa. Watu wa Mozambique wanategemea mizigo yao kuchukua kutoka Tanzania, lakini leo kama wamechukua mizigo kutoka Tanzania unaupeleka Mozambique katika mazingira yale kwa kweli hatujaifanyia haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tusimame na bandari ndogo ndogo, nimeona mwenzangu amezungumza hapa. Leo Lindi tuna bandari ndogo. Tukismama na bandari ya Lindi tukasimama na Comoro kwa kweli uchumi tutakaoupata hii tunayosema tunategemea shilingi trilioni 50 ambazo zimeshaweza kukusanywa mpaka leo nina imani Mheshimiwa Waziri wewe ni mchumi na wewe ni mwanasheria utazisimamia tutaweza kuvuka mapato yatazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, mimi ninasema tena Wizara ya Madini, Wizara ya Kilimo, na Wizara ya Utalii tusimame kwa pamoja Wabunge tuangalie na tuone tuweze kuisimamia na watendaji wakakae kusimamia hizi Wizara ili uchumi bora wa Tanzania hii uweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaizungumzia tena Lindi; Lindi ni kisiwa, leo Mkoa wa Lindi kipindi cha masika mtu wa Liwale hawezi kutembea, huwezi kwenda Liwale hata kwa gari,, mpaka hata Waziri alikwenda wakati ule Mheshimiwa Bashungwa alikwenda kwa helkopta. Sasa yeye alikwenda kwa helkopta, je, wananchi wa Lindi wanafanya nini.
Mheshimiwa Spika, hivyo, ninomba katika bajeti zenu hata kama pengine mlikuwa mmeitoa bajeti ndogo ninaomba bajeti ya Mkoa wa Lindi barabara zake ni mbaya, huwezi kulinganisha na mikoa mingine yote.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya ninakushukuru sana na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri - balozi kwa watu wenye ulemavu. Leo ninaona walemavu wako vizuri na wanakupenda, wanasema ahsante sana. Mwenyezi Mungu awabariki nyote. Ninawashukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Riziki Lulida, nilikuacha umalizie mchango. Nimesikia hapo umeitaja M23.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Nimetaja nini?

SPIKA: Kisha nikakusikia umetaja chama fulani hivi na jambo lao na kama unaweza kuzihusianisha hivi. Nimeelewa kama ulikuwa unazihusianisha hizi mbili?

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunirekebisha. Amenambiaje? Sijamsikia vizuri.

SPIKA: Kumbe uko tayari kwa marekebisho. Basi mchango wako kuhusu lile eneo la M23 ukikilinganisha na chama cha siasa kilicho hapa nchini ninayaondoa kwenye Taarifa Rasmi za Bunge.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana, tuko pamoja. (Makofi)