Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja muhimu hii ya Wizara ya Fedha na kabla sijasahau ninaunga mkono hoja ya Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, ukisoma taarifa ya Waziri moja ya jukumu kubwa la Wizara ya Fedha ni kutafuta vyanzo vya fedha na kukusanya mapato.
Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge wote humu ndani kwenye majimbo yetu tuna miradi ya maendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa. Tuna miradi ya maji, tuna miradi ya afya, tuna miradi ya elimu, tuna barabara, lakini miradi yote hii haiwezi kutekelezwa kama hakuna fedha. Kama fedha hazijatafutwa, hazijakusanywa miradi yote hii niliyoitaja haiwezi kutekelezeka itabaki kwenye makaratasi na itakuwa maneno matupu.
Kwa hiyo, Wizara hii ina jukumu kubwa sana la kubuni vyanzo na kuhakikisha mapato yanakusanywa ili miradi ya maendeleo iweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Spika, ukitembelea tovuti au website ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo ndiyo taasisi kubwa inayosimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani hapa nchini ukiingia kwenye tovuti yao ukaangalia takwimu za makusanyo, ukilinganisha na malengo ya makusanyo kwa mwaka huu wa fedha tulionao ambao unaisha mwezi huu na ukienda kwenye tovuti hiyo utakuta kwamba kuna takwimu za robo ya kwanza, robo ya pili na robo ya tatu na takwimu zote hizo zinaonesha Mamlaka ya Mapato Tanzania imevuka malengo ya makusanyo yake, yaani imefikia 100% na zaidi kwa baadhi ya miezi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nitumie fursa hii kwa kweli nimpongeze Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ndugu Yusuph Mwenda na Menejimenti yote ya TRA na wafanyakazi wote kwa jitihada kubwa ambazo zimeonekana kwa vitendo kwa takwimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuweza ku-maintain kufikisha 100% ya makusanyo against malengo tangu mwaka huu wa fedha ulioanza kwa at least kwa robo tatu hizi (miezi tisa ya kwanza) ni jambo ambalo linaonesha kabisa kuna menejienti nzuri na kuna kitu kikubwa ambacho kinafanyika ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mheshimiwa Spika, pongezi hizi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ninazitoa hasa kuwapongeza kwa kuendana na dhamira na maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo aliyatoa clearly kabisa kwamba anataka Mamlaka ya Mapato Tanzania ikusanye mapato kwa walipakodi kwa approach ya urafiki na majadiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, feedback ambayo tunaipata kwa walipakodi ambao ndiyo wapigakura wetu ni kwamba kuna improvement kubwa sana ya Mamlaka ya Mapato ukilinganisha na miaka ya nyuma kwa namna ambavyo wanatengeneza urafiki na walipakodi. Wanakaa na walipakodi na kunapokuwa na changamoto yoyote wanaitatua kwa njia ya majadiliano na maelewano tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na hali kama ya enmity kama uadui kati ya Mamlaka ya Mapato na walipakodi.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi niwapongeze TRA kwa kusikiliza na kutembea kwenye maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwataka Mamlaka ya Mapato wawe marafiki wa walipakodi na hii ndiyo feedback ambayo tunaipata kutoka kwa wapigakura wetu wafanyabiashara kwamba kuna improvement kubwa hata kama hatujafika kabisa 100% tunakotaka kwenda, lakini kuna improvement kubwa sana ya namna ambavyo Mamlaka ya Mapato wana-approach walipakodi wetu.
Mheshimiwa Spika, umuhimu wa kuunga mkono hoja ya Wizara hii na hasa nilipozungumzia umuhimu wa ukusanyaji wa mapato na mapato yanaenda kufanya nini, sisi sote kama Wabunge kwa mfano mimi jimboni kwangu bado nina miradi ya maendeleo ambayo inahitaji fedha ili iweze kukamilika au kutekelezeka, bado nina barabara inayounganisha Mkoa wa Tabora inapitia jimboni kwangu Bukene mpaka kufika Mkoa wa Shinyanga, barabara hii inahitaji fedha iweze kutengenezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka kadhaa tumekuwa tukipata fedha kidogo sana, kwa hiyo, tunatengeneza kilometa chache sana. Sasa suluhisho lake ili tuweze kuitengeza kwa haraka na kwa ukubwa ni tupate fedha na fedha zinatokana na makusanyo yanayosimamiwa na Wizara hii hususani kupitia taasisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nina miradi ya afya; kuna vituo vya afya vinaendelea kujengwa. Leo hii tumepewa taarifa kwamba baadhi ya majimbo yamepata fedha za kwanza za miradi ya kimkakati ya vituo vya afya, lakini majimbo mengine wiki hii fedha zinaweza kuingia. Sasa fedha hizi ili zipatikane inabidi zikusanywe, ni lazima zikusanywe na Mamlaka ya Mapato chini ya Wizara ya Fedha ndiyo tuwe nazo ndiyo tuzipeleke huko kwenye vituo vya afya kwa sababu itabakia maneno na kwenye makaratasi tu bila kuwa na fedha.
Mheshimiwa Spika, nina miradi ya barabara, nina miradi ya maji ambayo yote hii inahitaji fedha. Kwa hiyo, kuna kila umuhimu wa Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hoja ya Wizara hii kwa sababu Wizara hii ndiyo inabuni na ndiyo inasimamia ukusanyaji wa mapato ili miradi yetu itekelezeke ili iende ikafanyike na isibakie tu maneno kwenye bajeti. Kwa hiyo, ndiyo umuhimu mkubwa wa Wizara hii wa kubuni vyanzo vya mapato na kusimamia ukusanywaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ambalo pia limetajwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni matumizi ya mifumo katika usimamizi wa malipo ya fedha za umma kwenye taasisi zetu. Haina ubishi kwamba matumizi ya mifumo yanaongeza ufanisi kwenye taratibu za malipo, makusanyo kwenye taasisi zetu, lakini tumeweka mifumo mizuri kama MUSE na mifumo mingine, lakini kwenye baadhi ya maeneo tuna tatizo kubwa la uwezo au ujuzi wa wale watumiaji wa mifumo.
Mheshimiwa Spika, kuwa na mfumo ni jambo moja, lakini uwezo wa wale watumiaji wa mfumo ni jambo lingine. Kwa hiyo, unaweza ukawa na mfumo mzuri, lakini watumishi wa umma ambao wanaopaswa kutumia hiyo mifumo wanapokuwa hawana uwezo stahiki ile mifumo haileti ile tija ambayo tulikuwa tunaitegemea.
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya scenario kwenye halmashauri zetu huko fedha zinakuja za maendeleo, zinapaswa kwenda vijijini kutekeleza kazi fulani, lakini unakuta zinachelewa kwa sababu ya mifumo ya ulipaji na mifumo ya matumizi na wakati mwingine ukifuatilia unakuta ni uwezo wa mtumiaji wa mfumo tu, afisa aliyepo pale namna ya kutumia ule mfumo hana funzo, hana uwezo, hana nini kwa hiyo unakuta kwamba malipo yanachelewa miradi inachelewa kwa sababu tu ya mapungufu ya uwezo wa watumiaji wa mifumo.
Kwa hiyo, ninaunga mkono mojawapo ya vipaumbele vya Wizara ya Fedha kwamba kutoa mafunzo ya utumiaji wa mifumo kwa maafisa wetu wanaotumia mifumo ya malipo na matumizi katika maneo yao ya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja kwa 100%, ahsante sana. (Makofi)