Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Meatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu, lakini nikushukuru sana kwa kipindi chote nilichokuwa katika Bunge la Kumi na Mbili nimehudumu katika Kamati ya bajeti. Ninashukuru kwa kuniamini kwa kipindi chote, lakini ninakushukuru wewe kwa miongozo yako uliyoitoa katika Kamati yetu ambayo iliwezesha Kamati yetu kufikia matarajio yake ambayo yalipaswa sisi tuyafanye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niunge mkono hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Fedha nikimpongeza Waziri, Mheshimiwa Mwigulu, Naibu Waziri - Mheshimiwa Chande, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Watendaji wote na taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri mlizozifanya kwa kipindi chote tulichokuwa katika Kamati yetu kwa kutupa ushirikiano wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru wajumbe wenzangu wa Kamati ya Bajeti kwa ushirikiano mzuri tuliokuwa nao katika Kamati yetu na kusababisha taarifa zetu za Kamati zimekuwa na tija kwa ajili ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anazozifanya za kutuletea maendeleo pamoja na kutafuta fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi kubwa zimefanyika kupitia Wizara ya Fedha ambayo kazi yake ni kukusanya fedha na kutafuta fedha; na fedha nyingi zimetafutwa. Niipongeze TRA chini ya Kamishna wetu Yusuph Mwenda kwa kuvunja malengo kwa kila mwaka na kusababisha miradi mingi katika majimbo yetu kutekelezwa na hata miradi ya kimkakati ikiwemo Daraja la Kigongo – Busisi ambalo limejengwa kwa fedha za makusanyo ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri iliyofanywa nipongeze Fungu Namba 23 limetekeleza kazi yake vizuri ikiwemo kuwasilisha michango ya kisheria kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati na hili limejidhihirisha katika Kamati yetu. Walituletea mchanganuo wa taarifa zote ikiwemo PSSSF pamoja na NHIF kwa jinsi walivyopeleka fedha bila kuchelewa. Pamoja na hayo lakini kumekuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa uhuishaji wa michango ya watumishi na mwajiri kunakosababishwa na kutokusomana kwa Mfumo wa MUSE na mifumo ya malipo kwenye mifumo ya Hifadhi ya PSSSF, ZSSF, NHIF na WCF. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niungane na Mheshimiwa Rais alivyoomba mifumo yote iweze kusomana iweze kuleta tija kutokana na gharama ilivyotumia, lakini kuunganishwa na mifumo hii niliyoitaja itasababisha kuboresha utoaji huduma kwa watumishi pamoja na wastaafu, lakini katika fungu hili hili pia kuna kupungua kwa ari ya utendaji kazi kwa baadhi ya watumishi wa Hazina Ndogo ambako kuna kunachangiwa na uchakavu wa miundombinu pamoja na magari, lakini nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa mwaka huu unaokwisha mmejenga jengo zuri sana la Hazina Ndogo katika Mkoa wa Geita ambapo na mimi nilishiriki kwenda kuzindua hilo jengo nikimuwakilisha Mwenyekiti wangu wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, changamoto iliyokuwepo watumishi wa Mkoa wa Geita huduma hii walikuwa wanaipata Mkoa wa Mwanza, lakini nikuombe sasa kituo kinachofuata mtujengee jengo la Hazina Ndogo katika Mkoa wetu wa Simiyu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee Fungu Namba 45 ambalo ni la Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Fedha zimepelekwa vizuri, katika bajeti yetu hadi kufikia mwezi Aprili fedha zilipelekwa kwa 88% lakini pamoja na hayo kumekuwa na changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakaguzi wote kwa mujibu wa viwango vya kimataifa, uhaba wa vitendea kazi ikiwemo vifaa vya kuwezesha ukaguzi wa kiufundi, lakini kuongezeka kwa maeneo ya ukaguzi ikiwemo ukaguzi wa wakati halisi (real time audit) na ukaguzi wa kiufundi na ukaguzi wa mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Wizara ya Fedha iliwatengea kwenye matumizi ya kawaida shilingi bilioni 80, lakini ilipeleka shilingi bilioni 70, sawa na 88% hadi kufikia mwezi Aprili. Hii kazi ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amekuwa akitoa ushirikiano na Ofisi ya CAG na kwa mwaka huu wa fedha kwenye mapato yale ya kawaida yasiyo ya mishahara wametengewa shilingi bilioni 87.3 kuna ongezeko la shilingi bilioni saba, niwapongeze sana, lakini fungu hili linahitaji kuendelea kuongezewa ukomo, tunajua mlizingatia ukomo katika mwaka huu ndio maana mmeongezea shilingi bilioni saba, lakini fungu hili lina kazi kubwa kama nilizoziainisha. Endapo kazi hizi zitatekelezwa tutapunguza ubadhirifu wa matumizi ya fedha katika miradi inayotekelezwa kama miradi hii itakaguliwa kwa wakati, kama kutakuwa na ukaguzi wa mabadiliko ya tabianchi, tutazuia vile vihatarishi ambavyo vingeweza kuweza kutokea na kuweza kunusuru fedha za kuweza kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipongeze kwa kuiwezesha kimtaji Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) ambayo jukumu lake la msingi ni kuongeza chachu katika utoaji wa mikopo ili kuweza kufanikisha maendeleo jumuishi ya sekta ya kilimo nchini na kuchangia Dira ya Taifa ya Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajua zaidi ya 65% ya Watanzania ni wakulima na kazi kubwa imefanywa na benki hii toka ilipoanzishwa mwaka 2015 shilingi bilioni 971 zilinufaisha wakulima milioni 1.9 pamoja na biashara 686. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, biashara hizi zimeendelea kukopwa na kusaidia kurasimisha sekta zisizo rasmi katika wafanyabiashara ambapo itasaidia kuongeza wigo wa walipa kodi; lakini benki hii inakabiliwa na mtaji kwa sababu mtaji wake ni shilingi bilioni 924 na haipokei amana yoyote kama zilivyo benki za biashara. Hivyo, sasa niungane na maoni ya Kamati kwa kuhimiza ili iweze kutimiza dhamira yake, benki hii iweze kupewa mtaji wa jumla ya shilingi 2,900,000,000,000 ili tuwe na naksi ya shilingi 2,000,000,000. Tutaongeza wigo, tutawakopesha wavuvi pia katika sekta hii ya kilimo; tutawakopesha wafugaji ambao kundi hili bado limesahaulika katika sekta hii ya kilimo ambapo wafugaji wengi wapo wafanyabiashara ya mifugo ambao hawalipi kodi, tukiwapatia mikopo itawasaidia kuwarasimisha na kuongeza wigo wa ulipaji kodi. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
TAARIFA
SPIKA: Mheshimiwa Leah Komanya kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge dada yangu Leah Komanya, kwanza mchango wake ni mzuri sana, lakini kupitia eneo hilo hilo la Benki ya Kilimo kwa maana ya Serikali, kwa maana ya Wizara ya Fedha ilivyoongeza mtaji kwa Benki ya Kilimo. Nilidhani sasa iko haja ya Wizara hii kuona umuhimu wa kupeleka Benki hii ya Kilimo kwenye maeneo ambayo ni wazalishaji wakubwa hususan Mkoa wa Ruvuma ambako tumekuwa wazalishaji, tumeongeza kwa miongo mitano kwa uzalishaji wa mazao ya nafaka nchini Tanzania. Kwa hiyo, itasaidia kuendelea kukuza sekta hii ya kilimo na wakopaji ambao ni wakulima watakopa kwa ukaribu na kwa kufanya uwekezaji wenye tija zaidi, ahsante. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Leah Komanya unaipokea taarifa hiyo?
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa hii na naweka msisitizo pia kwa kuwezesha wakulima hawa, tutaongeza fedha za kigeni ambapo mazao yatapelekwa nje na kupata fedha za kigeni pia na kuongeza ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)