Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ole
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMA HAMAD OMAR: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitumie fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii adhimu. Wewe umekuwa ni Mheshimiwa Spika wa viwango na siku zote nakuwa nakuambia katika nyumba hii wewe ni dictionary wa Kanuni za Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu uzoefu huo ulionao ndio maana Umoja wa Mabunge Duniani wakakuteua kama Rais wao. Chonde chonde wananchi wa Uyole tunawaombeni kwa heshima na taadhima mturejeshee Spika huyu au mturejeshee Mbunge huyu ili tuweze kumpa tena Uspika na Inshallah aendelee tena na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, nataka nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri na pacha wake na Naibu Waziri. Mimi nilibahatika kufanya kazi ya Naibu Waziri katika kipindi cha Mzee Ruksa na nilitumika miaka saba niko pale kutoka 1985 mpaka 1992. Nimefanya kazi na Mawaziri watatu wa Fedha, wa kwanza kabisa alikuwa ni Mheshimiwa Cleopa David Msuya ambaye kwa heshima zote amezikwa hivi karibuni na wananchi wake wa Mwanga na Serikali. Waziri wa pili alikuwa Mheshimiwa Stephen Kibona aliyekuwa Mbunge wa Ileje, yeye kwa kweli Mungu amjalie mahala pema peponi, alifariki wakati yuko anaitetea Tanzania katika mikutano wa fedha ya World Bank na IMF, tukapokea maiti hapa.
Mheshimiwa Spika, wa tatu nilifanya kazi na marehemu Profesa Kighoma Malima. Kwa hiyo, nina uzoefu sana wa kufanya kazi katika Wizara hii kama Naibu. Nafikiri kama kuna Manaibu Waziri the longest sub ni mimi hakuna mwingine na baada ya hapo nilipata nafasi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema hapa ni kwamba siku zote Mawaziri wa Fedha na wataalam wao wanakuwa very conservative yaani wanakuwa ni watu si roho mbaya, lakini ni watu wana misimamo yao, akishashika msimamo huwezi kumpinda tofauti na Waziri Mwigulu na Mheshimiwa Naibu Waziri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri Mwigulu tumeona ni daktari unampinda, unamshauri anashaurika. Nafikiri kama sikosei 80% ya mapendekezo ya Finance Bill (Sheria ya Fedha) ya mwaka 2024/2025 aliyachukua na ndiyo maana yake tumekwenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawaomba jamani na naomba chonde chonde wananchi wa Singida Mashariki na wananchi wa Kojani kule Pemba wawachague tena Mawaziri hawa ili waweze kuwa Wabunge na Inshallah pengine Mwenyezi Mungu atawajalia tena kuwa Waziri na Naibu Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu na kumpongeza kwa kuwa na uono wa kuwachagua hawa watu wawili, lakini na yeye pia kwa kuwa na uono mkubwa, maana hawa ni washauri wake, lakini ultimately yeye ndiyo anayekata shauri. Kila Mbunge hapa ni shahidi katika jimbo lake jinsi ya landmarks, landmark maana yake ya jinsi ya mambo aliyofanya Mheshimiwa Rais. Ukienda kule Singida Magharibi yapo, ukija Pemba kule Ole yapo, ukienda Iramba yapo, ukienda Ole yapo, ukienda Kojani yapo, ukienda kwa rafiki yangu hapa Ally Kassinge yapo jimboni kwake. Kwa hiyo, kila Mbunge hapa ni shahidi wa matokeo ya maendeleo aliyoleta Mheshimiwa Rais, nasema Mungu amjalie miaka mitano tena na Inshallah basi aendelee pace na speed hii hii ili nchi hii iwe kabisa ni nchi ambayo imepiga hatua sana kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nataka nizungumze mambo mawili; moja suala la pensheni ambayo inalipa Wizara hii. Kuna kipindi kile cha awamu ya kwanza alichotawala Baba yetu Hayati Mwalimu Nyerere; kuna kipindi cha awamu ya pili alichotawala Mzee Rukwa, kipindi hiki ni mishahara ilikuwa ni midogo sana. Mimi nakumbuka nikiwa Naibu Waziri mwaka 1987 kama sikosei nilileta azimio hapa la kupandisha mshahara wa Rais, maana wakati huo ilikuwa mshahara wa Rais unazungumzwa hapa hapa Bungeni na unapandishwa hapa.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka tukampandisha Mzee Ruksa mshahara wake sasa sikilizeni vizuri hapo, tukampandisha Mzee Ruksa mshahara wake kutoka nafikiri shilingi 30,000 mpaka ikafika shilingi 50,000. Sisi wengine huku mishahara yetu ilikuwa shilingi 20,000 mpaka shilingi 30,000. Pensheni ya mwisho au ile pensheni ya kila mwezi wakati huo inategemea na mshahara wa mwisho. Sasa kama mshahara wa mwisho ni mdogo ina maana pia pensheni yako ya kila mwezi inakuwa ndogo. Sasa kilichotokea baada ya kustaafu Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Pili akaja Mheshimiwa Mkapa ikaanza kupanda mishahara ya wafanyakazi.
Mheshimiwa Spika, leo hii wale watu waliofanya kazi katika awamu hizo mbili, awamu ya kwanza na awamu ya pili huwezi kuamini pensheni yao wanayochukua kila mwezi ni chini ya kima cha chini. Sijui kama inaeleweka hapo, ni chini ya kima. Mimi ni mmojawapo nakwenda kuchukua pensheni ya kila mwezi, sitaki kusema hapa lakini ni chini ya kima cha chini napata shilingi 140,000.
Mheshimiwa Spika, kuna wanajeshi wengine huko makanali na wale waliopigana vita wanapata chini ya shilingi 120,000. Sasa mtu anayetoka Makunduchi akaja kuchukua pensheni ya shilingi 120,000 nadhani hiyo ni nauli yake tu; lakini Mawaziri waliostaafu hivi karibuni baada ya kipindi cha Mheshimiwa Rais Mkapa wanapata. Sasa ninaloshauri hapa, nadhani najua mnalifanyia kazi huko nchi nyingine pensheni wana-index as per cost of living, hali ya maisha inapobadilika na inflation inapobadilika pensheni wanairekebisha. Kwa vyovyote isiwe chini ya kima cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huyu mzee, huyu mwanajeshi aliyefanya kazi in the spirit of perfection and dedication katika hali ya kutekeleza mambo yake kiuadilifu na kwa ukamilifu mnampa pensheni hiyo, jamani tufike mahala hili tulirekebishe.
Mheshimiwa Spika, la pili nitakalochangia ni suala la deni. Kwanza, nashukuru sana kwamba deni letu ni himilivu, tuna uwezo sasa wa kulipa deni la nje na deni la ndani, hatuna wasiwasi na kwa nini tulikopa? Tulikopa kwa sababu ni wazi kwamba idadi ya watu inaongezeka katika nchi hii, tunazungumzia milioni 60, nafikiri katika mwaka 2050 tutakuwa karibu watu milioni 100. Kwa hiyo, mahitaji yanaongezeka, mahitaji ya kujenga miundombinu yanaongezeka, mahitaji ya hospitali, mahitaji ya shule, mahitaji ya kila kitu yanaongezeka. Kwa hiyo, lazima tukope, haina matatizo lakini msishangae kwamba sisi tunakopa kidogo na deni letu ni himilivu kuliko nchi nyingine hizo tunazoita nchi za matajiri.
Mheshimiwa Spika, mimi nina mifano hapa, kwa mfano Japan ni nchi ya viwanda, lakini ukichukua uwiano wa deni na pato la Taifa. Japan wanazungumza 266.2%; Marekani uwiano wa deni na Pato la Taifa unazungumzia 107.6%; inafuatia Ufaransa 115.7%. Sasa kwa maana ya sisi kukopa tumekopa kidogo sana ukija katika uhusiano huo. Katika Kusini mwa Janga la Sahara, Tanzania ni moja katika nchi ambayo haijakopa sana ukilinganisha na wenzetu. Uwiano wetu wa deni vs Pato la Taifa ni kama sikosei 39%, sasa hiyo ni kidogo sana.
Mheshimiwa Spika, na katika yale makundi manake hawa wanaokopa madeni unaweza ukawaweka makundi manne. Moja kundi lenye lililokuwa halina mzigo mkubwa ni nchi ya Botswana peke yake, lakini ya pili ni nchi ambazo ina mzigo hafifu wa deni hii ni pamoja na Tanzania. Kundi la tatu ni nchi zenye deni kubwa lina mzigo mkubwa, deni ni kubwa kidogo, hii ziko nchi kama 16. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna nchi ambayo imedhoofu lahali yaani lile deni tena limefika mahala limewaelemea mpaka linawaumiza, mpaka wanaokopesha wanafika mahali wanasema mamlaka ya kukusanya kodi na sisi tuiendeshe sisi ili tupate kukata deni letu, ziko nchi za namna hiyo. Mimi sitaki kuzitaja hapa kwa sababu ni nchi ambazo ni jirani zetu. Nitataja kidogo kwa mfano, Malawi, Zambia, Zimbabwe hizo ni nchi zenye mzigo mkubwa sana sisi hatumo katika hao. Kwa hiyo, nasema bado deni letu ni himilivu na kwamba tumekopa kwa ajili ya mahitaji yetu na pamoja kuongeza uchumi wetu. Sasa nasema hilo ni jambo la busara.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba nitumie nafasi hii kuiunga mkono hotuba ya Waziri wa Fedha, lakini Waziri wa Fedha asingefika mahali hapa kama si msaada mkubwa au kama si maono makubwa ya Mheshimiwa Mtukufu Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)