Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipatia nafasi niwe miongoni mwa wachangiaji wa leo.
Kwanza, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama na kuweza kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya katika kuhakikisha kwamba pamoja na misukosuko ambayo dunia imepitia, lakini Tanzania imeendelea kuwa imara katika sekta ya uchumi. Naomba niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri, Mheshimiwa Chande, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu wote hakika Wizara imepata watendaji ambao wamekuwa msaada mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, na mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti, naipongeza Wizara kwa sababu wamekuwa wasikivu sana. Michango mingi ambayo imetolewa na Kamati yetu ya Bajeti wameisikiliza na ushauri wamepokea na kwenda kufanyia kazi, hivyo nina kila sababu ya kuwapongeza.
Mheshimiwa Spika, mimi ninaomba nijikite katika Fungu 21 - Hazina na najikita katika fungu hili kwa sababu ndio waliokuwa na jukumu la kusimamia sera za fedha hapa nchini Tanzania. Kwa hiyo, wana wajibu wa kuhakikisha kwamba masuala yote ya sera yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, eneo ambalo naomba nijikite ni juu ya matumizi ya fedha taslimu. Huu umekuwa ni wimbo ambao tumekuwa tukiusema mara nyingi na Mheshimiwa Rais naye amekuwa akielekeza kwamba, sisi kama Taifa lazima ifike wakati ambao tuondokane na matumizi ya fedha taslim au tuanze kwa kupunguza. Kwa hiyo, naomba niungane na mchango ambao tumeutoa kama Kamati.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na ninyi mmekuwa mkitembea duniani. Ukienda katika nchi za wenzetu, ukisema unatoa dola 1000, 2000, watu wanakushangaa za nini hizo? Lazima twende ambavyo dunia inataka twende, lakini kubwa kwa nini watu wetu hawapendi kutumia malipo kwa njia ya kieletroniki, ni kwa sababu gharama ni kubwa. Pale ambapo unafanya transaction ukija ukafatilia gharama ambazo zinatozwa ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, gharama ni kubwa pale ambapo unafanya transaction ukija ukafuatilia gharama ambazo zinatozwa ni kubwa sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali wahakikishe kwamba wanafanya mapitio ili gharama za kulipa kwa kutumia njia za mtandao zinashuka na niukweli usiyopingika kama ukipata nafasi ukienda kuomba bank statement kama umekuwa uki-transact kwa kutumia miamala hii umemtumia mtu, mara umepokea ukianza kupitia zile charges ambazo unatozwa ni nyingi sana na ndiyo maana mtu akiona kama anataka kutuma fedha analinganisha je, niite bolt au nichukue bodaboda nimpelekee mtu cash kulikoni gharama ambazo natozwa kwa kutuma kwa kutumia mitandao ya simu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali gharama juu ya matumizi ya fedha taslimu ziko wazi la kwanza hii inasaidia wale watu ambao wanataka kukwepa kodi kwa kutumia pesa taslimu, lakini pia hata mtu ambaye anataka kutoa rushwa ni rahisi kwa kutumia pesa taslimu.
Mheshimiwa Spika, kwa mtu ambaye anataka kutakatisha fedha kama ambavyo Taifa tulikuwa na changamoto kubwa sana naomba tusirudi huko, lakini hata mtu anapotaka kumuibia mwenzake atamwibia fedha ambayo ni taslimu katika hali ya kawaida kwa utumaji kwa kutumia mitandao siyo rahisi inadhibiti wizi. Kwa hiyo, niiombe Serikali kubwa zaidi tuhakikishe kwamba gharama zinapungua ili watu wetu wahamasike kutumia cashless badala ya kwenda kutumia hii habari ya noti na gharama zingine ziko wazi.
Mheshimiwa Spika, ukiwa na noti ku-print ni gharama siyo kwamba zinatolewa bure ni gharama, lakini hata utunzaji wa noti na sarafu nao ni gharama. Inafikia kipindi Benki Kuu wanalazimika kuchapisha fedha zingine kwa sababu ambazo ziko kwenye mzunguko zimechakaa. Kwa hiyo, niiombe Serikali tuhakikishe kwamba kama taifa ukienda kwa majirani siyo vizuri kutaja ukipanda hata taxi unavyotaka kulipa cash anakwambia nikupe pin uweze kulipia, hayo tuyaige mambo mazuri. Ukiona mwenzako anafanya vizuri hakuna ubaya kuiga hayo mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo naomba nishauri ni upande wa BOT. Wamekuja vizuri sana kuhakikisha kwamba kama Taifa hii habari ya dollarization tunaondokana nayo, lakini kuna sehemu ambayo naamini watalamu ni vizuri wakaenda kuchakata, wakaja na suluhu ambayo itakuwa inasaidia sisi kama Taifa. Ukisema kwa service ambazo natoa nje ya nchi halafu nataka u-quote kwa shilingi duniani hawatuelewi yaani unampata mtalii anafanya booking huko Marekani unamtumia kwamba shilingi ndiyo ambayo itumike kama quotation hawatuelewi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kama taifa tunahitaji dola kwa sababu siyo kwamba vitu vyote tunazalisha hapa nchini kwa hiyo uwepo utaratibu madhubuti wa kuhakikisha kwamba dola hizo zinaingia Serikalini tusijetukalazimika ku-create black market. Kwa sababu tunalazimisha watu kwamba lazima alete shilingi jambo hilo halipo dunia ya hivyo haipo.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana mnawaambia watu ambao wanashughulika na utalii mna-quote exchange rate ambayo inatolewa na BOT. Wakati ukienda kwenye mabenki yetu, ukienda kwenye bureau zetu hakuna hata sehemu moja ambapo utakuta quotation ambayo iko ya Benki Kuu ndiyo ambayo inatumika. Sasa tafsiri yake ni nini? Tunalazimisha black market.
Mheshimiwa Spika, mtu anachukua fedha, anaenda ku-change vichochoroni, halafu kwa sababu wewe ume-quote kwenye bei ya exchange rate ya BOT, maana yake kama Serikali mnapata hasara na hasa taasisi za Serikali kama TANAPA kwa sababu mnacho-quote ni kile ambacho hakipo duniani.
Kwa hiyo, hakuna sababu ya kuhakikisha taasisi za Serikali zinapata hasara kwa barua au waraka ambao umetolewa na Benki Kuu in blanket, hakuna jambo ambalo linaweza likawa moja lika-fit yote (one size fix all) haipo. Kwa hiyo, naomba kama Serikali mlichakate hili ili muone kama taifa tunahitaji dola, isijeikawa kwamba waraka mmoja unasaidia kwa watu wote.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo naomba nitoe mchango, naomba niipongeze Serikali, Waziri wa Fedha umekuwa msikivu sana juu ya uanzishaji wa tax ombudsman, lakini bila kuwa na sheria ambayo itasababisha akafanye kazi zake itakuwa ni kama tumeanzisha taasisi ambayo haisadii lolote. Ni vizuri upitie mchakato muitazame sheria ile ili iwe na manufaa juu ya uanzishaji wa ofisi hii, vinginevyo itakuwa haitusaidii kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, jambo jema pale ambapo anayelalamikia suala la kodi au analalamikia jinsi ambavyo labda hakutendewa haki awe na sehemu ambayo anaiamini kwamba nikipeleka malalamiko yangu nitasikilizwa na haki itatendeka kabla ya kwenda kwenye rufaa za kodi na taasisi zingine.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuchangia hayo naomba niunge mkono hoja, ahsante. (Makofi)