Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kasalali Emmanuel Mageni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote kabla sijasema sana naomba nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameifanya nchi yetu iendelee kukua kiuchumi, lakini iendelee kuwa na uimara wa pesa za kigeni na tuendelee kuwa na nchi ambayo inakopesheka na inayoweza kufanya miradi yake yenyewe. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais pongezi za watu wa Sumve zikufikie moja kwa moja.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nisiwe mchoyo wa fadhila nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu kwa namna ambavyo anasimamia Wizara hii na namna ambavyo amejitahidi kwa kazi kubwa aliyoifanya katika muda huu ambapo amekuwa Waziri wetu wa Fedha, lakini pia Naibu wake, ndugu yangu Mheshimiwa Chande kwa namna ambavyo umekuwa mtu mwema, umekuwa msaidizi mwema kwa Mheshimiwa Waziri na wakati mwingine mtu anaweza akakuona wewe akaona kama amemuona Waziri vile, amekuwa anafanyakazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo naomba sasa nijielekeze kwenye hoja yangu ya msingi. Unapokuwa Waziri wa Fedha unajua fedha, Wizara ya Fedha kwa dunia ya sasa pesa ni kila kitu yaani unahusika na maisha ya watu moja kwa moja na ili Serikali ipate pesa ni lazima ikusanye ushuru, hakuna pesa inapatikana nje ya utaratibu huo lazima tukusanye ushuru ili tuwe tuna pesa ya heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunazo sababu za msingi kabisa za kuhakikisha Mamlaka yetu ya Mapato (TRA) inaendelea kuimarishwa, inaendelea kufanya kazi vizuri ili Serikali yetu iweze kupata pesa ya kuendesha miradi ya maendeleo. Kwa kusema hayo naomba kwa sasa nimeangalia ripoti ya TRA ya robo ya mwezi wa kwanza mpaka Machi, wameongeza kiasi cha ukusanyaji wa mapato, lakini kiasi cha ukusanyaji wa mapato kimeongezeka kwa miezi tisa mfululizo yaani tumekusanya huu mwezi wa kwanza mpaka wa tatu zaidi ya trilioni saba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo inavyoonekana Mamlaka yetu ya Mapato inafanya kazi vizuri mpaka sasa, ongezeko la ukusanyaji wa pesa ni heshima kwa nchi yetu, lakini ni nafuu kwa Watanzania wote na kwa nafasi hiyo naomba nimpongeze Kamishna wa TRA, Ndugu Mwenda kwa namna ambavyo ameifanya Mamlaka hii ya Mapato kwa muda mfupi kuendelea kufanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato imefanya vizuri muda mwingi tangu Mheshimiwa Rais aiingie madarakani kila mara makusanyo yanapanda, lakini sasa yamepanda zaidi na zaidi kwa hiyo hongereni sana Mamlaka ya Mapato, lakini ipo kazi kubwa tunatakiwa kuendelea kuifanya, tunatakiwa tuongeze wigo wa walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado Watanzania wanaolipa kodi mbali na kwamba idadi ya mapato yanaongezeka wanaolipa kodi bado ni wachache sana. Kuna kazi kubwa ya kufanya kwenye Mamlaka yetu ya Mapato, ipo sababu ya watumishi wetu wa Mamlaka ya Mapato kuendelea kupata msasa na ushauri wa namna bora ya kuifanya nchi yetu ikusanye mapato zaidi na zaidi. Haiwezekani sisi na ukuaji wetu wa uchumi huu tuendelee kuwa na mapato ya shilingi trilioni 20 ngapi tunatakiwa kuwa mapato makubwa zaidi na zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mamlaka yetu ya Mapato inatakiwa iwekeze zaidi kwenye kukuza wigo wa mapato, lakini ipo kazi kubwa tunatakiwa kuifanya, kuna kitu mimi kwa uzoefu nimekiona, mimi nafanyakazi ya biashara biashara kidogo.

Kuna hawa watu sijui tusemeje kidiplomasia, lakini tuna wafanyabiashara wengi kutoka nje ya nchi, wengi wao wamejaa kwenye biashara zetu, kwenye mzunguko wetu wa biashara wanatoka Bara la Asia na hawa watu tunawaita Wachina wapo sana kwenye biashara zetu na ni wajasiriamali wazuri wameingia kwenye biashara, wako aggressive, wanafanyabiashara. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, ni kwa ushauri tu kwa Wizara ya Fedha na TRA kwa uzoefu wangu mdogo na tunayoyasikia ni wazoefu sana kwenye kukopa kodi, mna kazi kubwa sana ya kufanya. Yaani kutoa risiti na kulipa kwenye akaunti ni ugomvi mkubwa, yaani unapomwambia naomba akaunti nilipe atajitahidi akushawishi alipwe cash lakini unapomuomba risiti atakupa mpaka elimu kwa nini uchukue na kwa nini usichukue? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaani inafika wakati anakwambia nikikupa risiti nitakuuzia shilingi 200,000 nisipokupa risiti tutatoa hii ya TRA nitakupa ukaenayo wewe, kwa hiyo, mimi utanipa tu nisikupe risiti. Sasa hii elimu ya ujasiri wa kukwepa kodi Watanzania tulikuwa hatuna, tunaanza kupandikizwa elimu ya ujasiri wa kukwepa kodi na kujua kwamba hii 18% nikiipeleka TRA yaani wewe hutaishika, lakini mimi sasa hivi nikupe kwa laki na nusu hii 18% yako ubakinayo kila mmoja aendelee na maisha yake unipe cash. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nini tunapaswa kufanya kama nchi ili kuboresha ukusanyaji wa mapato? Lazima tutoke, kuna mchangiaji ametushauri hapa tutoke kwenye cash economy, ni lazima tutoke huko kama kweli tuko serious na tunataka tuweze kukusanya mapato vizuri na Taifa liendelee mbele, lazima tutoke mtu anahesimika kwa sababu ana cash hii ni imeishakuwa ni ushamba, lazima tutoke kwenye cash economy, ni lazima malipo mengi yafanyike kwa utaratibu wa kieletroniki, tutafanya hivyo kwa kuimarisha mifumo yetu ya malipo, ni lazima tuimarishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifikie wakati mtu awe na uwakika kwa sababu ukienda hata kwenye hoteli unakula, umemaliza kula nalipa ukisema tu nalipa kwa simu unaona yule muhudumu amebadirika sura yaani kila mmoja anata alipwe cash. Naomba risiti unaona mtu anarudi nyuma wakati mwingine hata alikuwa ana kitu anakwambia hana. Sasa hiyo elimu kwa wafanyabiashara lazima iende, elimu kwa Watanzania lazima iende, elimu kwa watumishi wetu wa Mamlaka ya Mapato lazima iende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watumie muda mwingi pia kuwaelimisha watu wanaolipa kodi, wafahamu umuhimu wa kulipa kodi, lakini wafahamu pia umuhimu wa kutoka kwenye hizi njia za cash. Watu wengi wanakimbilia huko kama mzungumzaji alivyosema Mheshimiwa Kandege, kwamba makato yanakuwa mengi, lazima tuweke makato rafiki ili kila mmoja awe salama, hakuna mtu anapenda kutembea na mahela, unatembea umebeba hela una hela una wallet yale mambo ya kizamani, sijui wallet imetuna hivi ni mambo hayo yanatakiwa yatoke huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwe tuna pesa kwenye simu zetu pesa kwenye kadi zetu unakoenda kokote unalipa unapata risiti, nchi inapata pesa tukipunguza makato karibu kila mtu atatumia huo utaratibu. Kuna wakati tunafanya biashara sisi unakuta bandarini kuna wakati unashindwa kupeleka mzigo mtandao umegoma, hii haitakiwi kuwepo lazima mitandao yote ya kupokea mapato, mitandao yote ya kupokea mizigo ihakikishe inakuwa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini mabenki yanakuwa muda wote wenyewe hawatuambii kwamba unapeleka hela wanakwambia mtandao haupo au mfumo kwa nini tusijifunze huko wao wanafanya nini? Yaani kwa nini mitandao yao ni imara? Mamlaka yetu ya Mapato ndiyo baba wa nchi hii, ndiyo mama wa nchi hii, anakusanya pesa sisi twende mbele, tumuhimarishe, tuhimarishe watoza ushukuru wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua hakuna jamii inapenda watoza ushukuru, lakini ili muishi lazima awepo mtu awasaidie kutoza ushuru, atoze ushuru, watu hawapende kulipa ushuru, lakini watozwe ili nchi iende, lakini ili nchi iende watu walipe kodi lazima tuweke mifumo rafiki ya ulipaji kodi na ili tuweze kupambana na uchumi wa dunia ya sasa tupambane na wale wanaitwa wakati mwingine mabeberu, tupambane na masharti magumu kutoka nje ya nchi yetu ni lazima tujitosheleze wenyewe. Watanzania lazima tuwe na morali ya kujitosheleza wenyewe tuwe matajiri wenyewe, tutumie pesa zetu wenyewe sasa ili tuzitumie lazima tuzikusanye vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na mambo hayo limezungumzwa suala hapa la wastaafu na nadhani mzungumzaji ameshauri vizuri sana. Serikali yetu mbali na kwamba tunafanya vizuri kwenye maslahi ya watumishi na tunaboresha mifumo yetu lazima hili tuliangalie suala la wastaafu, kwenye suala la pensheni message tunazo nyingi sana. Hata mimi nilivyokuwa hapa tu kuna mstaafu mwingine kutoka Jimboni kwangu kanitumia message tusemee pensheni yetu bado iko chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wastaafu ni wachache sana, wazee wetu hawa ambao wamefanyakazi kubwa ni lazima tuone namna gani sera zetu za pesa, sera zetu za nchi zinawaangalia na kuwafanya kwamba ustaafu au kustaafu isiwe ni tatizo; kustaafu iwe ni heshima ili kila mmoja ataniwe kustaafu kwa sababu anajua nikistaafu napumzika kazi maisha yanaendelea kuwa mazuri, isije ikatokea kwamba mtu anajua nikistaafu naenda kwenye mateso basi mtu ajitahidi asistaafu wakati mwingine aongeze hata umri, wakati mwingine awe king’ang’anizi kwenye jambo fulani, nadhani hiyo Mheshimiwa Waziri na timu yako nakupitia Wizara nyingine najua siyo la Wizara yako tu moja mnaweza kulifanya kwa uzuri na kufanya nchi yetu iendelee kuwa bora na Watanzania tuishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba uniruhusu niunge mkono bajeti, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kasalali umesema mwenyewe, lakini nikajua utajiambia wewe mwenyewe, naona wewe mwenyewe tena ukaenda ukapinda kwa mbele. Umewataja hapo watu kutoka Asia halafu ukawataja wengine maalum na ukaonesha kama wao wanawafundisha ujasiri Watanzania wa kukwepa kulipa kodi. Sasa wacha nikupe nafasi uyaondoe ni kukwepa tu awe Mtanzania awe mwingine wote ni kukwepa ili tusiingie huo mkanganyiko wa kuanza kutafutana kidiplomasia. (Makofi)

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba maneno hayo yaondolewe kwenye Hansard. (Makofi)