Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hii Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu, muumba wa mbingu na nchi kwanza kupata nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu ambayo kila mtu hapa ndani anaitegemea, ukweli ni kwamba bila Wizara hii yaani huwezi ukafanya chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameonesha kuwa Rais wa pekee mpiganaji na kila mmoja hapa tumekuwa tukiulizana mambo ya wilayani yanaenda vizuri kwa maana ya kwamba mama amesimama imara kuhakikisha kwamba anaipigania nchi yetu na kutupambanania kuhakikisha kwamba Taifa letu linapiga hatua.
Mheshimiwa Spika, tatu nikushukuru Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, ukweli ni kwamba mnajitahidi kadri ya uwezo na Mungu aendelee tu kuwapa uwezo na fikra za mbali zaidi ili kusudi tuweze kuenenda na mambo yanayotakiwa kwenye ulimwengu wa sasa wa kidigitali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru wananchi wangu wa Mbogwe ambao ndiyo wamenituma hapa niweze kusimama ndani ya Bunge lako kuwasilisha mawazo yao, lakini pia kuchangia hii hotuba ya Wizara ya Fedha, maana kila kitu tunahitaji pesa kwa hiyo kikubwa hapa kwanza Waziri naomba unikubalie ni kweli kwamba watu wengi hawalipi kodi, ukiangalia vizuri kiuhalisia watu wengi kweli hawalipi kodi, wanakwepa sana, wafanyabiashara wadogo na wakubwa hasa maeneo ya mjini, Kariakoo huko unakuta mtu anafanyabiashara na kama alivyopita huyu mzungumzaji anakupa na elimu kabisa nikikupa risiti nitakuuzia shilingi milioni mbili ila nisipokupa risiti nitakuuzia shilingi milioni 1.5.
Mheshhimiwa Spika, Waziri kwa hiyo wewe ndiyo refa wa hii Wizara, ukisimama vizuri wewe na vyombo vyako hakika tutapita hapa tunapopafikiria kwenye shilingi trilioni 50, lakini ukisimama legelege wanasemaga yaani mtu ukiwa legelege na mambo yataenda legelege tu, kwa hiyo, kuna kila sababu taratibu na miongozo mnayoitengeneza kwenye Wizara hii lazima iwe na makali kidogo kwa sababu suala la kulipa yaani kutumia ni rahisi, lakini kulipa yaani ni kazi ngumu sana, lakini kwa vile hata kwenye maandiko matakatifu hili limo kwamba kulipa kodi ni muhimu kwa vile hata kwenye maandiko matakatifu hili limo kwamba kulipa kodi ni muhimu kwa sababu watu tunataka maendeleo na hatuwezi kupata maendeleo kiukweli bila kulipa kodi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna kila sababu Waziri kuangalia kwamba ni utaratibu upi utumie kusudi watu na Watanzania wote tulipe kodi.
Mheshimiwa Spika, mimi nimpongeze kaka yangu Dkt. Doto Mashaka Biteko, wakati anaingia kwenye Wizara ya Madini, ulipaji wa kodi ulikuwa chini sana, lakini alikaa kama Waziri akatengeneza timu na mpaka sasa hivi kwenye madini huko na mimi ni-declare interest ni mfanyabiashara wa madini, tunalipa haki wote sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hakuna dhambi kujifunza kwa Biteko kwamba yeye alifanyaje akafanikisha vipi (kutoa mapato yaliyokuwa yanakusanywa kwenye dhahabu mapaka kufika mpaka sasa hivi pale tulipo). Ina maana alitengeneza miongozo lakini ikiwemo na kukaa na wafanyabiashara kwamba nini na nini tufanye, ili kusudi tuache kukwepa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kila sababu Waziri pamoja na Naibu wako na watendaji wote kwa sababu wapo hapa mbali ninaongea nikiwa ninajua vyombo vyote vipo hapa. Kuna kila sababu kila mtu kwenye eneo lake kukaa na wafanyabiashara, mkoa ama wilaya akawauliza wafanyabiashara hawa wa ndani ni nini ambacho kinachowafanya wakwepe kodi na wao wanazo sababu za msingi.
Mheshimiwa Spika, kwanza, Waziri ninaomba nikushauri, wewe ni msimamizi wa benki. Hii biashara sasa hivi tunafanya na mataifa mbalimbali kwenye nchi zetu (East Africa Community) biashara tunafanya kwa pamoja. Unakuta mwenzio amechukua benki ile ile amefanyiwa 8%. Wewe huyo wa Dodoma hapo ama Mbongwe umepewa 22%, sasa vita inaanzia pale. Bahati mbaya zaidi sisi wafanyabiashara huwa hatufichani. Tukikaa kwenye dawati la biashara lazima uulize wewe meneja amekupa mkopo wa riba gani. Sasa vita inaanzia hapo wenzako ana 8% wewe una 22%. Hapo kwanza unaanza kujisikia vibaya, hapo tu kwenye butcher wewe aumeshapunjwa 12%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna kila sababu ya kuanza kutengeneza mifumo kwa vile mimi wananiona hawa ni wa nini, acha tuanze sasa kukwepana, lakini lazima tujifunze kwa wale waliotutangulia. Kwa mfano, kwenye mafuta, Wizara ya mafuta sisi tuna mashine za EFD. Sasa hivi huwezi ukatoa mafuta bila risiti. Sasa ni kazi kwenu Wizara hii na ninyi kutengeneza performance ya kuangalia ni jinsi gani kwenye sabuni huku, kwenye maduka mtumie mifumo gani kama walivyotu-tight sisi wauza mafuta hata kama ukiwa unafaulisha ina maana unalipa kodi.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa kawaida sana Mheshimiwa Waziri kuna kila sababu hata ya kukaa na wafanyabiashara a kuwawekea mifumo kama hizi ni kamera, ili bidhaa zinapokuwa zinauzwa zinaonekana kwamba stock mteja amechukua boksi ngapi za sabuni ama nguo ngapi. Huo ni ushauri wa kwanza, kwa sababu tunaweza tukaongea maneno mengi sana kama hatuna fedha ki ukweli hatuwezi kupiga hatua.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri unakumbuka nilikuuuliza swali mwaka 2023 kwamba ni kwa nini sisi Shilingi yetu haipandi? Sasa huu ni wakati muafaka pamoja na kwamba mnafanya vizuri zaidi, lakini niwakumbushe tu Wizara hii kuna kila sababu kufikiria kama wachumi na wasomi wetu Wizara ya Fedha, tutumie mifumo ipi ili kuendana na wenzetu majirani?
Mheshimiwa Spika, mimi binafsi huwa ninaumia sana, mimi ninafanya biashara sana. Ukitoka Rusumo tu ukiingia Rwanda kama una shilingi milioni 100 yako uka-change faranga za Rwanda yaani unabakiza mfuko mdogo tu. Sasa unafikiria kwa nini sisi tunafanyiwa vitu kama hivi? Pia hata ukiondoka hapa ukaenda na shilingi milioni 100 ukifika tu Kenya mpakani uka-change fedha zako hata kama usiponunua kwenda na kurudi tayari unakuwa umeshakula hasara. Kwa hiyo, kuna kila sababu hapo Mheshimiwa Waziri na lenyewe kuliangalia ili kusudi muweze kupandisha shilingi yetu na uchumi wetu uweze kupanda kidogo. Tukipandisha uchumi ina maana vitu vyote vinashuka chini. Madeni tunakuwa nayo uwezo wa kuyashusha chini, vilevile kila kitu vitakaa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri hapa ambalo ninapenda nikushukuru nikukumbushe ulinipatia akili mwaka 2022 na mpaka sasa hivi wilaya yangu inajitegemea. Walimu zamani walikuwa wanafuata mishahara Bukombe, sasa hivi wanapata hapohapo Masumbwe. Wameniomba Halmashauri ya Mbogwe inahitaji tena ofisi nyingine pamoja na matawi ya benki kwa maana NMB na CRDB. Makao Makuu ya Mbongwe kutoka Masumbwe Mjini kwenda Mbogwe ni kilometa zaidi ya 50. Kwa hiyo, mwalimu atoke Ikungwigazi pamoja na Ngemo akiwa anafuata mshahara tu inam-cost.
Kwa hiyo, ninaomba uniweke kwenye bajeti yako hii tena matawi ya benki yaweze kuongezwa makao makuu ya wilaya yangu, ili kusudi wananchi waliopo maeneo hayo waweze kufaidika na Serikali hii pamoja na mimi Mbunge mwenyewe ambaye ninaenda kumalizia muda wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri, hii mifumo kweli Serikali tunaipongeza inajitahidi sana kutupatia fedha, lakini mmeweka mifumo hapa katikati wengi hawajui kuitumia hii mifumo. Mimi nina Mfuko wa Jimbo, nina fedha sasa hivi zina miaka miwili. Nimeahidi, nimepita kila maeneo, lakini kila wakifanya kwenye mifumo, fedha sawa zimo lakini hazitoki. Kwa hiyo, na penyewe kuna kila sababu Mheshimiwa Waziri kuliangalia na kuwapatia semina hawa Watumishi wa Serikali kwa maana ya Watendaji wa Kata, tena uzuri unao hapahapa wa jimboni kwako unaweza ukaanza nao na wao wakaenda kuambukiza kwenye wilaya nyingine huko, ili kusudi fedha zisiwe zinakwama kwenye mifumo hii ya NeST. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine Mheshimiwa Waziri ninapenda kukupongeza kweli unapambana lakini hapa kwenye NeST angalia vizuri baba yangu, ili kusudi mambo yaende vizuri zaidi. Kweli tunahitaji fedha hasa, lakini swali la kwanza kabisa ni vyema hapa kwenye kukusanya tu ndio unatakiwa ukae vizuri wewe pamoja na wenzako ili kuiwezesha Serikali yetu iweze kupiga hatua, halafu na kazi nyingine zifanyike.
Mheshimiwa Spika, mwisho ninapenda nikushukuru wewe, pia niwashukuru wananchi wangu wa Mbogwe wote wapigakura. Tukiwa tunaelekea tumebakiza Bajeti Kuu na penyewe ninaimani nitapata nafasi. Niwaombe tu viongozi wangu humu ndani wazidi kunipanga na kuniamini na kwa kweli sasa hivi nimekomaa na mimi ninajiona nipo fit, nipo vizuri. Hakuna jambo litaharibika katika kuishauri Serikali kwa sababu jukumu la Mbunge ni kazi tatu nimeona na mimi nimesimama imara kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utakumbuka wakati ninaingia humu ndani Wilaya ya Mbogwe ilikuwa haikusanyi kabisa. Mliniambia kama Serikali kwamba nikasimame kuhakikisha maovu yote ya yanapoonekana jimboni ninatoa taarifa hapa na Serikali inafuatilia. Ninawapongeza Serikali ambao wamenipatia ushirikiano ndani ya miaka hii mitano, kwa kweli wakinipatia miaka mitano mingine ina maana mambo yatazidi kuwa mazuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimuombe huyu msimamizi tumeambiwa kuna Mkurugenzi wa Kusimamia Fedha Haramu. Hili jambo Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana. Huku ninamalizia.
Mheshimiwa Spika, hili jambo ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri. Kweli kabisa hizi fedha haramu zipo. Unajuaje zipo wewe ni mtaalam na msomi. Unaweza ukamuona mtu anajenga ghorofa lakini hajulikani anafanya biashara gani. Kwa hiyo, kuna kila sababu anapoonekana mtu kwamba anafanya maendeleo fulan,i lazima tujue kwamba huyu anafanya biashara gani, Serikali ametulipa kodi ya design gani? Hakuna kuoneana huruma katika mambo ya fedha haramu kwa sababu tunafahamu wapo watu wanaouza madawa ya kulevya, pia wapo watu ambao wanaibia wengine na wanafanya maendeleo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho nikushukuru mama yangu. Mungu akubariki sana Spika wetu, Mbunge na Rais wa Mabunge yote Duniani. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)