Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kupewa nafasi hii adimu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Waziri wa Fedha na nianze kwa kuwapongeza sana kwa kazi nzuri sana ambayo mmeifanya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha. Kwa kweli mmefanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuthibitisha kwamba wamefanya kazi nzuri unaweza ukaona hata mapato ya Serikali yalivyoongezeka, lakini unaweza ukaona Bajeti ya Serikali wakati wanaingia ilikuwa chini ya shilingi trilioni 29, sasa hivi ni zaidi ya shilingi trilioni 50. Hiyo ni ishara ya kazi nzuri mliyoifanya kwa kweli tunawapa hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Wizara kwa sababu Wizara hii ndio wasimamizi wa hesabu zote za Serikali na ndio wasimamizi wa wahasibu na wakaguzi wa ndani na wa nje. Katika kipindi hiki tumeshuhudia ripoti ya CAG, ripoti zake zimeonesha uimarikaji wa uwajibikaji na usimamizi mzuri wa fedha za umma. Ripoti hizo zimeonesha kutokana na ukiangalia taarifa za CAG zinazoridhisha zimeendelea kuimarika na zimekuwa ni nyingi kabisa na sasa hivi zile hati chafu zimekuwa kama ni historia, hazipo. Hii ni ishara kwamba kazi nzuri imefanywa na inaendelea kufanywa na hii Wizara Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee mimi ninaomba nizipongeze taasisi ambazo zimeonesha umahiri mkubwa wa kutayarisha hesabu za fedha vizuri na kwa viwango vizuri vya kimataifa. Moja ya taasisi hizo ni taasisi unayoiongoza wewe, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefanya vizuri sana. Katika mashindano ya vitabu vizuri vya uhasibu, Bunge tuliongoza tukashinda, kwa hiyo tumefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi ninakupongeza lakini ninaipongeza Wizara kwa kusimamia vizuri na kuhakikisha kazi inafanyika vizuri. Pia CAG ninampongeza kwa namna anavyofanya kazi ya ukaguzi. Kazi ni nzuri na ndio maana tunasema waendelee kuongezewa uwezo na fedha na rasilimali, ili aendelee kufanya kazi vizuri na uwajibikaji Serikalini uendelee kuimarika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ninapenda nitoe mapendekezo machache; la kwanza, sasa hivi kumekuwa na taasisi nyingi zile ambazo zilitakiwa zijitegemee, zilitakiwa zizalishe, zikusanye mapato yao, zijiendeshe kibisahara, taasisi hizo nyingi zimekuwa zinarudi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kutegemea mishahara kutoka Hazina. Sasa hii ya kutegemea zaidi mishahara kutoka Hazina inazifanya zile taasisi zibweteke, zisifanye kazi vizuri. Zipo taasisi nyingi za namna hiyo.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mkalifanyie kazi mzichambue. Zile zinazoweza kusimama zenyewe, zisimame zenyewe. Wakala wanaoweza kusimama wenyewe, wasimame wenyewe badala ya kutegemea fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali. Hili ni suala muhimu na ninafikiri litasaidia sana kupunguza mzigo wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ninamuomba Mheshimiwa Waziri, kwanza ninawapongeza maana yake nimesikiliza taarifa yako nzuri na taarifa ya kamati imeonesha vizuri. Kwanza mafunzo ambayo mmeyatoa kwa wahasibu ni wengi nimesikia, mmetoa mafunzo mengi, lakini ninataka kuongezea kusema kwamba, bila mafunzo na wahasibu hawa kupata mafunzo ya kila wakati, bila wakaguzi wa hesabu hawa kupata mafunzo ya kila wakati hawawezi kutekeleza majukumu yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi katika utayarishaji wa vitabu vya uhasibu kwa kuzingatia viwango vya kimataifa kuna mabadiliko kila siku yanajitokeza na mabadiliko haya yana-necessitate kwamba lazima wahasibu wafundishwe kila wakati ili waweze ku-comply na hizo standards. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukaweka mfano, kwa mfano, IPSAS-17 kiwango hiki cha utayarishaji wa hesabu za kimataifa za taasisi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Kwa upande wa Serikali IPSAS-17 inataka mali za Serikali zile za kudumu zifuate taratibu fulani, lakini ukiangalia ukichukua taarifa za taasisi mbalimbali zilizofanya zikiwemo Wizara wameshindwa ku-comply vizuri na hii standard IPSAS-17.
Mheshimiwa Spika, wengine katika ku-calculate depreciation unakuta kwa mfano gari linatakiwa liwe depreciated kwa miaka mitano liwe limekwisha na likiisha linatakiwa liwe na zero, labda kama limebaki linabaki tu carrying value unless wanafanya revaluation. Wao unakuta wana depreciate, wanafika miaka mitano wanaendelea ku-depreciate, mpaka inaenda kwenye negative. Ukichukua taasisi nyingi ukiwauliza kwa nini hii ipo hivi? Wanakwambia ni kwa sababu ya mfumo. Sasa, hatuwezi kusema kwa sababu ya mfumo. Mfumo upo kwa ajili ya kuwasaidia kuweza kuandaa mahesabu, siyo kwa ajili ya kwamba mfumo unawajibika, wewe kazi yako ni kuchambua kile kilichotoka kwenye mfumo uone kama kina-comply na viwango, uweze kurekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ni vizuri muendelee kutoa mafunzo kama ulivyosema kwenye ripoti yako, mtoe mafunzo zaidi kwa wahasibu, hawa wakaguzi waweze kujua na ku-comply na standards hizi za kimataifa ili Tanzania iwe ni mfano katika utayarishaji wa mahesabu. Ninayasema haya kwa sababu mimi mwenyewe ni mtaalam wa hesabu na nimepitia mahesabu yale nimeona namna ambavyo yanakwenda yanavyofanywa vizuri na hii taasisi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo nilitaka kushauri, sasa hivi kutokana na kwamba tuna mifumo mizuri ya kufunga hesabu, ule muda tuliokuwa tunautumia kufunga hesabu baada ya tarehe 30 mwezi Juni mpaka hadi tarehe 30 mwezi Septemba miezi mitatu, ni muda mrefu sana. Tumeshauri kwa muda mrefu kwamba sasa muangalie huu muda upunguzwe, ninajua mmeupunguza lakini bado hamjapunguza kisheria. Kwa hiyo, hebu angalieni ile Sheria ya Fedha, punguzeni ule muda basi wapewe mwezi mmoja au miwili kwa sababu sasa hivi sesabu zinafungwa kwenye mifumo. Basi wafunge ili kusudi CAG aende kuanza kukagua mapema.
Mheshimiwa Spika, ule muda ambao CAG anapewa ule wa miezi sita badala ya miezi sita kuanzia mwezi wa tisa, urudishwe nyuma kusudi ripoti yake ile tuweze kuipata mapema na iweze kujadiliwa na Bunge na uwajibikaji uendelee kuimarika zaidi na hiyo itatufanya tufanye maamuzi kwa wakati na kuhakiksha kwamba kila kitu kinakwenda vizuri.
Kwa hiyo, mimi ninapendekeza mpitie Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu (CAG) ile ya NAO ili tuweze kurekjebisha, tufupishe ule muda. Pia, mpitie Sheria ya Fedha ya mwaka 2001 na marekebisho yake ya mwaka 2020 mpaka sasa hivi, ili kususdi tupunguze muda na uwajibikaji uweze kuimarika. Hilo litasaidia sana kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni hii mifumo; hii mifumo tunaomba ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema ni vizuri sana mifumo iwe inaonana na ni vizuri kwa sababu mifumo yenyewe inagharimu fedha nyingi tunazozitumia katika kuweza kutayarisha hiyo mifumo. Sasa mifumo ile ikionana itaturahisishia sana kuweza kufanya kazi na njia nyingine ambayo itatusaidia sana tunaposema mifumo ni pamoja na ku-manage uchumi wetu, kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anajulikana anafanya nini na tuwe na mfumo wa namna hiyo. Sisi tunasema tukiwa na sera hii jumuishi ikitekelezwa ipasavyo, hali ya uchumi wa nchi yetu itakuwa ni nzuri, tutaweza kusimamia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, financial inclusion ni kitu muhimu mno na bila kuifanya hivyo tutaendelea kuwa na informal sector na hivyo kutakuwa na upotevu mwingi wa mapato sasa hivi yapo nje ya mfumo, lakini pia watu wengi wanakwepa kodi kwa sababu tunatumia hiyo cash system. Tungekuwa wote tupo kwenye mfumo jumuishi wa fedha, ninaamini mambo yangekwenda vizuri na kila kitu kingekwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa mimi niombe kushukuru na nimpongeze tena Waziri, watendaji wote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. Waendelee kuisimamia Serikali, mahesabu na fedha za umma ili kusudi Taifa letu liweze kuendelea. Tuweze kupata fedha za maendeleo, tuweze kuleta maendeleo katika maeneo mbalimbali.
Kwa hiyo, mimi nina uhakika kwamba kila kitu kinakwenda vizuri, uwazi umeiongezeka na uwajibikaji umekuwa vizuri. Hongereni sana na ninaunga mkono hoja. Ninawatakia kila la kheri. (Makofi)