Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususani barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba - Waziri wa Fedha, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”
Mheshimiwa Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Fedha, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, Serikali kupitia Wizara ya Fedha imesimamia kwa ufanisi ukusanyaji mapato na utekelezaji wa miradi mingi ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na kadhalika. Naipongeza Serikali kwa mwendelezo mzuri wa utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa umeme Mto Rufiji, mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. Umeme, reli na bandari ni nguzo imara ya kiushindani katika uchumi wa Tanzania na nchi za maziwa makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki wakati dunia inaendelea kupambana na athari za vita vya Urusi na Ukraine na pia janga la corona virus (covid-19), tumejifunza umuhimu wa kuwepo kwa mikakati mbadala kutokana na nchi nyingi tunazoshirikiana kibiashara na kiuchumi kukumbwa na mtikisiko wa kiuchumi. Katika kipindi cha hivi karibuni, tumeshuhudia wadau wakubwa wa maendelea wakibadili sera zao kiasi cha kuathiri mipango yetu.
Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyoguswa ni pamoja na afya na maeneo mengine ya kibajeti ya maendeleo. Serikali iendelee kujipanga kimkakati kuongeza uwekezaji katika kilimo, madini, uchumi wa bluu, maliasili na utalii ili kuongeza uzalishaji na tija. Serikali kupitia Msajili wa Hazina anapaswa kuendelea kuimarisha mitaji kwa mashirika ambayo yatachochea ukuaji wa uchumi ikiwemo benki za TADB, TCB, TIB na ATCL ili iweze kusimama kibiashara ikiwa ni nguzo muhimu hata kwa sekta zingine. Msajili wa Hazina anapaswa kupewa nguvu zaidi ili asimamie mashirika ya umma ili yaendeshwe kibiashara na kwa tija ya kiushindani kwa hapa nchini na hata nje ya nchi. Kuongezeka kwa tija kwenye mashirika ya kibiashara itapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa mapato ya kikodi na hata mikopo kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea hata kwa kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kugharamia ujenzi huo, kwa vile kutakuwa na fursa kubwa za usafirishaji. Pamoja na ujenzi wa SGR, napendekeza kuendelea na kuboresha reli ya TAZARA na uboreshaji wa bandari zetu ikiwemo ujenzi wa bandari kavu ikiwemo ya Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki ili kupunguza gharama za kusafirisha pembejeo na mazao. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija.
Mheshimiwa Spika, kuna umuhimu mkubwa kuchukua hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu. Usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za usafirishaji mizigo kwa wateja wa bandari kutoka Zambia, DRC, Malawi na hata kwa kupunguza gharama za usafirishaji wa pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Spika, kuna fursa nyingi za muda mfupi za kuongeza mapato kupitia hatua za kiutawala ikiwemo ya kuondokana na matumizi na malipo ambayo hayana tija kwa Serikali na hata walipa kodi. Kutokana na mahitaji makubwa ya uwekezaji kwenye miradi ya kimkakati, uchumi wetu utaendelea kuwa na mahitaji makubwa ya mikopo ya pesa za kigeni na wakati huo huo kulipa mikopo iliyoiva.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha mapato ya fedha za kigeni yanaongezeka kupitia mazao ya kilimo, madini na utalii. Kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni yatasaidia kuimarisha uhimilivu wa Deni la Taifa na pia kuendeleza utulivu wa shilingi yetu dhidi ya sarafu kuu za kigeni na hata kuhakikisha utulivu wa mfumuko wa bei. Serikali ihakikishe kipaumbele cha kuwekeza kwenye kilimo ikiwemo pembejeo na umwagiliaji kwa lengo la kuongeza tija na pia kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kulinda mfumuko wa bei. Serikali inashauriwa kuchukua hatua zaidi za kuimarisha sekta za kilimo, utalii, na madini ili kukabiliana na athari za kiuchumi wa kidunia.
Mheshimiwa Spika, kutokana na athari za kiuchumi uliokumba dunia nzima ikiwemo changamoto za upatikanaji wa fedha za kigeni, hatua za kuimarisha sekta hizo hapo juu, inaweza kuwa fursa kwa Serikali kuvutia uwekezaji zaidi kwenye madini hasa dhahabu, viwanda vya mbolea kutokana uwepo wa mali ghafi za madini ya calcium carbonate, lime na phosphate. Dhahabu ina historia ya bei kutoyumba kwenye soko la dunia kwa vile mabenki yanatumia dhahabu kwenye kuwekeza na kutokana pia na kuyumba kwa thamani ya shilingi na hata dola ya Marekani.
Pia Serikali inaweza kutumia dhahabu kama mbadala wa kuwekeza amana zake. Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi kidunia, Benki Kuu nyingi duniani zimeanza kuwekeza zaidi kwenye dhahabu na hii ni ishara nzuri kwa bei ya dhahabu kuendelea kuimarika kwenye soko la dunia. Serikali ijielekeze kununua dhahabu kwa shilingi toka kwa wachimbaji wadogo na kisha kuzitafutia soko kigeni la moja kwa moja na hatua hii itapunguza na kuzuia uvujaji wa mapato ya fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Benki Kuu kuendelea kununua na kuwekeza kwenye dhahabu, napendekeza hili zoezi lilenge pia kuuza dhahabu wakati bei zinapanda kwenye soko la Dunia. Pia Serikali iweke mkakati wa kusaidia wawekezaji Wazawa kwenye uchenjuaji wa madini ili waweze kukabiliana na ushindani kimataifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Mradi wa Liganga na Mchuchuma, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa. Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo yanapatikana milima ya Pandahill Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) yanaendelea kuwa makubwa duniani na hapa kwetu pia.
Mheshimiwa Spika, Serikali inahitaji kujiwekekea mikakati ya haraka (quick wins) ili kuhakikisha inaimarisha uchumi ikiwemo kuboresha urari wa biashara kukabiliana na athari za changamoto za mabadiliko ya sera za wadau wa maendeleo na hata vita vya Urusi na Ukraine. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi ikiwemo kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ferroniobium utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) na uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa itachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanzo cha fedha ya kigeni.
Mheshimiwa Spika, kutokana na upotevu mkubwa wa fedha za Serikali ikiwemo miradi ya Serikali Kuu na Halmashauri, napendekeza Serikali kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ili kuongeza ufanisi na uhuru wa Wakaguzi wa Ndani. Serikali ihakikishe Mkaguzi wa Ndani wakati wote anakuwa huru kutoka kwa Afisa Masuuli. Wakaguzi wa ndani wa halmashauri wasimamiwe na Mkaguzi Mkuu wa Mkoa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Serikali iimarishe uhuru wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor General) na napongeza Serikali kupandisha hadhi ya Ofisi kuwa na Fungu la Bajeti linalojitegemea.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.