Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii ya kutoa mchango wangu pamoja na tu kuweka nyalio kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakuja kuhitimisha rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu Rahimu, Mungu ambaye kwa uwezo wake ametujaalia kukutana siku ya leo hapa tukiwa katika hali ya uzima na afya na kujadili mambo muhimu na adhimu kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini. Miaka yote hii niko katika sekta hii ya Wizara ya Fedha mimi na Mheshimiwa Waziri wangu. Hii ni imani yake kubwa sana na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais pia kwa namna anavyokuwa na uwezo mkubwa sana wa kutafsiri sera kwa vitendo na kila mmoja wetu anajua kwamba Mheshimiwa Rais ni mahiri sana kwenye kutafsiri sera kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni sera nyingi zilikuwepo kwenye makabati, zilikuwemo kwenye vitabu, leo Mheshimiwa Rais anazitafsiri kwa vitendo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunaomba tumpe maua yake Mheshimwia Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kusema kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa yale mema na makubwa ambayo ameyafanya katika nchi yetu, kila mmoja mwenye macho na asiye macho haambiwi tazama, anayaona mwenyewe na hii tunasema kabisa kwamba Mheshimiwa Rais kwa makubwa yale aliyoyafanya, hata kijana yule basi anaelewa kwamba mama anafanya mambo mazuri na makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili naomba nikushukuru sana wewe na nikupongeze kwa mambo kadhaa. Naomba uniruhusu nitaje matatu; jambo la kwanza, kwa kutambua mchango mkubwa sana wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mkasema hatutotambua kwa kushukuru tu kila mmoja wetu wakati akichangia, aah aah, tunamwita tunampa tuzo yake. Tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili kwa kuwa Rais wa IPU; siyo jambo rahisi, ni jambo kubwa sana. Nafasi ile imepata mtu sahihi na kwa wakati sahihi. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu naomba uniruhusu nimshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu, kwa maelekezo yao kwetu. Tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu pia nimshukuru mentor wangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kwa kweli nimejifunza mengi na namshukuru kwa malezi yake mazuri. Hapa nilipofika leo nimesimama kwa miguu miwili ni kwa sababu ya malezi yake. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru sana Kamati ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Oran Njeza, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wenzangu. Kwa kweli wamefanya kazi nzuri na wanatupa ushirikiano makubwa kwa kila wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano wao makubwa sana. Lile ambalo lilitokea Jumatano kama ya leo wiki iliyopita ni kwa sababu ya dua zenu na sala zenu, nawashukuru sana. Nami niwaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana kwa pamoja. Halafu niwapeni siri; uko usemi usemao zimwi likujualo halikuli likakwisha. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu wote In Shaa Allah mrudi awamu hiyo ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuje tushirikiane katika ujenzi wa Taifa hili, kwa sababu kama ingekuwa inaruhusiwa, kama ipo kwenye utaratibu Waheshimiwa Wabunge hawa walioshuhudia mema na makubwa yaliyofanywa na kwa namna walivyosimamia na wao katika majimbo yao na mikoa yao, basi wangewekwa katika wino maalum wa dhahabu. Majina yao yaandikwe kwa wino maalum wa dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo ni siku ya kuhitimisha na mhitimishaji ni Mheshimiwa Waziri. Nataka niongee tu mambo machache. Waheshimiwa Wabunge wengi wameshauri na wameelekea kwamba tuimarishe ulipaji wa kodi, yaani uimarishaji wa upatikanaji wa mapato. Serikali hili imelipokea na tunaenda kulifanyia kazi na kwa kweli tumeandaa mifumo mingi na tunajitahidi sasa iende kusomana ili kukuza mapato ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na ni kweli walichosema Waheshimiwa Wabunge, kwamba wako baadhi ya watu ambao labda niseme hawaitakii mema nchi yetu au wamekosa uzalendo, ambao wanakwepa kodi kwa makusudi na bahati mbaya wale ambao wanakwepa kodi baadhi ya watu wanawafurahia, wanawaona wanalolifanya ni jambo jema.
Mheshimiwa Spika, hii ndiyo bahati mbaya na tumeelekezwa kabisa na vitabu vyetu vya dini kwamba ukiona uovu, yaani kama mtu anakwepa kodi huo ni uovu. Ukiona uovu, ukiona tendo baya basi liondoe kwa mkono wako, kama huwezi lisemee, angalau sema tu, toa taarifa, lakini ukishindwa basi chukia tu usifurahie, chukia ingawa huo ni udhaifu kidogo unapaswa uliondoe ama ulisemee.
Mheshimiwa Spika, hili Serikali inaahidi itaenda kulifanyia kazi na tutahakikisha kwamba mianya yote ya ukwepaji wa ulipaji kodi imezibwa kwa wakati muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Balozi Subira amesema tuongeze mapato kupitia bandari zetu, Serikali imeimarisha mifumo na tutaendelea kuimarisha na kuifuatilia na kusimamia kabisa kuhakikisha kwamba mifumo inasomana na tumeongeza mapato yetu hasa katika sehemu zetu za bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge, wenzangu wakisema kwamba tuendelee kuimarisha cash economy. Serikali imeshatoa miongozo, imeshatoa maelekezo jambo hili lipo, hatutakiwi tutembee kama alivyosema ndugu yangu, wakati mwingine ni ushamba kabisa kutembea na pochi zile na fedha amesema ndugu yangu. Sio nzuri, kwanza tunaambiwa wallet ukiweka mfukoni kama umeweka upande hivi unaweza ukaumiza mgongo wako, kwa hiyo hatutaki wananchi wetu waende kuumiza migongo kupitia hizo pochi kubwa ambazo wameweka kwenye mifuko yao.
Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, niwaambie kwamba haya tunaenda kuyafanyia kazi na tutaimarisha kuhakikisha kwamba tunatumia cashless katika matumizi yetu ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niseme kwamba tumepokea pongezi ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge, zile za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tumezipokea kwa mikono miwili na niwaambie tu yale mema na mazuri yote ambayo mmeona Wizara ya Fedha imefanya basi Mheshimiwa Rais apewe maua yake kwa sababu yale ni maelekezo yake na kama kuna mapungufu ndani ya Wizara ya Fedha, basi mapungufu hayo ni ya kwetu sisi, yeye hayamuhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru sana familia yangu, watoto wangu, wake zangu nawashukuru sana kwa namna walivyotoa ushirikiano mkubwa lakini nawashukuru sana Wana-Kojani, Wana-Kojani nawashukuru sana na nawaomba sana pamoja Spika hapo nawe piga sala zako nirudi tena katika mjengo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaombe sana wananchi wa Iramba Magharibi, huyu Mheshimiwa Waziri ambaye wametuletea bado tunamuhitaji sana. Niwaombe sana, sana waturejeshee mtu huyu, chonde chonde wasije kufanya masihara na hili, lakini niwaombe na mimi wananchi wa Uyole watuletee Spika wetu. Wananchi wakati huo wa Mbeya Mjini walimchagua Mbunge tu, amekuja amekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameenda kuwa Rais wa Mabunge Ulimwenguni, sio kazi rahisi sana, niwaombe sana waturejeshee Mheshimiwa Spika, tuendelee kujenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache mimi naunga mkono hoja. (Makofi)