Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuhitimisha hoja hii siku ya leo, nikianza na kukushukuru wewe mwenyewe pamoja na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia pamoja na maoni ya Kamati ambayo ni kwa niaba ya Bunge zima, ambayo imefanikisha hotuba ya leo pamoja na maoni haya ambayo tumeyapokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee zaidi niwashukuru na ndugu zangu wananchi wa kutoka Iramba ambao wapo hapa na kama unavyoona tukitumia lugha ya mashujaa, leo kwako hapa ni kama kwetu tu maana yake tuko wengi kweli kweli, tunakushukuru sana kwa nafasi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikijibu hoja kwa ufupi kwa maana ya baadhi ya hoja zingine tutazitolea tamko kwenye hotuba kuu ya Serikali, niseme tu machache; moja tumepokea hoja zote ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa zikiwemo za taarifa nzuri ya Kamati pamoja na michango ambayo Waheshimiwa Wabunge wamechangia na kama ulivyoona michango iliyotolewa na Wabunge ni ya kibunge kweli kweli, ya kizalendo kweli kweili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, una Wabunge makini sana na Watanzania waliyochagua Wabunge hawa ni Wabunge ambao wamefanya kazi nzuri sana, hoja za kizalendo, hoja za kibunge na kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyotangulia kusema pamoja na wachangiaji Watanzania wasisite tena kuwarudisha Wabunge hawa ambao wamefanya kazi nzuri ya kizalendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikianza na hoja moja ambayo amechangia Mheshimiwa Kandege, kwa ukubwa wake; moja tumeipokea Mheshimiwa Kandege, hoja ya utekelezaji wa sheria yetu mpya ya masuala ya matumizi ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni. Tumeipokea na tumeshapata maoni mengi na tumepata maoni mengi pia hata kutoka kwenye sekta na bahati nzuri sana Gavana wa Benki Kuu pamoja na timu yake ya wataalamu yupo hapa lakini si tu kwamba yupo pia ameendelea kufanya vikao na sekta kuweza kuangalia ni jambo gani, ni sehemu gani inahitaji maboresho zaidi kuweza kuona ni sehemu gani inahitaji ufafanuzi na yote hayo tumeyapokea na yale ambayo yanahitaji marekebisho tutafanya na yale ambayo yanahitaji mabadiliko tutafanya na yale ambayo yanahitaji ufafanuzi kupitia Bunge lako Tukufu tutaendelea kuyafanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, nikumbushe tu kwamba kwa nini tulichukua hatua hizo, nchi karibu zote za Afrika na duniani tulipita kati ka kipindi ambacho kilikuwa kigumu sana cha upatikanaji wa fedha za kigeni na Bunge lako Tukufu litakumbuka. Kuna wakati nchi zinazotumia bandari yetu zilikuwa na mizigo inakaa bandarini mpaka siku 30, siku 40 mpaka siku 60 kwa sababu hawana fedha ya kigeni ya kutoa mafuta yao, ilikuwepo inakuwa pale bandarini.
Mheshimiwa Spika, si hivyo tu hata sisi pia tulikuwa tunapata uhaba huo pamoja na kwamba tulikuwa vizuri kuliko nchi nyingi za Afrika, lakini hata sisi Waheshimiwa Wabunge watakumbuka tulikuwa tunapata shida hiyo. Shida ambayo ilikuwa inatishia upatikanaji wa bidhaa za muhimu ambazo hazipatikani ndani ya nchi, mfano uagizaji wa mafuta, mafuta ya kula, pharmaceuticals ambazo zinatoka nje pamoja na bidhaa zingine ambazo ni za sekta binafsi kabisa za masuala ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa inatokana na nini? Pressure ya uhitaji wa dola ulikuwa mkubwa sana, sasa hivi pameimarika imarika tunaweza tukapata uhuru huo wa kulegeza legeza lakini kwa wakati huo kwa sababu kulikuwepo na utofauti wa uhitaji wa bidhaa ilikuwa ni busara Serikali lazima ichukue hatua na katika kuchukua hatua iweze kupata shuruhisho la tatizo ambalo lilikuwa kubwa. Sisi tumetangulia, nchi nyingine bado hawajaimarika kama sisi ambavyo tumeimarika. Kuna nchi bado wanashida kubwa hiyo ya kuweza hata kupata bidhaa muhimu kama mafuta, zipo nchi ambazo bado wanapata shida na kinachosababisha hasa washindwe kupata mafuta si kwamba mafuta hayapatikani kule yanakotakiwa kutoka, wanakosa fedha ya kigeni ya kuweza kulipia mafuta hayo, wapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zipo nchi nyingine zinashindwa kuchangia michango yao ya kimataifa, wana-default kwa sababu wanakosa fedha ya kigeni. Sisi tumepiga hiyo hatua, lakini tulichukua hatua kuna sehemu tuliweza kubana zaidi, kuna sehemu tuliweza kutokuelewana vizuri tu katika namna tuna maanisha nini kisheria, lakini angalau hivi tunavyoongea lile lililokuwa tatizo kubwa la kiwango hicho la upatikanaji wa fedha za kigeni halipo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo yale yapo ambayo kiukweli yalikuwa yanatakiwa tuchukue hatua kama hizo, kwa mfano, natoa mfano, kwa mfano taasisi ya Serikali inayotoa leseni kwa mwananchi, kwa nini imtake mwananchi ambaye fedha yake ya nchi ni shilingi ya Kitanzania, kwa nini imtake mwananchi apeleke dola kupewa leseni ya kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani hili ni jambo ambalo Serikali na Idara zake za Serikali inapotoa huduma kwa Mtanzania kwa kweli inatakiwa isimsumbue Mtanzania kwenda kutafuta dola na wakati ule ilikuwa haipo, inamtaka akalete dola katika mazingira ambayo hata Serikali inatambua kuna uhaba wa dola.
Kwa hiyo, tulisema baadhi ya maeneo kama hayo ambayo Serikali ndio inatoa huduma na inatoa huduma kwa Mtanzania tuliona tuondoe hilo sharti la kutaka alete dola, kwa hiyo, hilo tuliona tuliweke kwa namna hiyo na nadhani kwenye hilo hatujapata usumbufu na wala hatujapata malalamiko kutoka kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna eneo lingine ambalo lilikuwa linahusisha masuala ya ada za shule, masuala ya nyumba na kuna maeneo mengine hata mahitaji ya watu wanafanyiana biashara kiwanja wakawa wanaweka sharti hilo kwamba walipane kwa dola. Hiyo tuliona inakiuka sheria na inawafanya wananchi wetu wapate shida ya kutafuta dola wakati fedha yao halali ya kikatiba, ya kisheria ni shilingi ya Kitanzania. Kwa hiyo hilo tuliona likae kwa namna hiyo, lakini yapo maeneo ambayo tumeona, ambayo Gavana wa Benki Kuu anaendelea kushauriana na wataalam pamoja na sekta husika. Yapo maeneo ambayo yanahusisha biashara kubwa kubwa zile za kimataifa, tumesema hata hivyo katika baadhi ya maeneo ilikuwa ni tafsiri tu kwamba kwa biashara ile ya kimataifa inayovuka mipaka ambayo inahusisha masuala mengine ya kimataifa ilikuwa ni tafsiri tu ilikuwa haihusishi kwamba na wao wanatakiwa wapate sharti hilo la shilingi.
Mheshimiwa Spika, ile ilikuwa imetajwa, ilikuwa imejumuishwa kwa ukubwa wa sheria ambapo kusudi lake lilikuwa sio hilo na kama bado kuna tafsiri itakuwa bado inaleta ukakasi tumekubaliana na wataalam wa Wizara ya Fedha pamoja na taasisi zetu ikiwemo Benki Kuu kuweza kuona maeneo yale ambayo yalikuwa yanapotoka kwa utaratibu wa tafsiri yake tuweze kuyanyoosha ili kusudi lililokuwa limekusudiwa liweze kufikiwa, lakini tumekaa pia na taasisi zinazofanya shughuli kubwa hizo, Wizara ya Nishati, The Light ya TANESCO, TPDC na maeneo mengine ambayo wanafanya shughuli kubwa ikiwemo na miradi mikubwa kama bomba la mafuta pamoja na maeneo mengine, tuweze kuona matatizo yanayojitokeza ili tuweze kurekebisha.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ilikuwa njema ya kuondoa pressure ile ambayo na kwa kweli leo hii tumeona imejitokeza kwamba tatizo lile la ukosefu wa fedha za kigeni tumelivuka na tunaamini kwamba tutaweza kurekebisha. Kilichokuwa kinatokea na hata sasa tunaendelea kusisitiza katika baadhi ya maeneo, kama taasisi ya nje inafanya shughuli zake mathalani inauza bidhaa zake nje na inapata dola, ikija kulipa dola kwenye taasisi zetu ama kwa wananchi wetu bado dola inakuja na inatusaidia kupata dola. Kwa ukubwa ule mathalani wameuza kama ni dhahabu, wameuza kama ni…, taja bidhaa yoyote wameuza nje wakapata dola kama wanakuja kuilipa taasisi kwa dola hizo haitengenezi pressure yoyote ndani ya uchumi wetu, lakini kama wanataka wakalipe dola kwa viwango vikubwa vikubwa, lakini na wao kumbe dola hizo wanatarajia wazipate ndani ya nchi pale ndio tatizo linapoanzia kwamba yule aliye mkubwa ataenda kukusanya dola kote na wale walio wadogo watakosa hata za kufanya hivi vishughuli vidogo vidogo.
Mheshimiwa Spika, tulifika wakati wafanyabiashara wetu walikuwa wanapata shida sana kwamba mtu anazunguka kwenye benki anapewa dola 500 yaani hata anahitaji dola 6000, dola 7000 anaenda kwenye benki anakusanya anapewa dola mia tano, mia tano. Mzigo wake umeshafika bandarini au mzigo wake umeshakuwa tayari au ameshaishiwa mzigo mwingine anataka aagize mizigo mingine, ilikuwa ni shida na ilikuwa inashusha kasi ya kukua kwa uchumi.
Kwa hiyo, tumelipokea kwa sababu sheria ilikuwa mwaka jana na sasa hivi tuna fursa ya sheria pale ambapo panahitaji maboresho ili twende vizuri zaidi tumepokea na tutaboresha na pale ambapo hapana malalamiko na panaenda sambamba na sheria tutaendelea kutoa elimu kama jambo lilikuwa ni suala la uelewa.
Mheshimiwa Spika, amelisemea vizuri ndugu yangu Kasalali na Wabunge wengine waliyoongea kuhusu jambo la masuala haya ya kodi. Ni kweli bado pana shida ya uelewa na uunganishaji kwamba maendeleo yetu ni kodi zetu, kila jambo tunaloliona la maendeleo ni kodi zetu. Zamani ambazo zilishapita, kwenye bajeti zetu kulikuwa na fedha zinaitwa fedha za misaada za kibajeti.
Mheshimiwa Spika, wakati ule ulishapita haupo tena, kwa sasa hivi kila kitu tunachokiona cha maendeleo, kuanzia miradi mikubwa hadi ile miradi ya huduma za jamii pamoja na maeneo mengine yote ni fedha za kodi zetu na kuna mwingine atasema sasa kama ni kodi zetu mbona bado huwa mnakopa? Hata ukikopa utalipa deni kwa kodi zetu, kukopa ni kuyaleta mapato yako yote karibu ili utekeleze mradi, halafu uanze kurejesha kwa kipato chako cha muda mdogo mdogo cha mwezi mmoja moja na hili jambo si jambo geni hata katika maisha yetu ya kawaida huwa yapo kwamba mtu yeyote ambaye analipwa mshahara yule anayepitisha mshahara wake kama ni benki anampitishia mapato yake kwa mara moja ili afanye jambo moja kubwa halafu mapato yake yale anayoyapata aanze kurejesha kidogo kidogo. Huu ni utaratibu ambao upo hata kwenye maisha ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata Wabunge huwa wanatumia utaratibu huo, anapata mapato yake, halafu anafanyia jambo lake kubwa la maendeleo, anachangia vituo vya afya, anachangia ujenzi wa madarasa, anaunga mkono pale ambapo wananchi wamejitolea, halafu mapato yake yeye anaanza kuwa pakame, yale mapato yake anaanza kurejesha kidogo kidogo kila mapato. Huu ni utaratibu wa kawaida na wala si jambo la kutisha wala watu wasitishike, kubwa tu ni kwamba bajeti ya Serikali inazingatiwa, Serikali haikopi zaidi ya ilichopitishiwa na Bunge lake Tukufu na vilevile haikopi kwenda kupeleka kwenye matumizi yasiyo ya maendeleo, mnakusanya unapeleka kwenye miradi iliyo ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba mradi amabo unaweza kuujenga kwa miaka mitano kwa kuchukua fedha kubwa mathalani dola bilioni tatu kama wa reli ya kisa ungeamua kuujenga kwa cash budget kwa makusanyo ya kila mwezi ungejenga kwa miaka 40. Sasa kiuchumi unasema nenda kachukue mkopo ambao utaulipa kwa miaka 40 ujenge kwa miaka mitano wananchi waanze kupata huduma halafu hiyo miaka 40 ambayo ndio ulitakiwa ujenge mradi kwa miaka 40 utatumia tu kufanya marejesho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiki tunachokisema ndicho ambacho Serikali ya Tanzania inafanya, kwenye Deni la Taifa la Tanzania 67% ni mikopo ya multilaterals, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, IMF, mikopo ambayo kipindi chake cha kurejesha ni miaka 30 mpaka 35 mpaka 40 ndio maana nikiwa Waziri hapa nimeshuhudia ulipwaji wa mikopo ya Serikali ya Awamu ya Kwanza, Serikali ya Awamu ya Pili, ni mikopo ya muda mrefu, kwamba mradi ambao ulianzishwa na Serikali ya awamu ya kwanza tungeamua kulipa kwa mapato ya mwezi ndio ingetakiwa sasa hivi mradi mmoja uwe unamalizika leo, kwa hiyo inamalizwa kwa mara moja, lakini inabaki deni inalipwa kidogo kidogo kwa sababu mapato tuliyakusanya hivi.
Mheshimiwa Spika, asilimia tano ni mikopo ya nchi kwa nchi ambayo na yenyewe ni kama ile ile ya multilaterals ambayo ni midogo. Kwa zaidi ya 72% ya deni la Taifa ni ile mikopo ya muda mrefu ambayo riba yake ni ya chini takribani 23% mpaka 24% ndio ile ambayo inaangukia kwenye mikopo ya kibiashara na yenyewe ni kwenye maeneo mahususi sana.
Kwa hiyo, niliona nilisemee na hili kwamba ni jambo ambalo ni la msingi sana la kusisitiza mapato na wakati Mheshimiwa Kasalali, anaongea nikasema kule jimboni kwako kama kura zinapungua pungua kwa sababu wapiga kura wangu wapo hapa na wamenihakikishia nikatamani kama inawezekana kugawia tukugawie kidogo ili urudi utoe hoja za msingi hizo za kibunge na za kizalendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wameongea na Waheshimiwa Wabunge wengine kama nilivyosema pamoja na Mheshimiwa Kingu, ambaye kaongea vizuri sana tumepokea hoja hizo; Mheshimiwa Hasunga kaongea vizuri sana tumepokea hizo hoja; Mheshimiwa Balozi wetu Mheshimiwa Subira kaongea vizuri sana tumepokea hoja hizo; Mheshimiwa Kandege ndio nilikuwa nafafanua tumepokea hizo hoja tutazifanyia kazi; pamoja na Balozi wetu aliyechangia mwanzoni pale mama Mheshimiwa Riziki Lulida, my best umechangia vizuri hoja zako tumezipokea na hili ambalo alikuwa analimalizia Mheshimiwa Kingu, la ndugu yetu Mtanzania na shughuli anayofanya tumelipokea na tutateta vizuri tuone ni kitu gani ambacho kinaweza kikafanyika, tutashukiriana na sekta pamoja na Foreign Affairs tuone ni kitu gani kinachotakiwa kufanyika ili tuweze kufanikisha jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeona kengele ya kwanza imeshagongwa nitumie fursa hii tena kuwashukuru Wabunge wote tumepokea hoja zenu, nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Hamad, MCC - Mjumbe wa Kamati Kuu nakupongeza sana. Mheshimiwa Naibu Waziri ni Naibu Waziri wa viwango vya Wizara ya Fedha, Naibu Waziri wa viwango vya Hazina. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri huyu amejaliwa hekima sana, amejaliwa ushirikishaji mzuri sana na Mheshimiwa Naibu Waziri mara zote hata ninapokuwa kwenye vikao vile vya lazima ambavyo kuna wakati nalazimika kuwa kwenye vikao vile hata wakati Bunge linaendelea ama Kamati zinaendelea huwanakuta ameweza kushirikiana vizuri na Kamati na ndiyo maana kwa kweli hata mara zote hata nisipokuwepo ni kama nipo tu kwa sababu Naibu Waziri anafanya kazi nzuri na tuwaombe wapiga kura wa Kojani waturudishie Naibu Waziri wetu, kazi anaiweza na anaifanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kama walivyosema wengine, ili nisimtaje Mbunge mmoja mmoja kuwaomba wananchi wake waturudishie, nitumie tu fursa hii kuwaomba wananchi wa Uyole wakurudishe na Wabunge wako wote ili kuweza kumalizia hii kazi ambayo iliyokuwa inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wamefanyaka kazi nzuri Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, Wana-Uyole waturudishie Spika wetu, waturudishie dada yetu anafanya kazi nzuri na wawarudishe Wabunge wote ambao kwa kweli wameshiriki kwenye shughuli hizi zote ambazo rekodi za maendeleo ambazo zimekuwa recorded katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, naomba sasa kutoa hoja.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naafiki.