Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza kabisa kwenye Wizara hii muhimu katika kuleta furaha, amani, upendo na mshikamano wa Taifa letu. Kabla sijaweka mchango wangu nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi makubwa aliyoyafanya katika Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tutakuwa mashahidi kwamba ni katika kipindi cha miaka michache tu (miaka mitatu, minne) nchi yetu sasa imekuwa na identity (utambulisho). Nchi yetu sasa inafahamika kwa namna ilivyo; kwa nini? Kwa sababu ya mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Michezo na mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Sanaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukisikiliza nyimbo zinazopigwa hapa Tanzania, ukiangalia maigizo na filamu zinazofanyika Tanzania ni tofauti kabisa kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuweka fedha, kuunga mkono shughuli zinazofanywa na wasanii na wanamichezo nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu. Nimekuwa kwenye hii sekta tangu nimeingia kwenye Bunge hili huu ni mwaka wa tano. Kila bajeti ambayo imeletwa mbele ya Kamati yetu tumeona namna ambavyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiongeza fedha mwaka hadi mwaka kuhakikisha kwamba anawaunga mkono Wasanii na Wanamichezo na mwisho wa siku tunakwenda katika ile Tanzania tunayoitamani kuiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea ninaomba niseme jambo moja. Mheshimiwa Waziri, Profesa Kabudi wakati ameteuliwa kuwa Waziri (na yeye huwa analisema kwenye majukwaa lakini na hapa nirudie). Wakati ameteuliwa kuwa Waziri mimi binafsi niliamini ni mtu ambaye anatumika zaidi kwenye hard power sikutegemea kama ni mzuri kiasi hiki kwenye soft power. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninataka nikiri mbele ya Bunge lako Tukufu kwa muda ambao tumefanyakazi na Mheshimiwa Profesa Kabudi tumeona kwamba kweli Mheshimiwa Profesa Kabudi ana-fit kwenye hard power na soft power. Tunampongeza sana na tunamtakia utekelezaji mzuri sana wa majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu na kaka yangu Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Mwinjuma maarufu kwa jina la Mwana FA. Waheshimiwa Wabunge, ninadhani wanafahamu tupo pamoja kwenye hii nchi siku zote, wameshakuwepo Naibu Mawaziri wa Michezo kadha wa kadha kwenye nchi hii lakini Mwana FA yupo peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hayo kwa sababu gani? Mwana FA siyo tu kwamba ni mtumishi, ni msomi, ni Mbunge lakini ni mwanamichezo kindakindaki. Tumemuona akiahangaika na sekta ya michezo kila uchao siyo Simba au Yanga, siyo Taifa Stars au Twiga Stars. Kila sehemu tunamwona Naibu Waziri anahangaika kutafuta matokeo kwenye sekta aliyopewa kuisimamia. Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mwana FA, kazi yake ni nzuri na sisi tuliopo nyuma yake tunakuunga mkono na tunaona namna gani ambavyo tunaweza tukafaidi katika Sekta hii ya Michezo kwa miaka ijayo, kama utaendelea kuwa katika dawati hilo. Tunakupongeza na tunakutakia kila la heri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefanya kazi na hii sekta na sasa ninafanya nayo kama Mwenyekiti. Hii Wizara kipindi cha nyuma wengi walikuwa wanaamini ni mlango wa kutokea, yaani ukipelekwa kwenye Wizara ya Michezo baada ya muda kidogo kazi yako imekwisha, lakini ninataka nikuhakikishie kwa timu ya wataalam Wakuu wa Taasisi waliopo kwenye sekta hii ya michezo kwa sasa, hakika sasa umekuwa mlango wa kuingilia na siyo mlango wa kutoka tena. Kazi inayofanyika tunaiona kwa macho tukilinganisha na miaka ya nyuma, tunaona matokeo ya wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapatia mifano, leo Tanzania katika mwaka mmoja tu wa utekelezaji wa bajeti tumeanza ujenzi wa viwanja vitatu vikubwa, jambo ambalo halikuwahi kutokea. Tumejenga Uwanja wa Benjamin Mkapa years and years huko nyuma lakini leo Dkt. Samia Suluhu Hassan anapeleka fedha billions of moneys. Kiwanja cha Arusha peke yake zaidi ya bilioni 200, ukarabati wa Benjamin Mkapa zaidi ya bilioni 35. Ujenzi wa Uwanja wa Dodoma peke yake zaidi ya bilioni 300. Hii inadhihirisha kwamba, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kwa dhati kuwekeza kwenye michezo kuhakikisha kwamba Tanzania inapata identity. Tunakwenda kutambulika kama Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumeshuhudia michuano ya indoor football iliyochezwa na timu za mabinti Afrika kwa ajili ya kufuzu kwenda kwenye Michuano ya Kimataifa ya Kidunia. Timu yetu ambayo imepata kufanya mazoezi kwa mwezi mmoja tu, imekwenda mpaka hatua ya fainali na ilikuwa chupuchupu wangechukua kombe. Hii, maana yake ni kwamba tunapiga hatua kubwa sana kwenye Sekta ya Michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya hayo yote kupiga hatua kubwa kwenye michezo, sanaa, filamu na kila eneo maana yake ni kwamba, tunakuwa na Taifa lenye furaha. Leo asubuhi mmeona wenyewe wakati wametambulishwa hapa viongozi wa vilabu, soka na TFF makofi yalikuwa mengi. Hii inadhihirisha kwamba Tanzania tunapenda michezo na kuwekeza kwenye michezo siyo jambo la kawaida kwa sasa ni jambo la msingi na lazima liwekewe dhati katika bajeti, mipango na uendelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme jambo moja. Tanzania ni nchi ambayo ina amani. Amani iliyopo imejengwa kwa muda mrefu, lakini inalindwa kwa namna nyingi. Moja ya eneo muhimu ambalo linailinda amani yetu ni kuendeleza na kuwekeza kwenye michezo. Watu wakiwa na nafasi ya kucheza, kufurahi na kuburudika wanapata fursa ya kupunguza stress, msongo wa mawazo na mwisho wa siku tunakuwa na Taifa lenye furaha hatimaye tunakuwa tunaendeleza amani na mshikamano uliopo katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa kunipatia fursa, lakini ninataka nikuhakikishie kwamba, kazi ambayo ameifanya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miaka mitatu ambayo tumeishuhudia kwa macho haijapata kutokea. Tupitishe bajeti, kazi hiyo ikaendelezwe na mwisho wa siku tuweze kufika katika Tanzania yenye utambulisho wake ndani ya dunia yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)