Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, vilevile tumpongeze Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira ya dhati anayoionesha kupenda michezo nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo niendelee kumpongeza Baba yangu Mheshimiwa Waziri Kabudi, watoto wa Mjini tunasema homeboy, sasa hivi singeli anacheza na kukesha anakesha kama CNN. Kwa hiyo, alhamdulillah wanasema ukienda Chile fanana na Watu wa Chile, hongora sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninapenda kumpongeza ndugu yangu huyu ni msanii wangu niliachiwa anaitwa Mwana FA, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma. Hii Wizara ina Naibu Waziri anapambana kwa ajili ya sanaa pia. Tumeona mfano wa ile Samia Festival ya juzi, Jukwaa la Kimataifa na kila kitu kimekaa vizuri. Hatuna cha kusema zaidi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuenda kuibadilisha hii Wizara ya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vilevile mtani wangu ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo na pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, hongera sana na tunaona, tulisimama hapa na Kamati tukipambana bajeti ipande, leo hii tukizungumzia Wizara ya Michezo unaona Wizara bora kabisa na hata bajeti imepanda, imesimama. Tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, piga makofi kwa Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye soka. Mimi ni mpenzi wa mpira wa miguu, hata wakati Naibu Spika anatambulisha Viongozi wa Simba na Yanga pale, kilichoonekana Wabunge wanapenda soka. Kinachoendelea kwenye soka la nyumbani, kwanza niipongeze TFF kwa ujumla wake kwa kile wanachokifanya kwenye soka letu la Afrika Mashariki nzima, sisi tunaongoa Tanzania. Ninaipongeza pia Bodi ya Ligi Tanzania tunafanya vizuri na tunakwenda ku-compete na timu kama za Morocco na wapi huko tunaonekana tuna klabu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tuwe wawazi wote hapa, Simba na Yanga haiwezi kufungwa na timu yoyote ya nchi hii kuna nini? Wanasema ‘yamshillajabar illa jarda’ punda haendi bila bakora. Viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi waache kudekeza Simba na Yanga. Acheni kutengeneza utaratibu ambao tunaona kabisa kama hawa wanabebwa wengine hawabebwi, waache! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wawazi, mimi ni Simba, tunaona juzi wenzetu walikuwa wanacheza pale Zanzibar, wakiwa hawachezi hapa utasikia Yanga kampiga mtu tano na Simba kampiga mtu saba. Wakitoka nje ya hapa, jini katoka mganga hoi. Yaani wanashinda kwa shida, kuna siasa mnafanya kwenye mpira, siyo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ligi ya Italy imepoteza heshima yake kwa sababu ya hiki ambacho leo hii tunakileta Tanzania. Hiki tunachokileta…
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza kumshukuru mchangiaji kwa mchango mzuri anaouchangia. Ninaomba nimpatie taarifa kwamba hili alilolisema ni muhimu sana na ndiyo sababu timu ya Taifa ya Tanzania Bara ina muda mrefu sana imeshindwa kuifunga timu ya Taifa ya Zanzibar. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Taletale, unaipokea taarifa?
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nilikuwa nawaza dakika saba ulizonipa ni ndogo. Tuongee ukweli, hakuna watu wanafanya vizuri wameikuza na kuiheshimisha ligi yetu kama Viongozi wa Bodi wa Ligi ya sasa. Hakuna watu wameweza kukuza mpira wa nchi hii kama Kiongozi wa TFF, Brother yangu Karia hongera sana, lakini pole kwa kumpoteza mama yako, lakini leo hii fuateni sheria, haina huruma. Mtu anakurupuka amevaa tai yake hatuchezi khaa! Viongozi wanajua sheria, wasimamie sheria, ndiyo itakayotubeba, kama wanashindwa kufuata sheria tunakwenda kuua soka ambalo watu wote humu ndani tunapenda mpira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya nirudi kwenye mchezo wa ngumi. Ninapotokea starehe yetu kubwa ni mchezo wa ngumi. Vijana wangu wa pale kwenye Kata ya Kiloka niliwapelekea gloves na kadhalika nikijua ngumi sasa hivi ni biashara. Ametoka muungwana mmoja huko alipotoka amekwenda kuishtaki Azam badala yake leo hii ngumi hazichezwi, hakuna ngumi. Ametoka tu kijana mmoja anatokea Tanga anaitwa Mafia ameandaa vijana wake, wanaenda kimungumungu ili wafike, leo hii hakuna mchezo wa ngumi. Kwenye hili Mheshimiwa Waziri ninaondoka na shilingi yako kama hatokuja na utaratibu wa kutuambia, vijana wetu wanaocheza ngumi hatima yao ipo wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amempa Waziri kitengo cha habari ana TBC, one of the biggest media kwetu Tanzania aweke nguvu pale basi au atuambie huyu muungwana ambaye leo hii ameweza kuzuia michezo ya ngumi isichezwe, mimi nina mpiganaji wangu bora pale Morogoro Ndugu Twaha Kiduku ana-struggle leo hii, Azam wamefunga milango, sasa tujiulize wale vijana wanakwenda wapi? Wanataka kuongeza wakabaji mtaani? Kwa nini tunashindwa kuwasaidia hawa watu? Hili ni jukumu la nani kama siyo Wizara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitakuwa kipaumbele kwa kushika shilingi kama Mheshimiwa Waziri au Ndugu yangu Mwana FA hajaja na kauli ya nini hatma ya wacheza ngumi nchini tutaiona. Tusimuachie Mafia peke yake hatoweza tutamuumiza yule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, Mheshimiwa Waziri hapa amezungumza kuhusu Mfuko wa Wasanii, ninamwona pale mwanangu Barnaba, hongera baba. Mfuko wa Sanaa, huu Mfuko Mheshimiwa Rais ameleta fedha kwa wasanii hawa, lakini Wizara wameibadilisha hii fedha wameipeleka benki, inadaiwa benki. Kwa hiyo, tukienda kukopa mkopo una sura ya kibenki, yale maono ya Mheshimiwa Rais siyo tena hayo, maono hayo ni ya kwao wao. Wizara warudishe maono ya Mheshimiwa Rais, anataka wasanii wafaidike, wao wametoa hizo hela wamezirudisha benki, wasanii wakienda kukopa mpaka wawe na nyumba, wana nyumba wale, wamewapa nyumba tangu lini? Hamna msanii mwenye nyumba hapa. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Taletale tafadhali. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)