Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuchangia katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia fursa hii. Pia, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wizara hii. Amekuwa karibu sana na wanahabari, wanautamaduni na wanamichezo kwa ujumla wao, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizo ziende sambamba kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake, wamefanya kazi nzuri sana na ninaona hii Wizara ipo ndani ya damu. Siyo mara moja ama mara mbili Mheshimiwa Waziri nimeona akirekebisha lugha kwamba tutumie hivi badala ya hivi. Pia, Naibu Waziri nimemuona siyo mara moja wala mara mbili akipiga mistari kutusherehesha, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni katika sehemu ya sanaa au utamaduni. Kuna makusanyo yanayoingia kutoka kwenye kanda tupu (blank tape levy). Hizi fedha huwa zinapelekwa COSOTA kwa ajili ya sekta mbalimbali za sanaa na maendeleo ya wasanii. Wanufaika hadi sasa inaonekana ni sanaa za maonesho, watu wa filamu na watu wa muziki, lakini sijaona mpaka sasa hivi sanaa za ufundi wanafaidika vipi na fedha zile. Kwa hiyo, ni vizuri watuambie sanaa za ufundi na wao wananufaika vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tunaingia katika michuano ya AFCON hapa nchini, ningependa pia kujua BASATA mmejipangaje kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wabunifu kama wachoraji, wafinyanzi na watengeneza viungo kama vile Zanzibar spices, watengeneza mapambo ili waweze kuonesha na kuuza bidhaa zao kwa kutangaza nchi na pia kujipatia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiria kwamba katika kipindi hiki basi ni vizuri wakae nao wawape mbinu, michakato ya kufanya pia wawaandalie hata lugha rahisi za biashara, kwa sababu wanaokuja siyo wote wanaojua Kiswahili. Sasa, wawaandalie angalau mafunzo mafupi kwa ajili ya lugha za baisahara na wawaandalie wakalimani. AFCON inayokuja wajasiriamali wabunifu wanataka wafanye biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine la usajili wa wasanii. BASATA wanakusanya ada na kodi nyingi kuliko TRA. Msanii binafsi akiimba mwenyewe peke yake anaenda kuambiwa hilo ni kosa la jinai lazima akajisajili. Huko kwenye kujisajili anaambiwa alipe fedha, msanii mchanga hela anatoa wapi? Kuna tozo wanatoa, tozo hiyo hiyo yule msanii ambaye ameshakua wanamweka sawa na msanii mchanga, sasa hawa wachanga watakua lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna malipo ambayo wanayafanya mtu anasema kuna tamasha langu nitafanya nchi nzima, BASATA ndiyo wanajua nchi nzima ina mikoa mingapi, lakini akija Dar es Salaam akilipa akienda Mwanza anaanza utaratibu mpya, akienda Mbeya mwingine akienda Mtwara mwingine, akienda Zanzibar pia, msanii huyo huyo fedha yake mpaka waichukue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi sijajua BASATA walishawasaidia nini wasanii. Wasanii wana makosa mbalimbali wameyafanya sijasikia BASATA wanatoa Mwanasheria wa kwenda kumsaidia msaniii. Pia, BASATA haohao sijaona msanii katengeneza nyimbo yake anataka kurekodi hana fedha, wakasema sisi tumepitia nyimbo yako, tumeipenda, tunakupa hizi nenda karekodi, sijaona, lakini fedha zao wanakusanya! Wakija hapa watuambie kitu gani ambacho wanawasaidia wasanii siyo tu kukusanya ada na fedha zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanawafungia wasaniii bila hata kuwahoji, kwa sababu wanawaacha wanaingia gharama kubwa, wanatengeneza video zao tayari wanamaliza, ikitoka wananchi tumeshapenda wimbo tunataka kurukaruka, tunaambiwa imefungiwa. Halafu yule mwenyewe hawamwiti wakamwambia wamemfungia kwa sababu zipi na hawampi nafasi ya kujieleza, pia hawaangalii gharama alizotumia kutengeneza hizo video. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilipenda kuzungumzia suala la Vazi la Taifa na Mdundo wa Taifa, linakera. Zaidi ya miaka 10 tunazungumza hayo hayo, kwa hiyo hata sasa hivi tukiongea ni kama vile tunampigia gitaa mbuzi. Ninaomba kabla ya hiyo shilingi sijafanya kampeni ya kumnyang’anya basi atakapokuja atupatie jibu la Vazi la Taifa na Mdundo wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilitaka nizungumzie kuhusu Tuzo ya Kalamu ya Mama Samia. Nichukue nafasi hii kuwapongeza waandaji wote TAMWA na TCRA. Hapa tumepata funzo kubwa sana na ndiyo maana siku zote ninasema mama akifanya kitu basi kafanya kwa wote. TAMWA ni Waandishi wa Habari Wanawake, lakini tumeona tuzo wamepewa mpaka wanaume. Hongereni sana TAMWA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TCRA nao wameshiriki wameonesha jinsi gani kwamba hizi Taasisi za Serikali zinashuka kwa wananchi na hawa wananchi wanajua kwamba wapo pamoja na wao. Nishukuru Wizara zote zilizotoa ahadi, ninaomba ahadi hizi zikatekelezwe maana nyingi zimeongewa hapa tumezisikia. Kubwa zaidi katika mwono wangu, katika zile zawadi sijaona watu wa picha za video na kwenye magazeti na nini, kwa sababu zile nazo pia ni habari. Mtoto mdogo hajui kusoma, hajui kuandika, lakini akitazama picha anakwambia huyu ni Mama Samia. Waangalie na wao jinsi gani watu wa picha za video nao wanaweza kuwapa tuzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, ninaomba hawa BASATA wakae na wasanii wao. Wasanii ni kioo cha jamii, tunakaa tunawaangalia, tuna wapenzi wao, tuna rafiki zao ambao tunapenda kuwafuatilia. Kinapofika kipindi wasanii wanaanza kugombana, kudhalilishana, kutukanana, kukashifiana, pale hawataki umaarufu, ule siyo umaarufu, umaarufu hauji kwa hivyo. Wafanye kazi, sisi tutawapa umaarufu, tunajua umaarufu wao; hawana sababu ya kutukanana. BASATA wakae nao wawaeleze mafunzo mbalimbali ya uelewa juu ya mila, desturi, tamaduni, malezi na makuzi ya Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwa haipendezi mtu binafsi na demu wake wanaachana wenyewe, matangazo yanakuja huku. Unamzibia mwenzio riziki asiolewe tena, jamani au asioe tena! Siyo vizuri. BASATA semeni nao wasanii wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme kwamba, kwa kuwa, Wizara imejipanga vizuri kwa bajeti hii ya mwaka wa fedha 2025/2026. Nimeiangalia mikakati waliyoiweka; na kwa kuwa, Mawaziri ninyi ni wasikivu na waelewa na wako tayari kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kazi zake kuhusu Wizara hii, niko tayari kuunga mkono hoja. Ninaunga mkono kwa asilimia mia moja. Ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)