Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa hii nafasi asubuhi ya leo. Kwanza kabisa ninachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyosaidia na kuhakikisha Wizara hii inafanya kazi zake kwa sekta zote, ikiwemo michezo, utamaduni, sanaa, pamoja na Lugha yetu ya Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zake anazofanya katika kuhakikisha Wizara yake inafanikiwa kwa asilimia kubwa, ikiwemo kuwa mtetezi mkubwa wa Lugha ya Kiswahili. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, hapa upele umepata mkunaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wasaidizi wote katika Wizara hii. Wanafanya kazi sambamba kuhakikisha Wizara yao inafanikiwa katika sekta zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu, ninapenda pia, kuwapongeza Wizara wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri katika kuhakikisha kwamba, ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unakuwa wa pamoja katika ushirikishwaji wa masuala yote ya kupeana elimu, uzoefu na kujengeana uwezo. Tunawashukuru na tunawaomba waendelee kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana kwa makongamano yanayofanyika ya Kimataifa na Kitaifa katika kukuza utamaduni wetu na kuueneza, pamoja na kueneza Kiswahili duniani. Pamoja na hilo, ninapenda kuongezea kwamba, katika kuhakikisha tunaeneza utamaduni wetu tutumie sana ngoma zetu za asili na vionjo vyetu vya asili. Kama Zanzibar kule Taarabu Asilia ndiyo inatakiwa itangazwe na siyo hii Taarabu ya sasa hivi. Ninaona hapo nimeshaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu, ninawapongeza sana kwa kongamano lililofanyika kule Havana Cuba, pamoja na Kamusi zile za Kiswahili kwa Kihispania na Kihispania kwa Kiswahili, ninawapongeza sana. Kazi hii iendelee, ili Kiswalihi kiendelee kukua duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kuwapongeza na kuwashukuru waasisi wetu waliofanya Taifa letu Lugha ya Kiswahili iwe Lugha ya Taifa, lakini leo imekuwa si Lugha ya Taifa, imekuwa ni Lugha ya Dunia. Tuendelee kuwaombea dua na maisha mazuri huko waliko peponi. Amina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika balozi zetu tunafundisha Kiswahili, lakini pia, ninaongezea, tufundishe na utamaduni wetu wa asili. Kwa mfano, South Korea, ndugu yetu Tunu Mayemba anajitahidi sana kufundisha Kiswahili, lakini anaeneza Utamaduni wa Mtanzania kule South Korea. Anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kwenye Bodi ya Baraza la Kiswahili. Bodi ya Baraza la Kiswahili ina wajumbe sita na mmoja kutoka Zanzibar. Ninaona sasa kuwepo na umuhimu wa kuongeza idadi ya wajumbe kutoka upande wa pili wa Muungano ili kuleta ile hamasa zaidi ya Lugha yetu ya Kiswahili kwa sababu, sasa hivi Kiswahili kimekuwa ni Lugha ya Afrika na ni Lugha ya Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wazo kwa Wizara hii, kama watashirikiana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanaokuja Tanzania kusoma basi wapate ile, kama orientation, ambayo watakuwa na Mafunzo ya Kiswahili kwa muda wa miezi mitatu mpaka sita ili kukitangaza zaidi Kiswahili. Pia, kuongeza mapato ndani ya nchi kwa hao wanafunzi wanaokuja kujifunza masomo mengine ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, tumeona kwenye bajeti kutakuwa na mapitio na kuongeza baadhi ya maneno mbalimbali ya Kiswahili. Ushauri wangu ni kwamba, tuendelee kufuata utaratibu katika kuongeza haya maneno na istilahi mpya za Kiswahili. Kwa sababu, kuna maneno tayari yamo kwenye Lahaja za Kiswahili na inasemekana kwamba, Lahaja za Lugha ya Kiswahili, kama lile neno lipo, basi lisitafutwe neno jipya kwa sababu, maneno yale tayari yapo na yanatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano wa neno “Guruguru”. Guruguru nimeambiwa ni ngurumo, lakini neno ngurumo lipo! Sasa kwa nini tena tunatafuta haya mambo ya maguruguru kuingiza kwenye Kiswahili wakati guruguru tayari ni mdudu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujitahidi lugha yetu iwe nyepesi, inayoweza kuzungumzika, inayoweza kusomesheka, inayoweza kutafsirika kwa watu wanaotaka kujifunza Kiswahili. Tukiendelea tu kujaza maneno, maneno, maneno, kwa sababu, tunayakataa maneno ya kigeni! Lugha zote zinatohoa maneno kutoka lugha nyingine. Mfano, kwa sasa kuna vitu vinavumbuliwa, sasa hivi hilo neno tutalipata wapi wakati kile kitu ni kipya na kimevumbuliwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kutoa mfano, nikichangia bajeti hii, mara nyingi ninatoa mfano kwenye Lugha yetu ya Kiswahili jinsi tulivyotohoa maneno kutoka lugha mbalimbali, Kihindi, Kiarabu, Kifaransa, Kiingereza na Lugha nyingine. Ninataka kutoa mfano mwingine leo kwa lugha nyingine, kwa nchi nyingine walivyotohoa maneno tuone kwamba, hakuna haja ya kubadilisha maneno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda kwenye Lugha ya Kingereza, kuna neno “bus”, Kifaransa “bus”, lakini ki-Mauritius ni “bis”, ki-Komoro ni “bis”, lakini kwa maana ya basi. Ninakuja neno “train”; Kifaransa “tra", lakini ki-Mauritius train, wametohoa wanaita vilevile train, wametumia kwa Kiingereza. Neno “tablet” Kingereza, “tablete” Kifaransa, tablet ki-Mauritius. Ninakuja neno ‘tea’, tea kwa maana ya tea kwa lugha tatu; Kingereza, Kifaransa na ki-Mauritius. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini “television” Kingereza, “television” Kifaransa, “television” ki-Mauritius. “Doctor" Kingereza, “Docteur” Kifaransa, “doctor” ki-Mauritius, mmetumia hapa! Tuone kwamba, kutohoa lugha za kigeni ni kawaida katika lugha katika dunia yetu. Kwa hivyo, tusiwe tunaongeza maneno magumu, mazito, yasiyoweza kutamkika, yasiyoweza kutafsirika, lugha itakuwa ngumu, lugha haitikuwa nyepesi, tutakimbiwa. Watu watakwenda kutafuta wataalam wenye lugha nyepesi, ili waweze kujifunza kuongea tu na kubadilishana maneno na mawazo kwa sababu, siyo watu wote wanakwenda kufanya mitihani; kama wataingia darasani wafanye mitihani, maneno magumu. Watu wanataka kujua kuzungumza Kiswahili, kuelewana na kufahamiana. Ninafikiri nimeeleweka (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kupongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kuwajengea uwezo wataalam wetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Khadija Hassan Aboud, muda wako ulishakwisha, lakini kwa uzito wa hoja nilikuachia dakika mbili. (Makofi)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiswahili ni ajira, tuendelee kuhamasisha vijana wetu na Wizara itenge kitengo au watu maalum wa kuwasaidia vijana wetu wa Tanzania namna ya kuzitafuta hizi fursa za ajira. Kwa sababu, wengi hawana upeo na uelewa mkubwa wa kujua hizi fursa za ajira, matokeo yake nchi ni nyingine na nchi jirani wanazipata wao wakati vijana wetu wana uwezo zaidi kuliko hao wanaokwenda kufundisha na kuwa wakalimani. Ninaomba tuwasaidie, tuweke kitengo au watu maalum wa kuwasaidia vijana wetu. Mwisho, ninawapongeza Wizara kwa andiko la kuomba kujengewa Kituo cha Utamaduni na Mambo ya Kiafrika, UNESCO. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Muda wako ulishaisha.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)