Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Ninampongeza sana rafiki yangu Mheshimiwa Profesa Kabudi kwa kuteuliwa kuiongoza Wizara hii. Siku nilipoona uteuzi wake niliamini kabisa kwamba, anaenda kurekebisha mambo yote kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake anazofanya katika kuinua michezo nchini kwetu. Ninamuomba Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa iliyofanywa na Simba; mimi ni Mwanayanga, lakini kwa kazi kubwa iliyofanywa na Simba wanastahili na wao kupewa ndege, ili waende kwenye fainali huko Morocco. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimewaona viongozi wa Bodi ya Ligi na nimemwona Rais wa TFF, ninampongeza sana. Nimemwona Rais Mstaafu, Bwana Tenga; ninadhani Bwana Tenga ni mtu wa kuigwa sana kwenye hii Tasnia ya Michezo. Kwa kweli, ni kiongozi ambaye alifanya kazi yake vizuri na akastaafu na bado wanamtumia, lakini ni mtu anayeheshimika sana kwenye Tasnia ya Michezo. Sasa ninadhani na wale walioko kwenye madaraka waige mfano wa jinsi gani Mzee Tenga aliongoza michezo yetu hapa Tanzania, vinginevyo watamaliza vipindi vyao halafu watakuwa ma-oya-oya huko mtaani, hawaeleweki na hawaheshimiki kwa kazi walizozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuuliza kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kabudi, Waziri, na nilikuona, kutokana na mgogoro uliopo kwenye timu zetu hizi kubwa mbili, nilimwona alitoka saa nne usiku kwenye kikao. Baada ya kutoka mle shaah! Mpaka leo hatujajua kilichotokea kule. Ninatanguliza maneno haya, ili uyajue, leo nitashika Shilingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpira wa Simba na Yanga. Timu ya Simba na Yanga kwenye nchi hii ndiyo burudani pekee iliyobaki kwa watu wote. Sasa wanatambua kabisa ipo migogoro, lakini hata kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Profesa Kabudi sijaona mahali ambapo anataja. Ikiwa Rais mwenyewe anafadhili mpaka anatoa hela zake mfukoni kuwapa vijana hamasa, halafu wanaona huu mchezo tuendelee kusikia tu ngonjera za huyu na huyu! Ninamtangulizia kabisa shilingi Mzee Profesa Kabudi, ninaondoka nayo. Kama hatakuja na taarifa sahihi, alichokisikia akieleze hili ndilo Bunge la wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa tunasikia mitandaoni na wewe mwenzetu aliyeteuliwa kwenda kutuwakilisha amesikia sirini, halafu analeta taarifa tumpitishie bajeti, tunaacha kuelewa kinachoendelea. Sisi tukirudi huko majimboni kwetu na sisi tuwe tena watu wa mitandao? Leo kama hatatoa taarifa sahihi nitashika Shilingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamini Simba hawana makosa, Yanga hawana makosa, lakini kinachoendelea, nani anayetakiwa kutueleza taarifa sahihi? Tunaona kama mchezo, eeh! Kesi imeenda CAS, imerudi CAS imekuja huku, kabla hajamsikiliza mlalamikaji anatangaza mechi, anacheza Bodi ya Ligi, inacheza Yanga? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka kujua, Mheshimiwa Profesa Kabudi yeye alienda, alisikiliza pande zote mbili, Simba na Yanga. Sitaki kusema Yanga ina makosa wala Simba ina makosa, Waziri aliyesikiliza atupe majibu sisi Wabunge, ili tukawaeleze watu wetu. Michezo ni furaha, Simba na Yanga ni part ya maisha ya kuburudisha Watanzania. Kwa hiyo, akija bila maneno, leo nitamzingua Mheshimiwa Profesa Kabudi, lazima aje na taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania tumepata heshima ya kuandaa AFCON, halafu dunia yote itaangalia AFCON imeandaliwa Tanzania. Halafu tunakuwa na viongozi wahuni tu, wanaamua wanavyotaka, hatuwezi kwenda kwa design hiyo. Hapana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunaweza kuwa Marais wa TFF, wote humu tunaweza kuwa Viongozi wa Bodi ya Ligi. Hata mimi ninaweza kuteuliwa, lazima niwe wazi, siyo tu kama tumempa mtu kuongoza familia yake. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, kuliko kulitia aibu Taifa hili tunakokwenda kwenye michezo yetu, ni lazima aje na taarifa Bunge tufahamu. Asipokuja nayo, leo nitaondoka na Shilingi. Mimi ni Daktari, yeye ni Profesa. kwa hiyo, Mzee ajiandae na yeye mwenyewe amenipandisha kuniita Profesa, ananiita Profesa. Kwa hiyo, leo nitamzingua kiprofesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie, nishauri; Bodi ya Ligi isiongozwe na TFF, iwe independence, Wazungu wanasema ijitegemee. Tunaona...
MBUNGE FULANI: (Hapa hakusikika vizuri)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: …hivyo hivyo! independent, hivyo hivyo. Tunaona sasa inapokea maelekezo tu kutoka kwenye TFF. Kwa hiyo, ninaomba sana tuache na tuunde Bodi ya Ligi inayojitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwenye Mfuko wa Wasanii; nimewaona rafiki zangu wasanii. Unajua tatizo huko Serikalini huwa wanakurupuka, hawajui biashara, tuna mipango mizuri ya pesa, lakini biashara hawaifahamu. Tukitoa mawazo, mimi nimeshiriki sana kuzitafuta zile pesa wasaniii wanajua, ukifika muda wa pesa wanakurupuka na shule. Sasa, hili ndiyo tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Wasanii, pesa alizotoa Dkt. Mama Samia, leo tukiuliza kuna shilingi ngapi au waliowakopesha wamerudisha shilingi ngapi? Wako hapa! Kuchukua hela leo na wengine kuoa, kununua magari, starehe, wengine zimewaua na kuwaua! Badala ya kuwapa watu wanaoandaa filamu, wanaoandaa muziki, ma-producer, wanaenda kuwapa watu wanaoonekana kwenye TV kwa kuangalia shape! Hii haifai! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa yote imeisha. Wako hapa, tuwaulize; halafu tunaanza kuwasingizia masharti yamekuwa magumu mpaka walete hati. Hakuna pesa inatoka kirahisi, pesa lazima iwe na masharti ili tupate marejesho. Hatuwapi hela ya kwenda kula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kuwapa watu wanaoandaa filamu, msanii anayeonekana kwenye TV wengi wao wanamalizana na ma-producer, analipwa cash yake anaondoka. Badala ya kuwapa wale waandaaji wa muziki, kuwapa waandaaji wanaoandaa filamu, wanaenda kuwapa watu wanaoonekana kwenye TV. Waziri aniambie kwenye taarifa yake, zile shilingi milioni 50, milioni 40 tulizotoa, aje na majibu, wangapi wamerudisha? Hata mmoja na anazifanyia nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukakague biashara zao, wote wamenunua Kluger, wamenunua Alphard, zimeisha zote hamna hata mia. Sasa wangetuchukua tukawashauri, tuliozoea maisha ya kitaa, leo hii tungekuwa na wasanii mabilionea. Kwa sababu, ukimwezesha mwandaaji ni sawa umemwezesha yule anayeonekana kwenye TV. Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa, akija hapa aje na majibu yanayoeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais na ninaendelea kuwaombea Simba wakafanye vizuri. Unapoenda kuiwakilisha nchi kwenye fainali sisi wote tunaungana, kama Taifa moja. Serikali iangalie ndege na kama kuna nafasi, ninaomba lift kabisa, ninatanguliza, nikashangilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Profesa Kabudi, yeye ni mzee, mwalimu mbobevu wa Kitivo cha Sheria, nina imani anaweza kurekebisha hii Wizara. Ninajua yeye ni Mwalimu mzuri, sidhani kama ata-fail. Aki-fail, kama kuna kitu kinamsumbua mimi nipo, ninaweza kumshauri bila malipo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)