Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami leo niweze kuchangia katika Taarifa hii ya Bajeti au Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo. Awali ya yote ninapenda nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa jitihada kubwa anazofanya na uwekezaji mkubwa anaoufanya katika Sekta ya Michezo, Utamaduni na Sanaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mzee Wangu, Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi. Kwa kweli, anaiongoza vizuri Wizara hii kwa ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, Katibu Mkuu Ndugu Gerson Msigwa, pamoja na Naibu Katibu Mkuu Methusela. Pia, ninazipongeza taasisi zote zinazosimamia michezo yetu na sanaa na utamaduni, pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kazi kubwa inayoifanya katika kuboresha tasnia zote ambazo ziko chini ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninapenda nichangie upande wa michezo. Hoja ya kwanza kwa kweli, ninapenda kama nilivyosema hapo mwanzo, nimempongeza Mheshimiwa Rais na kwa kweli, Rais wetu anastahili pongezi. Kwa sababu ku-host CHAN Mwaka 2024, AFCON Mwaka 2027, kuwa na timu ambazo zinafanya vizuri za Mpira wa Miguu, Under 17, Under 20, kwenye Golf, kwenye Cricket, kwenye Women’s Football ya Afrika kwa kweli, ni hatua kubwa ambayo imefikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina pendekezo; kwa kuwa, Mheshimiwa Rais wetu ameshirikishwa katika kutoa tuzo mbalimbali kwa wasanii, wanamichezo na wadau wengine wa tasnia ambazo ziko chini ya Wizara hii, mzee wangu Mheshimiwa Profesa Kabudi, ninafikiri tuandae tuzo kwa Mheshimiwa Rais pia, katika kumtia moyo kuendelea kuzisimamia tasnia hizi na kuhakikisha uwekezaji mkubwa unakuwepo katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kuipongeza Klabu ya Simba, ambayo imefikia hatua ya kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Sanasana ninampongeza pia, ndugu Mo Dewji kwa uwekezaji mkubwa ambao amekuwa akiufanya katika Klabu ya Simba na hivyo kuiwezesha kushika nafasi ya nne kwa ubora Barani Afrika katika Vilabu vya Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio ya Simba yamelifikisha Taifa letu kuwa na ligi namba nne, msukumo mkubwa umetoka Simba na mapinduzi makubwa katika soka la nchi hii yametokea Simba kutokana na uwekezaji wa Mo Dewji. Siwalazimishi wana-Simba wajenge sanamu kule Mo Arena Bunju wala pale kwenye club yao ya Msimbazi, lakini nafikiri wanaweza wakafanya jambo hata kumpa tuzo Mheshimiwa Dewji, ninasema Mheshimiwa kwa sababu alishawahi kuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo, siku ya tarehe 8 Machi tulitarajia kwamba kungekuwa na mechi ya lingi kuu, mechi namba 184. Mechi hii ilifutwa lakini baada ya kufutwa jana tumepata taarifa kwamba imepangiwa kuchezwa tarehe 15 mwezi Juni. Hata hivyo nisikitike kusema, kwamba mamlaka zetu za mchezo wa mpira wa miguu hazijatutendea haki, kwa sababu hawajatupa taarifa yoyote kwamba kilitokea nini mpaka kupelekea mechi ile isichezwe siku ya tarehe 8; lakini pia hatujapewa taarifa ni hatua gani zimechukuliwa kwa wote waliohusika na mechi ile kutokuchezwa tarehe 8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri, pamoja na kutangaza tarehe 15 mechi itachezwa mwezi Juni tunatakiwa tufahamu nini kilitokea na hatua gani zimechukuliwa. Hii itapelekea kuhakikisha kwamba matukio yasiyokuwa na afya katika mchezo wa mpira wa miguu hayatokei tena siku zijazo na ninataka nikwambie, kwamba timu zetu za Simba na Yanga ni timu maarufu sana Afrika Mashariki na Kati. Kuna wakati fulani nilisafiri kwenda Bujumbura nikafika mtaa mmoja unaitwa Buyenzi, siku hiyo mechi ya Simba na Yanga ilikuwa inachezwa, timu moja ikafunga goli, mtaa wote ulishangilia utafikiri upo Kariakoo Jijini Dar es Salaam. Kwa hiyo ni timu zenye hadhi kubwa na mambo yetu yanatakiwa yaende kikubwa kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo ninapenda kulizungumza ni kuhusu taasisi simamizi ya viwanja. Niiombe Wizara yetu ya Sanaa, Utamaduni, Habari na Michezo iteue watu makini kwenye hii taasisi ili hivi viwanja vyetu viweze kusimamiwa vizuri. Serikali imetenga fedha nyingi na inakarabati kwa kutumia fedha nyingi na kujenga viwanja. Ukienda pale Benjamini Mkapa ukarabati unaendelea, ukienda kule Zanzibar Kizimkazi matengenezo ya uwanja yanaendelea na viwanja vingine ambavyo vitatumika kwa ajili ya mashindano mbalimbali ikiwemo mashindano ya AFCON mwaka 2027. Kwa hiyo ninaomba hii taasisi simamizi iteuliwe watu madhubuti; sio kama wale ambao wametuletea aibu siku ile ya mechi ya Simba na Al Masry, uwanja ukawa hauchezeki, mpira haunogi kabisa pale uwanjani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia hata siku ile ya tarehe 7 inadaiwa kwamba kulikuwa na watu wameingia wanazuia watu wengine kufanya mazoezi na kadhalika, lakini TFF nao katika vile viwanja ambavyo vinatumika kwa ajili ya mchezo wa mpira wa miguu kwa ligi mbalimbali ambazo zinatambuliwa na TFF watoe mafunzo kwa hawa watendaji watakaopatikana kwa taasisi hii simamizi; watoe mafunzo kuhusu zile kanuni za mchezo wetu wa mpira wa miguu na michezo mingine. Wapewe mafunzo ya kutosha ili kuhakikisha kwamba basi hivyo viwanja vinasimamiwa vizuri ili fedha nyingi ambazo zimewekezwa katika viwanja hivyo ziweze kuleta tija na ufanisi kwa michezo yetu yote hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)